Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsikiliza Mkazi wa mjini Bukoba alipokuwa anaeleza kero yake mara baada ya Waziri huyo kuwaita wananchi hao mbele waweze kutoa kero zao, mara baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Mayunga mjini humo, leo. Lugola licha ya kuwa amewataka waendesha bodaboda wafuate sheria za usalama barabarani, lakini ametoa onyo kwa Polisi mjini humo kuacha kuwakamata waendesha bodaboda wakiwa hawajavaa sare.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsalimia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Bashiru Ally, wakati alipoonana naye Uwanja wa Ndege wa Bukoba, leo. Lugola yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi akitembelea Wilaya zote, akisikiliza kero mbalimbali za watumishi wa Wizara yake pamoja na wananchi mkoani humo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akitoka Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Bukoba mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Kituo hicho, leo, kwa kufuatilia utendaji kazi wao. Katikati ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, na kulia ni Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoani humo, ACP Raymond Mwampashe. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Na Felix Mwagara, MOHA-Bukoba.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Askari Polisi nchini kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za Jeshi.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa uhuru, Mayunga, mjini Bukoba Mkoani Kagera, leo, Lugola alisema polisi wanapaswa kufuata utaratibu wa kijeshi hasa wanapokamata vyombo vya moto na siyo kuvunja utaratibu.

Lugola aliongeza kuwa, bodaboda zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biashara hiyo. “Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha bodaboda,” alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Bukoba na Tanzania kwa ujumla wafuate sharia za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa. Lugola ameanza ziara yake ya siku nane mkoani humo akitembelea Wilaya zote za Mkoa huo akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.

Lugola mwaka jana alitoa maagizo kwa makamanda wa mikoa nchini ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.

Waziri Lugola tayari amemaliza ziara yake kwa Wilaya ya Bukoba na Kesho ataanza ziara Wilaya za Misenyi, baadaye Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Januari 8, 2019 atamalizia ziara yake Wilaya ya Muleba ambapo katika Wilaya hizo pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya Gereza.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: