Wachezaji wa Bunge Sports Club, kutoka kushoto Flatei Massay, Venance Mwamoto na Angelina Mabula wakifanya mazoezi Uwanja wa Jamhuri leo.
 Mbunge wa Manyoni mashariki na Mkimbia wa timu ya Bunge Sports Club, Daniel Mtuka akifanya mazoezi Uwanja wa Jamhuri.
 Mchezaji wa timu ya Bunge ya Netbal, Agness Marwa akimiliki mpira wakati wa mazoezi ya timu hiyo leo.
 Kocha wa timu Netiboli, Eleonora Mongi (mwenye mpira) akizungumza na wachezaji wake.
 Wachezaji wa mpira wa Miguu wa Bunge FC 'Ndugai Boys' wakifanya mazoezi Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo tayari kwa kushiriki michuano ya Mabunge ya Afrika Mahsriki Bujumbura Burundi mapema mwezi ujao.

 Naibu Waziriu wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na mchezaji wa timu ya Mpira wa Pete ya Bunge , Dk. Angelina Mabula akimiliki mpira mbele ya wachezaji wa timu ya Chuo cha Mipango wakati wa mchezo wa kirafiki baina ya timu . Bunge Queens inajiandaa na michezo ya Mabunge ya Jumuia ya Afrika Mashariki itakayofanyika Bujumbura Burundi kuanzia Desemba mosi mwaka huu. (Na Mpigapicha wetu).
Mchezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Bunge "Ndugai Boys", William Ngeleja akiambaa na mpira wa kati wa mazoezi ya timu hiyo inayojiandaa na michuano ya Mabunge ya Jumuia ya Afrika Mashariki jijini Bujumbura Burundi mapema mwezi ujao. Ngela pia ni Mwenyekiti wa Bunge Sports Club. (Na Mpigapicha wetu).

Na Mwandishi wetu, Dodoma.

TIMU ya Bunge Sport Club imeendelea na mazoezi makali katika uwanja wa Jamhuri Jijini hapa kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya michezo ya Wabunge wa Afrika Mashariki yanayotarajiwa kuanza Desemba mosi mwaka huu Jijini Bujumbura nchini Burundi.

Gazeti hili limefika katika uwanja wa Jamhuri jana asubuhi na kushuhudia timu hiyo ikiendelea na mazoezi makali ambapo kwa upande wa Soka ilikuwa chini ya Kocha Msaidizi ambaye ni Mbunge wa Wawi,Ahmed Juma Ngwali.

Kwenye Netiboli timu hiyo ilikuwa ikicheza mchezo wa kirafiki na Chuo cha Mipango huku Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula akionesha ufundi mkubwa wa kufunga mabao.

Aidha wakimbiaji wake, Daniel Mtuka, Yosepha Komba, Zubeda Sakuru nao walikuwa wakifanya maozezi ya kukimbia kujiweka sawa na mashindano hayo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini hapa,Kocha Mkuu wa timu ya Soka,Venance Mwamoto alisema wamejiandaa kufanya vizuri katika mashindano hayo na kuwatoa kimasomaso Watanzania.

Mwamoto ambaye ni Kocha mchezaji na Mbunge wa Kilolo, alisema kwa sasa timu za Taifa zimekuwa zikifanya vibaya katika mashindano mbalimbali hivyo akawataka Watanzania kuamini kwamba timu ya Bunge la Tanzania itawafuta machozi kwa kufanya vizuri.

“Hivi karibuni tumefanya vibaya kwa timu yetu ya Taifa kwa kufungwa na Lesotho pia timu ya Vijana nayo ilipoteza mategemeo yapo kwetu niwaahidi Watanzania hatutawaangusha,”alisema Mwamoto.

Kuhusiana na maandalizi ya mashindano hayo,Mwamoto alisema wameweka kambi ya zaidi ya wiki tatu pamoja na kucheza michezo miwili ya kirafiki ili kuangalia mapungufu ya timu kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Mwamoto ambaye amewahi kuzichezea timu za Majimaji ya Ruvuma,RTC Kagera na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ miaka ya nyuma,alisema kwa sasa timu hiyo ina majeruhi wawili ambao ni Mbunge wa Rufiji Mohammed Mchengerwa na Sixtus Mapunda ambaye ni Mbunge wa Mbinga Mjini .

Kwa upande wake,Kocha wa timu Netiboli, Eleonora Mongi alisema maandalizi yanaendelea vizuri kwa mchezo huo lakini changamoto wanayokutana nayo ni kumkosa Mbunge wa Tarime Mjini,Ester Matiko kutokana na kesi inayomkabili.

Alisema Matiko ni mchezaji muhimu katika kikosi hicho kutokana na kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani.

Kocha huyo alisema wanauhakika wa kutetea ubingwa wa mashindano hayo kutokana na maandalizi ya kueleweka waliyoyafanya.

Mbunge wa Viti Maalum,Agnes Marwa (CCM) aliwatoa wasiwasi Watanzania kwa kuahidi kwamba timu hiyo itarudi na ubingwa wa mashindano hayo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: