Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari zilizochapishwa katika Gazeti la Tanzania Daima la tarehe 26 Oktoba, 2018 toleo namba 4979 na toleo namba 4982 la tarehe 30 Oktoba, 2018 zenye vichwa vya habari “Madudu yaibuka TRA” na “Barua za madudu TRA zavuja”. Habari inayofanana na hizi, ilisambazwa pia katika baadhi ya Mitandao ya Kijamii ikiwa na kichwa cha habari "PCCB Tanzania, to investigate the two tax collectors TRA and ZRB". 

Habari hizi zinadai kuwa, Mfumo wa Ulipaji Kodi kwa Njia ya Kielektroniki – Electronic Revenue Collection System (e-RCS) umezimwa na kuhujumiwa na baadhi ya Maofisa wa Serikali kwa lengo la kujinufaisha na kuzorotesha juhudi za ukusanyaji mapato ya Serikali.

Ukweli ni kwamba, mfumo huo haujahujumiwa wala kuzimwa isipokuwa kuna maboresho ya kiufundi ambayo yanaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa, unakidhi malengo yaliyokusudiwa. 

Katika kipindi hiki ambacho maboresho yanaendelea kufanyika, Kampuni za Simu pamoja na Benki mbalimbali zinaendelea kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na hakuna upotevu wowote wa mapato kama ilivyoripotiwa na Gazeti la Tanzania Daima na baadhi ya Mitandao ya Kijamii.

TRA inapenda kuuhakikishia umma kwamba, hakuna Ofisa yeyote wa Serikali mwenye nia ya kuhujumu mfumo huo kwa lengo la kujinufaisha na kuzorotesha juhudi za Serikali za ukusanyaji wa mapato. 

Mamlaka ya Mapato Tanzania inatoa wito kwa vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari kufanya utafiti wa kina kabla ya kuandika habari na kuzingatia weledi wakati wote wanapotimiza majukumu yao ili kuepuka upotoshaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: