Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Mheshimiwa Zainab Telack akizungumza wakati wa kutambulisha mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria unaotekelezwa na asasi ya T- MARC kwa ajili ya kuhamasisha jamii kupambana na ugonjwa wa malaria katika halmashauri za wilaya za Ushetu,Msalala na Kishapu mkoani Shinyanga - Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack, akiwasihi viongozi na wataalamu kushirikiana na asasi ya T- Marc kutekeleza mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria.Wa kwanza kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga,Mohammed Kahundi akifuatiwa na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima. Wa kwanza kushoto ni Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akifuatiwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha.
Kushoto ni Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- Marc, Hamid Al- Alawy akifuatiwa na Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka T- MARC, Levina Thobias na Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima (kulia).
Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima akielezea kuhusu Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015-2020) wa kudhibiti Malaria ulioandaliwa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Wadau wakiwa ukumbini.
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- Marc, Hamid Al- Alawy akielezea kuhusu mradi huo na shughuli mbalimbali zinazofanywa na T-MARC katika kuwahudumia wananchi.
Wadau wa kupambana na ugonjwa wa malaria wakiandika dondoo muhimu.
Wadau wa kuzuia ugonjwa wa malaria wakiwa ukumbini.
Wadau wakiwa ukumbini.
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka T- MARC, Levina Thobias akiwasilisha mada kuhusu tafiti mbalimbali zilizofanywa na T-Marc ambapo walibaini kuwa bado jamii ina imani potofu kuwa utumiaji wa vyandarua unapunguza nguvu za kiume lakini pia kuleta kunguni.
Mkuu wa wilaya ya Kahama,Anamringi Macha akiwataka wadau wanaotekeleza miradi mbalimbali wilayani Kahama kuhakikisha wanatumia lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza akibainisha kuwa baadhi ya wadau wamekuwa wakisambaza vipeperushi vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza wakati wananchi wanaelewa vizuri zaidi Kiswahili. 
Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy akiagana na Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Zainab Telack.
Picha ya pamoja.

Mradi huo umetambulishwa leo Jumanne Machi 5,2019 katika ukumbi wa Submarine Hoteli Mjini Kahama wakati wa mkutano wa utambulisho wa mradi huo uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa kutokomeza Malaria.

Lengo la mradi huo utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili ni uhamasishaji wa kuzuia ugonjwa wa malaria ambapo walengwa ni akina mama wajawazito,wanaonyonyesha,walezi wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na watoa huduma kwenye kliniki za akina mama na watoto.

Akitambulisha mradi huo,Telack alisema ripoti ya Viashiria vya maambukizi ya Malaria ngazi ya jamii ya mwaka 2017/2018 inaonesha kuwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria yamefikia asilimia 6 kutoka asilimia 17 kwa mwaka 2015/2016.

“Pamoja na kupungua kwa maambukizi kulikochangiwa na juhudi za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa mikakati ya udhibiti wa malaria iliyopo inatakelezwa kwa ufanisi,hivyo bado juhudi zinatakiwa kufanyika ili kupunguza kiwango hiki kufikia asilimia 1 na hatimaye kutokomeza kabisa Malaria katika mkoa wetu”,alieleza.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kupitia Mpango Mkakati wa miaka mitano (2015-2020) wa Kudhibiti Malaria ulioandaliwa na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, kumekuwepo mafanikio mkoani Shinyanga ikiwemo kuongezeka kwa uwepo wa vyandarua vyenye dawa kwa jamii.

Aidha alisema kutokana na kuwepo kwa mwitikio mdogo wa wanajamii kushiriki katika mikakati ya kupambana na malaria ni imani yake kwamba kupitia mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria utatumika kuhamasisha jamii kushiriki kwenye mikakati ya kudhibiti malaria kwa vitendo.

Telack aliwataka viongozi na wataalamu wa ngazi ya mkoa,wilaya na halmashauri kushirikiana na T- MARC kutekeleza mradi huo vizuri ili kutokomeza Malaria huku akiitaka T-MARC kujipanga kutekeleza mradi huo kwenye mkoa mzima.

“Malaria inazuilika na inatibika,tiba ya mapema baada tu ya dalili za homa kuanza ni muhimu kuzuia vifo hususani kwa watoto na akina mama wajawazito”,aliongeza Telack.

Awali Meneja Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria kutoka asasi ya T- MARC, Hamid Al- Alawy alisema kupitia mradi watahamasisha wanawake wajawazito,wanaonyonyesha na watoto kutumia vyandarua vyenye dawa kuzuia ugonjwa wa malaria lakini pia jamii kupima afya badala ya kuanza kutumia dawa kwani siyo kila homa ni malaria.

Naye Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Teresia Shirima aliwataka wananchi kuondokana na dhana potofu kuwa vyandarua vinapunguza nguvu za kiume huku akiwahamasisha kutumia vyandarua kwa matumizi yaliyokusudiwa.

Mradi wa Badilisha Tabia Tokomeza Malaria' unatekelezwa na asasi ya T- MARC Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI na Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ili kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Malaria.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: