Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa (CCM), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Kushoto), akiwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, Mhe. Felista Bura (Katikati) wakiingia kwenye ukumbi ulipofanyika Mkutano Mkuu Maalumu wa Jimbo la Kondoa ambapo Dkt. Kijaji, aliwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Kipindi cha Miaka 3 ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano katika Jimbo lake.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Comrade Godwin Mkanwa (kushoto) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (katikati aliye vaa koti la njano), wakipokelewa na kundi wa wanachama wa chama hicho kwa kucheza ngoma wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kipindi cha miaka mitatu ya Uongozi wa Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, katika Jimbo la Kondoa.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa (CCM), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili Kushoto), akiimba wimbo wa hamasa wa CCM alipowasili ukumbini katika Kata ya Pahi, wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Jimbo la Kondoa ambapo Dkt. Kijaji, aliwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Kipindi cha Miaka 3 ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano katika Jimbo lake. wa tatu kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma Comrade Godwin Mkanwa ambaye alikuwa mgeni rasmi.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa (CCM), Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi-CCM, katika kipindi cha miaka 3, katika Jimbo la Kondoa, wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Jimbo la Kondoa uliofanyika katika Kata ya Pahi, Kondoa, mkoani Dodoma.
Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Amina Mollel, akifuatilia kwa makini matukio ya uwasilishwaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Kipindi cha Miaka 3 ya Serikali ya Awamu ya Tano katika Jimbo la Kondoa. Walioketi karibu naye ni wazazi wa Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Mzee Abdallah Kijaji na mkewe Aziza Selemani, katika Kata ya Pahi, Kondoa, Dodoma.

Na Mwandishi wetu, Kondoa

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa mkoani Dodoma, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu, maji, afya, miundombinu ya barabara na huduma nyingine za kijamii zimeimarika zaidi katika Jimbo la Kondoa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Dkt. Kijaji ameeleza hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Jimbo lake katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Jimbo la Kondoa uliowashirikisha zaidi ya wajumbe 1,200, uliofanyika katika Kata ya Pahi, wilayani Kondoa.

Ameyataja baadhi ya mafanikio makubwa kuwa ni kuchimba na kukarabati visima virefu na vifupi vya maji vipatavyo 56 pamoja na kukarabati visima vingine 4 vilivyoharibika zaidi ya miaka 15 iliyopita ambapo zaidi ya sh. bilioni 1.8 zimetumika, hatua iliyochangia wananchi zaidi ya laki moja katika Jimbo la Kondoa kuanza kupata huduma ya uhakika ya maji.

Kuhusu Sekta ya Elimu, Dkt. Kijaji ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mbili mpya za Sekondari katika Kata za Hondomairo na Bumbuta kwa gharama ya sh. milioni 140.5, ambazo zitaanza kuchukua wanafunzi kuanzia mwezi Januari, 2019 pamoja na kujenga na kukarabati vyumba ya madarasa, mabweni na nyumba za walimu, kwenye shule mbalimbali za Sekondari na msingi.

Alisema kuwa hatua hiyo imesababisha kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi kutoka asilimia 37 mwaka 2014 hadi asilimia 68 mwaka jana na kwa upande wa Sekondari, ufaulu umepanda kutoka asilimia 41 hadi asilimia 79.

Katika Sekta ya Afya, Dkt. Kijaji amebainisha kuwa katika jimbo lake, Serikali inajenga vituo vipya vya afya vinne kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 2.3 pamoja na zahanati kadhaa hatua ambayo amesema vitakapo kamilika, changamoto za upatikanaji wa huduma za afya zitapungua kwa kiasi kikubwa.

"Tangu uhuru hadi mwaka 2015, sawa na miaka 54, Jimbo la Kondoa lilikuwa na vituo vya afya vitatu tu, lakini katika kipindi cha miaka mitatu cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, tunajenga vituo vya afya vinne, na kupanua huduma za afya katika Kituo kimoja cha afya ili kitoe huduma ya upasuaji, haya ni mafanikio makubwa" alisema Dkt. Kijaji.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi aliyealikwa kwenye Mkutano Mkuu huo maalumu wa Jimbo la Kondoa, Dkt. Bashiru Ally, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma, Bw. Godwin Mkanwa, amempongeza Dkt. Ashatu Kijaji, kwa kutekeleza kwa umakini na umahili mkubwa ahadi za Chama hicho kwa wananchi.

Bw. Mkanwa ametoa wito kwa watendaji wa Serikali mkoani mwake kuendelea kutatua kero zinazoikabili jamii ikiwemo migogoro ya ardhi na upatikanaji wa huduma muhimu za jamii pamoja na kuwataka viongozi wa Chama na Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa za mapato na matumizi ya vijiji vyao.

Baadhi ya wanachama walioshiriki mkutano Mkuu Maalumu huo wa CCM Jimbo la Kondoa, wameeleza kuridhika na utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye maeneo yao na kumpongeza Mbunge wao, Dkt. Ashatu Kijaji kwa kusimamia ahadi zake hatua ambayo imesababisha kuonekana kwa maendeleo kwenye kata zao ikiwemo ubora wa huduma za afya, maji, ujenzi wa barabara na madaraja pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Jimbo la Kondoa linaundwa na Tarafa tatu, Kata 21, vijiji 84, vitongoji 386 na kuna matawi 172 ya Chama cha Mapinduzi, na kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Jimbo hilo lina idadi ya watu wapatao 234,185.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: