HAKYANANI mama wa staa maarufu Bongo, Wema Sepetu, Mariam Sepetu haishiwi vioja; hivi karibuni kafanya kingine kwa kumshushia kipingo shosti mkubwa wa mwanaye Diana Kimari; halafu akafunguka kuhusu tukio hilo. Risasi Mchanganyiko liliponasa fununu kuwa Diana kachezea makonde kutoka kwa mama huyo liliwasiliana naye Jumatano iliyopita kwa hisia kwamba huwenda atakanusha; lakini cha ajabu alisema: “Siyo kumpiga, nimempiga hasa na bado ipo siku nitamvunja mguu.”

Kwani kisa hasa ni nini cha kumkamia namna hiyo mtoto wa watu? Mwandishi wetu alipotaka kujua hilo kutoka kwa mama Wema alijibiwa kuwa: “Nimeshamwambia sitaki ushoga na mwanangu.” Inaelezwa kwamba hata baada ya kuonywa na mama huyo kuwa mbali na mwanaye, Diana hajawahi kusalimu amri na kwamba hivi karibuni alikiuka marufuku hiyo na kuongozana na Wema mkoani Arusha kwa shughuli binafsi.

Wakiwa huko mama Wema ambaye amejipa jukumu gumu la kumchunga mwanaye ambaye anaonekana mkubwa kuliko Diana aliendelea kufuatilia nyendo zake kujua watu alioongozana nao. Ubuyu ukaja kwamba aliongozana na kijana mmoja aitwaye Kenneth Sepetu ambaye mama huyo anashangaa hata hilo jina la Sepetu ‘msela’ huyo kalipata wapi wakati si miongoni mwa ndugu zake.

Mwingine aliyetajwa kuvamia msafara wa Wema Arusha ni Diana; mbaya wa mzazi huyo wa msanii maarufu ambaye kwa sasa anajitahidi kutulia baada ya kukwaa skendo nyingi zikiwemo za kupiga picha chafu. Habari zinasema siku waliporejea kutoka Arusha, Wema, Diana na Kenneth waliongozana hadi nyumbani kwa akina Wema ambako walikutana na mkasa wa kipigo.

“Wakati anaondoka nilimwambia aambatane na Petitman (kijana anaewasimamia baadhi ya wasanii hapa nchini) na mpiga picha wake Bestizo. “Nilipokuwa nawapokea nikashangaa kuwaona, nikasema sijui niende nikavae suruali kwanza ndipo nije niwafumue, basi nilijikuta nampiga teke Diana,” alisema mama Wema.

Aliongeza kuwa wakati akiendelea kutoa kichapo hicho Wema hakusema chochote kwa kuwa anafahamu kuwa amekanywa mara kadhaa kuwa na urafiki na Diana. Msingi wa katazo unaojengwa na mama Wema ni kwamba Diana ana tabia mbaya ambazo zinamharibu mwanaye.

Tabia hizo ni zipi? Maana kama ni pombe hata mwanaye anakunywa, kuvuta majani amewahi kutajwa, kujirusha ndiyo kwake sasa hizo mbaya anazotaja mama huyo mbali na hizo ni zipi au ndiyo hizohizo? Huu unabaki kuwa ni mchanyato wa kihabari katika kudadisi mambo. “Mimi naomba kumwambia Diana siku ile nimempiga haikutosha, kuna siku nitamuumiza ndugu zake watamkuta Muhimbili, maana Wema hawezi kuongozana kila mahali na watu wasiojielewa,” alisema mama huyo kwa ukali.

Diana anayetajwa kuwa na tabia mbaya ni yule binti aliyeigiza na Vincent Kigosi ‘Ray’ katika Filamu ya Family Disaster ambayo iliwavutia watazamaji wengi. Gazeti hili lilipomtafuta Diana kwa njia ya simu hakuweza kupatikana lakini Bestizo liyekuwepo siku ya tukio alikiri kutokea kwa ugomvi kati ya mama Wema na Diana.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: