Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akisoma jina la nchi inayozalisha vitasa vilivyotumika kwenye milango ya jengo la utawala 
Mmoja wa Wajasiriamali anayefanya shughuli zake katika eneo la stendi kuu mpya Njombe akionesha kitambulisho cha Wajasiriamali kilichotolewa na Mhe. Rais kwa Wajasiriamali wadogo 
Mkuu wa Mkoa Njombe akionesha utaalamu wake kwenye kusonga ugali wakati alipotembelea mabanda ya muda ya mama lishe katika eneo la stendi kuu mpya 
Mkuu wa Mkoa Njombe akiangalia zege iliyomiminwa katika meza za kuuzia mbogamboga kwenye eneo la ujenzi wa soko kuula kisasa Njombe 
Ujenzi wa Soko la Kisasa ukiendelea katika Mtaa wa Gwivaha Halmashauri ya Mji Njombe ujenzi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Tsh. Bilioni tisa mpaka kukamilika kwake. 
Mkuu wa Mkoa wa Njombe akikagua kitabu cha kukata risiti kwa abiria kwenye mojawapo ya basi ikiwa ni sehemu ya ziara yake alipotembelea stendi kuu mpya ya mabasi. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi . Ruth Msafiri 
Mkuu wa Mkoa wa Njombe akikata nyama za kuchoma 


Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akiongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Thadei Luoga (kushoto), Wahandisi (kulia),Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama na Wataalamu mbalimbali wakati wa ziara yake katika stendi kuu mpya 
Mhandisi Mkazi wa ujenzi wa stendi Didasi Joseph akionesha shughuli za ujenzi zinazoendelea katika eneo la maegesho ya mabasi madogo kwenye stendi kuu mpya Njombe 
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka akiwa ameshikilia kipande cha marumaru ili kujirithisha ubora wa marumaru hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri.

Hyasinta Kissiama-Afisa Habari H/Mji Njombe 

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amefanya ziara na kukagua shughuli za umaliziaji wa ujenzi stendi kuu mpya iliyoanza kazi rasmi 11 Mei 2019 na kukagua shughuli za ujenzi wa mradi wa soko kuu la kisasa na kuridhishwa na kasi na viwango vya ujenzi wa soko hilo. 

Ziara hiyo iliyolenga kutambua na kupatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi mara baada ya kuanza rasmi kwa stendi kuu mpya, na kuangalia thamani ya pesa iliyotumika katika hatua zinazoendelea za ujenzi wa soko kuu Njombe, ilijumuisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe. 

Akizungumza na Wasafiri, Wajasiriamali wadogo, Mama Ntilie na Wadau mbalimbali wa usafirishaji na Wananchi kwa ujumla waliokuwepo katika eneo hilo la stendi, ambao wengi walipongeza jitihada za Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo na kuonekana kufurahishwa kuhamia katika stendi hiyo mpya, Sendeka amewataka Wananchi hao kuendelea kuiunga mkono na kuipongeza Serikali ya Dkt John Pombe Joseph Magufuli ambayo imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa na yenye tija kwa wananchi wa hali ya chini na wanyonge. 

Mmoja wa Wajasiriamali wa bidhaa za vinywaji Mjini hapo John Msemwa alisema kuwa kero yake kubwa ni kuzuiwa kwa wao kuingia katika stendi hiyo kufanya biashara licha ya kuwa na kitambulisho cha Mhe. Rais jambo ambalo halikuwepo katika stendi ya zamani na linawakosesha wao kupata riziki. 

Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo Sendeka amewataka Wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambapo stendi ipo katika hatua za mwisho za umaliziaji na kwamba utaratibu rasmi utaandaliwa kwa ajili ya matumizi ya stendi hiyo. 

“Tupo katika hatua za mwisho za umaliziaji wa stendi. Ninachotaka niwahakikishieni ni kwamba Vitambulisho vya Mhe. Rais vitaheshimiwa kama ambavyo mwenyewe ameelekeza.Tutakaa na Halmashauri, Mkuu wa Wilaya na baadaye tutakaa na ninyi ili kuweka utaratibu ambao utakuwa, rafiki, shirikishi na wa uwazi kwa Wafanyabiashara, Wajasiriamali, Wadau wa usafirishaji na watumiaji wote wa stendi. Tukumbuke pia hatuwezi kuingiza Mji Mzima stendi kufanya shughuli zao. Alisema Sendeka. 

Akitoa ufafanuzi kuhusu taratibu za upatikanaji wa vibanda kwa ajili ya shughuli za biashara katika stendi kuu mpya, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Thadei Luoga amemuhakikishai Mkuu wa Mkoa na kumtoa hofu kuwa Halmashauri ilifuata na inaendelea kufuata taratibu zote za manunuzi katika ukodishaji wa rasilimali za stendi mpya na mchakato wa manunuzi unaendelea kulingana na sheria kanuni na taratibu na kumthibitishia kupeleka nyaraka zote za masuala ya manunuzi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kama alivyoagiza kwa ajili ya kwenda kuzipitia na kujiridhisha na vyombo vya usalama kama taratibu zote za manunuzi zimefuatwa ipasavyo. 

Katika hatu nyingine Ole Sendeka ameipongeza Halmashauri na Mkandarasi Nandra Construction kwa kazi nzuri yenye kasi na ubora ya ujenzi wa soko la kisasa Njombe na amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha kuwa anamaliza kazi hiyo kufikia Octoba 2019 kwa mujibu wa muda wa nyongeza waliiomba na amesema kuwa kwa kasi na shughuli zilizosalia ana imani kubwa muda uliobaki unatosha kumaliza shughuli zilizobaki na soko kuanza kazi mara moja. 

Halmashauri ya Mji Njombe inatekeleza mradi wa Ujenzi wa stendi ya kisasa ambayo imeanza kutumika na mradi wa ujenzi wa soko la kisasa kupitia programu ya uboreshaji na uimarisha Miji ULGSP ambapo kila mradi unatarajiwa kugharimu zaidi ya Bilioni 9 mpaka kukamilika kwake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: