Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akionyesha kwa Waandishi wa habari baadhi ya simu zilizokamatwa kwa wafungwa katika Gereza La Ruanda jijini Mbeya. Habari na Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amemuelekeza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi askari magereza wanne wanaotuhumiwa kuingiza simu za mikononi kwa wafungwa na kurahisisha mawasiliano kati ya wafungwa na watu walioko nje.

Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari jijini Mbeya Naibu Waziri Masauni amesema kumekuwepo na tabia ya kuingiza vitu visivyoruhusiwa magerezani ikiwemo simu, madawa ya kulevya huku baadhi ya askari wachache wasio waaminifu wakitumika katika mchezo huo.

“Nimefanya ziara katika Gereza la Ruanda, nimezungumza na wafungwa na kugundua kuwepo kwa simu ambazo mkuu wa gereza alizikamata. Maagizo ya Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli wakati akimuapisha Kamishna Jenerali wa Magereza ni kukomeshwa kwa tabia ya kuingiza simu magerezani ambalo Rias alisema limekuwa jambo la kawaida,sasa haiwezekani maagizo ya kiongozi wa juu kabisa yapuuzwe...Sasa namuelekeza Kamishna wa Magereza kuwasimamisha kazi askari hao wanne na aunde tume kuchunguza kwa kina zaidi tukio hilo” alisema Masauni.

Aliwataja askari hao na vyeo vyao kuwa ni Longino Mwemezi (Inspekta), Alexander Mwijano (Stafu Sajenti) Benjamini Malango (Sajenti) na Ramadhani Mhagama huku askari wengine wanne wakiendelea kuchunguzwa kutokana na tuhuma hizo.

Jumla ya simu za mkononi tisa zimekamatwa katika Gereza la Ruanda mkoani Mbeya huku zikishikiliwa kwa uchunguzi zaidi wa kubaini watu waliokuwa wanawasiliana na wafungwa hao na aina ipi ya mawasiliano yaliyokuwa yakifanyika
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: