Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba akitoa taarifa ya ukusanyaji, Ukoboaji na uuzaji wa kahawa Mkoani Kagera katika msimu wa mwaka 2018/2019 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa kahawa katika ukumbi wa ELCT Mjini Bukoba. (Picha Na Mathias Canal-WK)

Na Mathias Canal-WK, Bukoba-Kagera.

Imebainika kuwa pamoja na changamoto zilizojitokeza katika msimu wa kahawa wa mwaka 2018/2019 lakini bado mfumo wa uuzaji wa kahawa kupitia ushirika umekuwa wa manufaa kwa mkulima kutokana na mkulima kupata uhakika wa kilo za kahawa alizozipeleka chamani tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Manufaa hayo yamejili kutokana na kuingia mikataba ya kuuza moja kwa moja, ambapo matarajio ya serikali ni kuhakikisha kuwa mkulima analipwa malipo ya awali na kiasi kingine kubaki kwa ajili ya kuendelea kukusanya kahawa na kufanya maandalizi ya malipo ya pili.

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba amebainisha hayo Leo tarehe 6 Octoba 2018 wakati akitoa taarifa fupi ya ukusanyaji, Ukoboaji na uuzaji wa kahawa Mkoani Kagera katika msimu wa mwaka 2018/2019 hadi kuishia tarehe 2 Octoba 2018 kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) kwenye mkutano wa wadau wa kahawa.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi ELCT Mjini Bukoba na kueleza kuwa ubora wa kahawa umeongezeka kwa kiasi kikubwa tofauti na misimu iliyopita.

Waziri Tizeba alizitaja changamoto zinazovikabili vyama vya ushirika kwenye zao la kahawa kwa msimu wa mwaka 2018/2019 kuwa ni pamoja na Bei za mnadani, Kahawa kununuliwa kwa kiwango kidogo mnadani na wakati mwingine kutonunuliwa kabisa.

Kuwepo kwa taarifa za upotoshaji kwa wakulima toka kwa Walanguzi za kuzuia wakulima kukusanya kahawa yao kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi kuwa wao (Walanguzi) watanunua na kuwapatia bei nzuri na Kuwepo kwa katizo la umeme mara kwa mara linalopelekea ukoboaji wa kahawa kutofanyika kwa wakati (hususani Wilayani Ngara).

Aidha, aliutaja mkakati wa kukabiliana na changamoto hizo kuwa ni pamoja na kuuza kahawa kupitia mnada wa Moshi na mauzo ya moja kwa moja nje ya nchi “Direct Export” ambao umeonesha kuwa na bei nzuri ukilinganisha na ile inayotolewa mnadani Moshi, na Kuomba mkopo wa nyongeza toka TADB kwa ajili ya kuwalipa wakulima malipo yao ya Awali.

Alisema Chama Cha Ushirika cha Karagwe KCU wanatarajiwa kupata mkopo wa Tshs. 2,000,000,000/= kwa wiki hii na kiasi cha Tshs. 2,000,000,000/= kinaendelea kushughulikiwa ili kiweze kutolewa wiki ijayo ambapo wanatarajiwa kupata malipo ya mauzo ya kahawa yao kwa wiki ijayo kiasi cha Tshs Bilioni 2.1

Mikakati mingine ya kukabiliana na changamoto ya zao la kahawa ni pamoja na Vyama kuingia mikataba mbalimbali ya kuuza kahawa moja kwa moja nje. KDCU Ltd wana mikataba ya mauzo nje yenye thamani ya Tshs 20,819,815,820.66 ambapo malipo yake yanatarajiwa kulipwa kuanzia wiki hii. Kwa KCU Ltd wana mkataba wa Tshs Bilioni 1.3 na wanatarajia kuingia mikataba mingine na wanunuzi wengine kwa wiki ijayo.

Dambamba na jitihada za kupatikana kwa umeme wa uhakika katika kiwanda kilichoko Wilayani Ngara zinaendelea kufanyika kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Katika hatua nyingine alieleza kuwa mpaka sasa Kahawa iliyoko ghalani ni Kiasi cha Kilo 3,000,464 za kahawa maganda ambayo ilikuwa bado kukobolewa huku Kilo 8,191,867 za kahawa safi kilikuwa bado hakijauzwa na kilikuwepo kwenye maghala ya vyama.

Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa ameanza ziara ya kikazi Mkoani Kagera kuanzia Leo tarehe 6 mpaka tarehe 9 Octoba 2018 ambapo pamoja na mambo mengine lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua Maendeleo ya zao la kahawa Mkoani humu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: