Na Mwandishi Wetu.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewakamata watu wawili mwanamke na mwanaume kwa kosa la kugushi Risiti za Kielektroniki za EFD katika maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Richard Kayombo, amesema kuwa, watuhumiwa hao ni Doreen Urassa (40) mkazi wa Kunduchi na Raymond Alexander (31) mkazi wa Kinondoni Mkwajuni jijini hapa.

"Tarehe 4 Oktoba, 2018 majira ya saa 1 jioni, tulifanikiwa kuwakamata watu wawili maeneo ya Sinza Mori wakiwa wanagushi risiti za EFD. Watuhumiwa hawa tutawafikisha mahakamani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria", alisema Kayombo.

Kayombo ametoa wito kwa watu wote wanaojishughulisha na makosa hayo kuacha mara moja kwa kuwa TRA itaendelea kufanya msako mkali na mtu yeyote akibainika anagushi risiti, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Mkurugenzi Kayombo amewaomba wasamalia wema waendelee kutoa taarifa za kuwafichua wanaogushi risiti na kuwahakikishia kuwa, majina yao hayatatajwa popote.

“Mamlaka haitamvumilia mtu yeyote anayejaribu kukwamisha ukusanyaji mapato ya serikali iwe kwa kugushi risiti au biashara ya magendo au njia nyingine yoyote ya udanganyifu. Hivyo, tunawaomba wasamalia wema waendelee kutupa ushirikiano kwa kuwafichia watu wadanganyifu na tunawahakikishia kutunza siri kwa kutoyataja majina yao popote pale”, alifafanua Kayombo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na zoezi la kuwasaka watu wote wanaojishughulisha na vitendo vya kugushi risiti ikiwa ni pamoja na kukamata biashara za magendo ambapo wanaobainika hufikishwa mahakamakani kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: