Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.

Jamii yatakiwa kutomaliza masuala ya ukatili wa kijinsia ndani ya familia na badala yake ishirikiane na Serikali ili sheria ichukue mkondo wake.

Hayo yameelezwa leo, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Zainab Mussa Bakar kuhusu lini Serikali italeta muswada wa sheria bungeni ili kurekebisha sheria hiyo iwe kali zaidi.

"Kwa ujumla sheria zilizopo zinajitosheleza kabisa kuwashughulikia wale wote wanaokutwa na hatia katika makosa ya ubakaji, kunajisi watoto wa kiume na wa kike. Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 1985 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, imeelekeza adhabu kali kwa yeyote atakayebainika kutenda kosa la kumdhalilisha mtoto au kumbaka ikiwemo kifungo cha miaka 30," amesema Dkt. Ndugulile.

Ameendelea kusema kuwa, imekuwa vigumu kuwatia hatiani wakosaji hasa wa ndani ya familia kwa kukosekana kwa ushahidi ikizingatiwa matukio mengi hufanywa na watu walio karibu na familia ambapo wengi wao wanaogopa kutoa ushahidi kutokana na hofu ya kupoteza mmoja ya wanafamilia kutokana na adhabu ya kifungo cha maisha.

Aidha, kutokana na mtazamo hasi wa jamii, familia nyingi uhofia kudhalilika au kunyanyapaliwa baada ya kubainika mkosaji.

Hata hivyo, Serikali inajitahidi kuweka mikakati ya kusaidia kupunguza au kumaliza kabisa tatizo hilo, lakini familia nyingi zimekuwa hazitoi ushirikiano ili kuwatia hatiani wale wanaopatikana na makosa ya ukatili wa kijinsia ndani ya familia.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: