Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali akifanya mahojiano maalum na kituo cha Radio cha Jembe Fm cha Jijini Mwanza kuhusu miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
 Mtangazaji wa Kituo cha Redio cha Jembe FM 93.7 mkoani Mwanza, Jimmy Kagaruki akisoma maswali yaliyokuwa yakitumwa na waskilizaji yaliyohusu miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Na Hassan Silayo - MAELEZO.

Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas ameendelea na utaratibu wa kuwapigia simu Wakuu wa Taasisi ili kujibu hoja za wananchi moja kwa moja katika ziara yake kwa vyombo habari inayoendelea nchini.

Katika mahojiano na kituo cha Redio cha Jembe FM 93.7 mkoani Mwanza,

Dkt. Abbasi alimpigia simu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dkt. Irene Isaka , ambaye alifafanua kuhusu Sheria mpya ya Hifadhi ya jamii.

Dkt. Irene alisema kuwa baada ya kuunganisha Mifuko mafao yamezidi kuboreshwa ili mstaafu awe anapokea fao kubwa la mwezi.

Dkt. Isaka amesema kuwa mstaafu atalipwa fao la mkupuo la 25% na baada ya hapo fao la mwezi litakuwa kubwa zaidi tofauti na ilivyokua awali ambapo fao la mkupuo lilikuwa kubwa lakini fao la kila mwezi likawa dogo kumfanya mstaafu ashindwe kumudu maisha.

Aidha, Mkurugenzi wa SSRA ametaja faida zingine za Sheria mpya kuwa ni familia ya mstaafu kuendelea kulipwa kwa miaka mitatu baada ya mstaafu kufariki, fao la kuachishwa kazi, kuweka usawa katika kulipa mafao na kuwa hivi sasa wanaweka utaratibu wafanyakazi wapate mikopo ya nyumba kupitia pensheni zao.

Katika mahojiano hayo ya moja kwa moja na Kituo cha Jembe FM, Dkt. Abbasi pia alimpigia simu Mkurugenzi wa Wakala wa Hufuma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamisi kujibu hoja na masuala ya usafiri wa maji hasa ununuzi w meli mpya Ziwa Victoria ulipofikia.

Bw. Hamisi alielezea vema hatua ambazo Serikali imechukua na inaendelea kuzichukua kuboresha usafiri wa majini.

Ameeleza kuwa mpaka sasa Serikali imeishatekeleza ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo ambao umeanza, ukarabati wa Meli ya MV Victoria ambayo ilikuwa imesimama kutoa huduma Kwa miaka mitano, ukarabati wa MV Ukerewe ambayo ilikuwa haifanyi kazi tangu mwaka 2010 na MV Butiama ambayo baada ya kukamilika itafanya safari za visiwa vya Nansio.

Amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendeleza mageuzi makubwa katika kuufanya usafiri wa majini uendelee kuwa bora na salama.

Katika mahojiano hayo Dkt. Abbasi alisema kuwa Diplomasia ya Tanzania imeendelea kuimarika kwa kutumia mabalozi wetu bila hata Rais kusafiri nje ya nchi mara kwa mara na imeleta matokeo mazuri katika eneo la uwekezaji.

Dkt. Abbasi aliongeza kuwa Diplomasia ya Uwakilishi imefanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa kuvutia wawekezaji ktk nchi za Afrika Mashariki.

“Bila hata Rais kusafiri kwenda China, lakini Tanzania imepata soko kubwa la muhogo kupitia Balozi wetu aliyopo huko na kulifanya zao la muhogo kuwa la biashara,” alisema Dkt. Abbasi

Akiongelea suala la Ulinzi na Usalama, Dkt. Abbasi alisema kuwa Tanzania imeendelea kuheshimika duniani kwa kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa amani duniani na pia kuendelea kuhifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: