Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Taifa, Jaji Mstaafu Mary Longway. (Picha na NEC)
Katibu wa Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Taifa, Ndugu Emmanuel Kawishe (kulia) akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo (hawapo pichani), kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Mstaafu, Mary Longway. (Picha na NEC)
Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Taifa wakiendelea na kikao kilichofanyika leo katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jijini Dar es Salaam. (Picha na NEC)

Mwandishi wetu

Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Taifa, imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiendelee kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga yaliyokitaka chama hicho kusahihisha makosa yaliyotendeka na kuomba msamaha hadharani kwa kosa la kimaadili walilotenda.

Uamuzi huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji Mst. Mary Longway baada ya kakio cha kamati hiyo kupitia na kujadili rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Maadili Jimbo la Uchaguzi Ukonga, iliyowasilisha na Chadema Septemba 5, 2018 ikiitaka kamati hiyo itengue uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Jimbo.

Alisema kwa mujibu wa vielelezo vilivyoambatishwa katika Rufaa hiyo, Kamati ya rufaa imefikia maamuzi ya kuwa rufaa hiyo imewasilishwa nje ya muda wa saa 48 kinyume na maelekezo ya kipengele cha 5.7 (b) cha Maadili tajwa.

“Rufaa iliyowasilishwa yenye Kumb. Na. CDM/ILALA/MAADILI/2018/28 ya tarehe 5 Septemba, 2018 iliyopokelewa Tume tarehe 7 Septemba..Imewasilishwa nje ya muda wa saa 48 kinyume na maelekezo ya kipengele cha 5.7 (b) cha Maadili tajwa. Hivyo, Kamati inaelekeza kuwa mrufani aendelee kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo.”, alisema Jaji Mst. Longway.

Kwa mujibu wa uamuzi wa Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga, Chadema kimeonywa kuhakikisha kuwa kinafuata Kanuni na Taratibu za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 na kutekeleza maamuzi hayo ndani ya saa 48 tangu kutolewa na adhabu hiyo.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga Jumanne Shauri mnamo Agosti 27, 2018 alipokea malalamiko na kupitia utetezi wa Chadema na kujiridhisha kuwa Chadema kilitumia kiongozi wa dini kumpigia kampeni mgombea wa chama hicho kinyume na kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.

Msimamizi huyo wa Uchaguzi aliongeza kuwa “Dr. Makongora Mahanga akiwa kiongozi wa Chadema, siku ya kampeni tarehe 25/8/2018 alitumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji dhidi ya mgombea wa CCM, ikiwa pia ni kinyume na kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015” aliongeza taarifa ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Jimbo hilo”

Mbali na uamuzi juu ya rufaa hiyo, Kamati hiyo pia imepitia barua ya tarehe 5 Septemba, 2018 iliyowasilishwa Tume tarehe 7 Septemba, 2018 kupinga maelekezo ya Kamati ya Maadili Jimbo la Ukonga yaliyokiagiza Chadema kuwasilisha ndani ya Saa 48 kuanzia tarehe 4 Septemba, 2018 vielelezo vilivyothibitishwa na Mamlaka ya Mawasiliano na wataalamu wa lugha ya Kikurya ili kutoa maamuzi ya shauri husika.

Akizungumzia barua hiyo, Jaji Mst. Longway alisema baada ya kupitia vielelezo na kujadili barua husika, imeamuliwa kuwa rufaa hiyo imekosa sifa kwa kuwa hakuna maamuzi yaliyofanywa na Kamati ya Maadili Jimbo la Ukonga.

Kutokana na jambo hilo, Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Taifa imekielekeza Chadema kuwasilisha vielelezo Kamati ya Maadili ya Jimbo la Ukonga kwa uamuzi kama ilivyoelekezwa na Kamati husika.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: