Na Khamisi Mussa.

Serikali ya Tanzania imewasilisha bungeni taarifa ya hali ya Dawa ya Kulevya nchini kwa mwaka 2017 ambayo inaitaja mikoa minane inayoongoza kwa kilimo cha bangi huku mkoa wa Mara ukiongoza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliitaja jana Ijumaa Novemba 16, 2018 mikoa hiyo kuwa ni Mara, Arusha, Njombe, Tanga, Simiyu, Rukwa, Geita na Morogoro.

Hata hivyo, alisema kiasi cha bangi kilipungua kutoka tani 68.23 kwa mwaka 2016 na kufikia tani 52.19 kwa mwaka 2017.

Amesema ukamataji wa mirungi uliongezeka kutoka tani 21.6 kwa mwaka 2016 hadi kufikia tani 67.8 mwaka 2017 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya mara tatu.

Amesema lakini idadi ya watuhumiwa ilipungua kutoka 2,397 mwaka 2016 hadi 1,797 kwa mwaka 2017 ikichangiwa na sababu ya watuhumiwa wengi kukamatwa na kiasi kikubwa cha mirungi na baadhi ya mirungi kukamatwa bila wahusika kuwepo baada ya kuitekeleza.

Mhagama amesema kiasi cha cocaine kilichokamatwa kilipungua kutoka kilo 18.52 katika mwaka 2016 hadi kufikia kilo 4.143 kwa mwaka 2017.

Amesema watuhumiwa waliokamatwa kwa kujihusisha na cocaine walipungua kutoka 263 kwa mwaka 2016 hadi kufikia 243 kwa mwaka 2017.

Hata hivyo, amesema kuna ongezeko la dawa za kulevya aina ya heroin zilizokamatwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya baada ya kuimarisha udhibiti wa dawa zinazopita mipakani na hivyo kupunguza uingizaji wa dawa nchini.

Amesema heroin ambayo ilikamatwa nchini katika mwaka 216 ni kilo 42.26 ikilinganishwa na kilo 185.557 zilizokamatwa mwaka 2017 ikiwa ni mara nne zaidi na kiasi hiki kikubwa kuwahi kukamatwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Amesema idadi ya watuhumiwa waliokamatwa wakijihusisha na heroine iliongezeka kutoka watu 716 kwa mwaka wa fedha 2016 hadi kufikia watu 1,005 kwa mwaka 2017.

Aidha amesema mashamba ya mirungi ya ukubwa wa ekari 64.5 yaliteketezwa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: