Rais wa Bunge la Cuba Mheshimiwa Esteban Lazo Harnandez kulia mwenye shati nyeupe akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Ofisi yake kufanya mazungumzo ya Ushirikiano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Bunge la Cuba Mheshimiwa Esteban Lazo Harnandez Mjini Havana Nchini Cuba.
Mheshimiwa Esteban Lazo Harnandez kulia akipokea zawadi ya Mlango wa Zanzibar kutoka kwa Balozi Seif kama ishara ya kufunguliwa milango ya kutembelea Zanzibar.
Mheshimiwa Esteban Lazo Harnandez akimtembeza Balozi Seif sehemu mbali mbali za Jengo la Bunge ya Cuba lenye Historia ya muda mrefu ambazo zimewekwa kama kumbu kumbu ya Taifa hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Pili kutoka kulia na Ujumbe wake akifanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Afya Mjini Havana Nchini Cuba.Kushoto ya Balozi Seif ni Mkurugenzi Mkuu wa Utafiti Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Mayasa, Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdullah na Mkurugenzi Tiba Wizara ya Afya Dr. Juma Salum Mbwana {Mambi}.Wa Kwanza kutoka Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya wa Cuba Bibi Marcia Cobas.
Naibu Waziri wa Afya wa Cuba Bibi Marcia Cobas akibadilishana mawazo na Balozi Seif mara baada ya kumaliza mazungumzo yao mwisho mwa ziara ya Ujumbe wa Zanzibar Nchini Cuba.Picha na – OMPR – ZNZ.

Cuba itaendelea kudumisha ushirikiano wake wa Kidiplomasia na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika mafungamano ya kustawisha Wananchi wake licha ya Taifa hilo la Caribean kipindi hichi kupita katika mabadiliko ya Kisiasa, Uchumi na Utamaduni.

Rais wa Bunge la Cuba Mheshimiwa Esteban Lazo Harnandez alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyefika kusalimiana nae pamoja na kumpongeza baada ya kuchaguliwa tena kuliongoza Bunge hilo hapo katika Ofisi ya Bunge hilo Mjini Havana Nchini Cuba.

Mhe.Esteban Lazo Harnandez alisema kutokana na mabadiliko ya mfumo wa Dunia uliopo hivi sasa katika masuala ya Uchumi, Siasa na Utamaduni Jamuhuri ya Cuba imelazimika kufanya mabadiliko ya Katiba yake ili yalingane na mfumo huo wa Dunia inayozunguuka katika mazingira ya Kijiji.

Alisema Bunge ya Cuba tayari limeshafanya marekebisho katika Katiba yake kutoa nafasi kwa Wananchi wake kuwa na Uwezo na Uhuru wa Kumiliki Nyumba Ardhi pamoja na uwepo wa Waziri Mkuu atakayekuwa na Mamlaka ya kusimamia utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Esteban alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wakati Vikao vya Bunge hilo vinatarajiwa kuanza Wiki ijayo baada ya kukamilika kwa Uchaguzi wa Wabunge wake, Serikali ya Nchi hiyo imeanza kupiga hatua kubwa zaidi ya Maendeleo kutokana na Mabadiliko hayo.

Rais huyo wa Bunge la Cuba alisisitiza kwamba Taasisi za Kifedha zitalazimika kuzingatia ukusanyaji bora zaidi wa Mapato katika maeneo yote ya Uchumi ili ushiriki wa Wananchi waliowengi katika katika mfumo huo wa kifedha upatikane vyema.

Mheshimiwa Esteban alimuhakikishia Balozi Seif kwamba ule uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili utaendelea kuimarishwa na kukuzwa katika muda wote.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zitaendelea kufuatilia Mabadiliko ya Cuba na kuangalia hatua inayoweza kuiga mabadiliko hayo katika azma ya kuimarisha Uchumi na Ustawi wa Wananchi walio wengi.

Balozi Seif katika mazungumzo hayo alimpongeza Rais wa Bunge hilo la Cuba Mheshimiwa Esteban Lazo Harnandez kwa kuchaguliwa tena kushika wadhifa huo ikionyeshawazi ishara halisi ya kukubalika vyema na Wananchi wa Nchi hiyo kupitia Viongozi wake.

Balozi Seif na Ujumbe wake alimalizia ziara yake Nchini Cuba kwa kufanya mazungumzo na Uongozi wa Waziri wa Afya wa Nchi Hiyo ukiongozwa na Naibu Waziri wake Bibi Marcia Cobas hapo Makao Makuu ya Wizara ya Afya Mjini Havana Nchini Cuba.

Katika mazungumzo yao ya ushirikiano wa Kidugu Balozi Seif alisema matunda ya Darasa la Madaktari Wazalendo waliosimamiwa na Wataalamu pamoja na Wahadhiri wa Nchi ya Cuba yameanza kutoa Matumaini.

Balozi Seif alisema Kitendo cha Serikali ya Cuba kukubali kupunguza gharama kubwa ya kuwaendeleza Madaktari hao Wazalendo wapatao 15 katika Shahada ya juu ya Udaktari wa Uzamili Nchini humo kinaendelea kuleta faraja kubwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Watu wake.

Alisema wakati Zanzibar ikiendelea kutekeleza Sera ya Afya ya kuwa na miuondombinu ya huduma za Afya katika umbali usiozidi Kilomita Tano kundi hilo na Madaktari linaloendelea kuongezeka kila Mwaka litakuwa Mkombozi wa utekelezaji wa Sera hiyo muhimu.

Naye Kaibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bibi Asha Ali Abdullah aliueleza Uongozi huo wa Wizara ya Afya Cuba kwamba Zanzibar hivi sasa inapita katika kipindi cha kujiimarisha kwenye mapambano yake dhidi ya Maradhi yasiyoambukiza.

Bibi Asha alisema maradhi yasiyoambakiza kama Kisukari pamoja na shindikizo la Damu hivi sasa yamekuwa yakiathiri Wananchi walio wengi na kuleta vifo vingi jambo ambalo jitihada zinachukuliwa katika kuona kasi hiyo ya athari inapungua au kuondoka kabisa.

Alisema kwa upande wa maradhi ya Malaria hivi sasa yamepungua kutokana na Kampeni kubwa iliyochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi na Mataifa wahisani katika kuangamiza vilui lui vya maradhi hayo.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya Zanzibar alimuhakikishia Naibu Waziri wa Afya wa Cuba kwamba ushauri wote walioupata katika ziara yao kwenye Taasisi za Afya Nchini Cuba likiwemo suala la Upatikanaji wa Dawa litazingatiwa na iwapo linaweza kuleta fueni ya gharama kwa Zanzibar watalichukulia hatua mara moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: