Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kuwaapisha Majaji wapya 6 wa Mahakama ya Rufani na Majaji wapya 15 wa Mahakama Kuu, Ikulu Jijini Dar es salaam. Januari 29,2019. Picha na Ikulu.

Na Paschal Dotto-MAELEZO 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amewataka Majaji, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri wapya walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, kufanya kazi kwa kuzingatia masharti ya kazi zao ili kuweza kutoa haki na kuwatumikia wananchi.

“Nawapongeza sana Majaji sita mahakama ya Rufani 15 mahakama kuu , Wakuu wa Wilaya wawili na Wakurugenzi wa halmashauri 10 mulioapishwa leo kikubwa kafanyeni kazi kwa kuzingatia masharti ya kazi zenu, kwa Majaji kasimamieni haki ili wananachi waweze kuondokana na dhuluma, lakini kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kasimamieni mapato nchi inahitaji mapato siyo mkaanze mabishano, uongozi ni kufanya kazi kwa ushirikiano kwa hiyo sidhani kama nitapata malalamiko”, Rais Magufuli 

Rais Rais Magufuli aliwasisitiza Majaji sita wa Mahakama ya Rufani na Majaji 15 wa Mahakama kuu kwenda kuchapa kazi kwani Serikali inahitaji wananchi wapate haki inayotakiwa na itakuwa njia bora kwa wananchi kujua haki zao.

Aidha Rais Magufuli alisema kuwa kuna sehemu hapa Tanzania ambazo imekuwa na dhuluma kubwa akitolea mfano Halmashauri ya Mufindi ambako tukio la ubakaji lilifanyika na mtuhumiwa aliachiwa huru. 

“Unapotazamwa na watu wengi na kupimwa, unapopewa kazi ya kusimamia haki hii ni kazi ngumu sana kwa sababu ina lawama kubwa kwa mfano niliona kwenye Televisheni wamama wakilalamika kwa Waziri Mkuu Mtaafu Mzee Pinda kuwa kuna mtuhumiwa mmoja huko Mufindi Iringa alifanya matukio 11 ya ubakaji lakini akaachiliwa huru, vitu hivi vinawaumiza watanzania kwa bahati nzuri Mhe, Jaji naye aliiona video hiyo mimi nilipoona nilimuagiza mzee pinda amwambie Mkuu wa Mkoa amshike huyu mtuhumiwa”, Alisema Rais Magufuli.

Katika tukio hilo amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro kulifanyia uchukunguzi tukio hilo lifanyiwe kazi kwa upande wa polisi huku akitoa maagizo kwa Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Juma kufuatilia mahakama ya Iringa kuona kama ushahidi unaotolewa unatosha .

Akitoa nasaha kwa wateule hao, Makamu wa Rais Samiah Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa wilaya zote mbili Mwanga na Tarime kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi kama walivyoapa mbele ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nawapongeza Wakuu wapya wa Wilaya hizi mbili lakini nawaomba mkazifanyie kazi changamoto zilizoko katika wilaya zenu, kwa mwanga watu wanapigana ngumi nadhani utaenda kuyarekebisha haya, lakini kwa Wilaya ya Tarime kuna vishawishi vingi sana vya rushwa pamoja ya unyayasaji wa kijinsia, Ubakaji na kupigwa kwa wanawake kwa hiyo kayafanyie kazi haya.”, alisema Makamu wa Rais. 

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi ametoa kongole kwa Rais Magufuli kwa kuteua majaji sita wa Mahakama ya Rufani na 15 wa Mahakama Kuu kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi katika utoaji haki nchini.

Aidha katika kuongeza ufanisi wa kushikiliza mashauri mbalimbali hapa nchini Prof. Kabudi alipenyeza suala la kuwepo kwa mahakama zinazotembea MOBILE COURT ili kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi. 

“Mhe. Rais nashukuru kwa kunipa hao 15 wa Mahakama kuu na sita wa Mahakama ya Rufani kwani sasa idadi ya majaji imeongezeka kutoka majaji 66 mpaka majaji 81 kwa Mahakama kuu baada ya hawa uliowapisha leo”, Jaji Mkuu Prof. Juma 

Akielezea mahitaji ya majaji katika mahakama ya Tanzania Prof. Juma alisema bado Majaji wanahitajika ili kukidhi hali ya sasa ya kuwahudumia wananchi, aliongeza kuwa bado kuna umuhimu wa kuongeza Majaji ikiwezekana wawe na idadi ya majaji 100 mpka 150 kwa sababu kwa sasa wananchi wamezidi kuzijua haki zao.

Jaji Mkuu alisema mahakama inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mahakama za mwanzo 12 ambazo zitazinduliwa hivi karibuni,Miradi 36 ya ujenzi itakayozinduliwa Juni mwaka huu, pamoja na Mahakama 28 za Wilaya nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: