“ This Isn’t Only Simba, It’s Astonishing Simba..!”
- Hii Sio Tu Simba, Ni Simba Ya Kushangaza..!

Ndugu zangu,

Matokeo yale yaliyoushangaza ulimwengu wa soka usiku wa juzi yalinifanya nirudi kwenye maktaba yangu kuona kama ilipata kutokea. Kuiangalia historia. Maana, nimekumbushia mara nyingi, kuwa historia ni Mwalimu Mzuri.

Ni hivi, Simba wale tuliowaona juzi walipata kutokea mwaka 1993. Tuliokuwepo tutakumbuka, Simba ya mwaka ule iliushangaza ulimwengu wa soka.

Mwaka ule Afrika kulikuwa na makombe matatu ya kugombania kwa ngazi ya vilabu; Kombe la Klabu Bingwa, Kombe la CAF na Kombe la Washindi.

Simba ilishiriki Kombe la CAF. Itakumbukwa, muasisi wa kombe lile alikuwa tajiri wa Nigeria, Mashoud Abiola. Huyu alikuwa swahiba wa Jenerali Ibrahim Babangida aliyetawala Nigeria enzi hizo.
Kuna wakati hata kombe lenyewe lilijulikana kama ‘ Kombe la Abiola’.

Simba ilianza mashindano yale kigoigoi. Lakini, cha kushangaza ikawa bora zaidi kwa kila mechi iliyofuata. Kama mwaka huu, kila timu iliyokanyaga Neshno kwa Mkapa ilipigwa. Na ikawa Simba iliyoshinda nyumbani na kukomaa ugenini. Simba ile ya kushangaza ilifika fainali ya Kombe la CAF.

Walivyoanza Simba wa 1993:

Walicheza na Flaviao ya Maputo nyumbani kwenye uwanja wa Kirumba, Mwanza. Wakatokw sare ya 0-0. Simba iliona mapema mapungufu yake. Kubwa kabisa wakandua kuwa Kirumba Stadium haukuwa uwanja wa nyumbani kwa Simba. Ilivyo Simba wako nyumbani wakiwa Neshno Kwa Mkapa. Faida za uwanja wa nyumbani kwa timu ni ile hali ya kuutawala uwanja ndani na nje. Simba hawajapata kuutawala uwanja wa Kirumba, Mwanza. Mechi ya marudiano Maputo Simba walishinda 1-0.

Mechi ya pili wakakutana na Mbabane Highlanders. Ugenini Simba wakashinda 1-0 na nyumbani hivyo hivyo.

Wakaja Al Haraach. Nyumbani Simba wakashinda 3-0 na ugenini wakafungwa 2-0.

Simba mechi iliyofuata wakawaribisha Club Aviacao ya Angola pale Neshno Kwa Mkapa. Aviacao walitisha, simulizi moja ya mjini wakati huo ni ukweli kuwa Aviacao kwenye mechi yao dhidi ya Gor Mahia, walitua Nairobi saa tano asubuhi kwenye siku ya mechi, jioni wakamfunga Gor Mahia.

Club Aviacao ya Angola hawakuamini macho yao walipolala 3-1 pale Neshno Edward Chumila alipachika mawili na Malota Soma ‘ Ball Jagler’ akatupia moja.

Ikaja mechi ya fainali dhidi Stella Abidjan. Simba walipambana ugenini wakatoa sare ya 0-0.

Nyumbani ilihitaji goli moja tu. Mfadhili wa Simba enzi hizo, Azim Dewji, akaahidi kila mchezaji kupewa gari aina ya Canter, mpya, Simba ikibeba kombe.

LAKINI, kuna mchezaji wa Stella Abidjan kila mpenzi wa Simba aliyekuwepo wakati huo hatamsahau, na atawasimulia wanawe. Aliitwa Boli Zozo.

Alipachika magoli mawili pale Neshno Kwa Mkapa na yaliyozima ndoto za Simba.

Mwaka huu 2019 nawaona Simba wa 1993. Wanaweza kuushangaza ulimwengu wa soka na kufuka nusu fainali na hata fainali.

This Is Astonishing Simba!

Maggid Mjengwa.

Whatsapp: 0688 37 36 52
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: