Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo.

Kuelekea Tanzania ya viwanda, jambo moja kubwa liko wazi kwamba Tanzania inahitaji nishati ya kutosha kuwezesha ujenzi wa viwanda vingi na kuipeleka Tanzania kufikia uchumi wa kati. Moja ya nishati ambayo Tanzania imebarikiwa kwa wingi ni gesi asilia ambapo tayari ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 umefanyika katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani. Ugunduzi huu umefanyika katika maeneo ya nchi kavu pamoja na maeneo ya bahari ya kina kirefu.

Juhudi nyingi zinafanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kutimiza adhma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati. Moja ya juhudi hizo ni maonesho mbalimbali yanayolenga kuisambaza nadharia ya Tanzania ya viwanda na kuchochea uwekezaji zaidi katika sekta viwanda.

Juma hili tumeshuhudia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan akifungua rasmi maonesho ya viwanda mkoa wa Pwani. Katika ufunguzi huo Makamu wa Rais aliliasa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kusambaza gesi zaidi viwandani ambapo alisema “TPDC tunataka gesi zaidi viwandani, tuleteeni”.

Kauli hii ya Makamu wa Rais ni chachu zaidi kwa TPDC kuendelea na jukumu lake la kutafuta, kuendeleza na kusambaza gesi asilia hapa nchini, anasema Afisa Uhusiano wa TPDC, Malik Munisi.

Hadi sasa kuna viwanda vipatavyo 40 vinavyotumia gesi asilia katika uzalishaji wake, na TPDC inaendelea na mazungumzo na viwanda takribani saba maeneo ya Mkuranga ambavyo vina mahitaji ya gesi asilia, anaongeza Malik Munisi. Nae Mhandisi Limi Lagu kutoka Idara ya Mkondo wa Juu aliongeza kwamba katika kuchochea uchumi wa viwanda, TPDC imetekeleza mradi wa kutoboa bomba kubwa la gesi maeneo ya Mwanambaya, Mkuranga ili kuwezesha wateja zaidi wa viwandani kuunganishiwa gesi asilia. 

Mhandisi Limi aliendelea kwa kusema kuwa “mradi huu umehusisha kutoboa bomba kitaalamu bila kuzuia gesi kwa kutumia teknolojia ya hot tapping na kisha kutandaza bomba la kilometa 3. kuelekea kiwanda cha Lodhia Steel”. Kwa mujibu wa Mhandisi Lagu, bomba hilo lina uwezo wa kuunganisha viwanda vingi zaidi na hivyo wawekezaji wanahimizwa kuja kuwekeza zaidi maeneo hayo na kutumia nishati ya gesi asilia.
Mhandisi Limi Lagu (mwenye suti jeusi) akitoa elimu ya gesi asilia na matumizi yake kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda la TPDC katika maonesho ya Viwanda Pwani.

Gesi asilia viwandani inaweza kutumika kwa namna tofauti, kwanza inaweza kutumika kama chanzo cha nishati ambapo inaweza kuzalisha umeme wa kutumia kiwandani, pili inaweza kutumika kwa ajili ya kupashia moto “heating” kama mbadala wa nishati nyingine kama mafuta mazito, kuni au umeme katika uzalishaji wa bidhaa viwandani au majumbani mfano inavyotumika katika viwanda vya saruji. 

Vile vile gesi asilia inaweza kutumika viwandani kama malighafi katika viwanda vya kemikali za petroli ambavyo huzalisha mbolea, plastiki, methanol na kadhalika. Kuna faida nyingi katika kutumia gesi asilia ambapo kwanza ni nishati rafiki kwa mazingira hivyo kwa kutumia gesi asilia unaokoa mazingira, pili gesi asilia ni nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati kama mafuta mazito na umeme lakini pia gesi asilia inaokoa matumizi ya fedha za kigeni kuagiza mafuta mazito nje ya nchi. Tanzania ya viwanda inawezekana na TPDC iko mstari wa mbele kuchochea Tanzania ya Viwanda.

Bi Neema Maganza, Mjiolojia kutoka TPDC (mwenye suti ya bluu) akifafanua jambo kwa baadhi ya wananchi waliotembelea banda la TPDC katika maonesho ya viwanda Pwani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: