Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ijumaa tarehe 7 Juni 2019 aliendelea kudhihirisha kwa vitendo dhana nzima ya maslahi ya taifa kwa nchi yetu.

Kwa wale waliosoma na wanaosoma somo hili la maslahi ya taifa pale Chuo cha Diplomasia Kurasini au Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) pale Kunduchi hakika watakuwa wamepata ile 'practical side' ya kile walichokisoma.

Ni imani yangu kuwa hata watanzania wengine pia wamenufaika mno na somo lile.

Mjengee picha yule mfanyabiashara ambaye alifanyiwa hila na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa TRA ambaye sasa anatakiwa alipwe fidia ya hasara aliyopata!

Baada ya kumjengea picha huyo, mjengee picha Kilua na mpango wake uliokwama pale Kibaha.

Ni nani kati yetu alikuwa anafikiria kuhusu masharti yaliyowekwa na wachina kwenye ujenzi wa bandari ya Bagamoyo?

Nadhani Rais Magufuli ni mwanafunzi mzuri wa Niccolo Machiavelli.

Niccolo Machiavelli ambaye aliandika vitabu maarufu vya masuala ya maslahi ya taifa kama "The Prince" cha mwaka 1513 ambacho kilikuja kutafsiriwa kwa kingereza mwaka 1532 na "The Discourses" cha mwaka 1517 ambacho kilikuja kutafsiriwa mwaka 1531 kama 'The Discourses on Livy' ni miongoni mwa watu waliokuwa wakihusudiwa sana na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kudhihirisha hilo, katika moja ya mahojiano yake Baba wa Taifa alipata kusikika akisema: "You want me to tell you what's a book I am reading now?... I'm reading Machiavelli!"

Akimaanisha, 'Unataka nimwambie ni kitabu gani nasoma sasa? Namsoma Machiavelli!'

KWA NINI NINASEMA RAIS MAGUFULI NI MWALIMU MZURI WA SOMO LA MASLAHI YA TAIFA?

Ili kufahamu sababu ni vema kwanza tukafahamu maana ya neno maslahi ya taifa japo kwa uchache.

Niccolo Machiavelli (1513) alitumia neno "Raison d' etat" au kwa Kingereza 'Reason of the State' kuelezea kwa kina namna nchi inavyoweza kufanya lolote liwezekanalo ili kupigania na kulinda maslahi ya taifa kwa kuwa rasilimali za taifa ndiyo sababu ya uhai wa dola.

Rasilimali za taifa zipo nyingi mno, kuna zile zinazoonekana na zisizoonekana kwa mfano bahari, mito, maziwa, milima, mabonde, mbuga, wanyama, ndege, samaki,misitu, mapori, madini, bandari na hata watu wenyewe.

Mimi hapa nitaongezea moja, nalo ni kodi. Kodi linabeba muktadha mpana wa maslahi ya taifa kwa wakati huu.

Hata waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki Profesa Paramagamba Kabudi alisema akiwanukuu waisrael na wamarekani kuwa wao (Marekani na Israel) wanaamini katika mambo mawili, *kuzifia nchi zao na kulipa kodi!*

Tukumbuke pia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusisitiza kwa kusema:

"Taifa lisilolipa kodi ni taifa mfu!"

Kwa nini Baba wa Taifa alisema vile?

Ritchie (2008:7) katika kitabu chake "US Nuclear Weapons Policy After the Cold War" alieleza:

"States constantly struggle for power because with power comes influence and a greater capacity to ensure national security and state survival in an uncertain and anarchic international environment."

Kwa tafsiri yangu:

'Madola hupambana kwa ajili ya nguvu kwa sababu kwa kuwa na nguvu hupelekea kuwa na ushawishi na uwezo mkubwa wa kuhakikisha usalama wa taifa na uhai wa dola katika mazingira ya kimataifa yasiyotabirika na yasiyo na serikali ya dunia.'

Kwa msingi huo kodi ndiyo uhai wa dola na ndiyo hupelekea dola kuwa na nguvu za kiuchumi na ushawishi.

Kutolipa kodi huweza kusababisha taifa kuanguka kama ilivyoanguka Ugiriki.

Rais Magufuli kwa kutambua hili la umuhimu wa kodi kwa uhai wa Dola alikutana na wafanya biashara kutoka wilaya zote 185 za Tanzania na kuwasisitiza kulipa kodi ili dola au nchi iweze kuishi (survive).

Kwa kusisitizia hili Burchill (2005:47) alieleza:

"Primary national interest of nation-states is the pursuit of national security usually defined as physical survival and territorial integrity."

Je Rais Magufuli si mwalimu mzuri wa maslahi ya Taifa?

Lingine linalothibitisha kuwa Rais Magufuli ni mwalimu mzuri wa Maslahi ya Taifa lilionekana kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikuwa mgeni katika Mashindano ya 20 ya usomaji Qur'an Tukufu yaliyofanyika pale uwanja Mkuu wa Taifa (KwaMkapa) Jumapili tarehe 19 May, 2019.

Wapo walioshangaa hatua ya Rais Magufuli kuhudhuria mashindano yale, ni muhimu wafahamu kuwa alichofanya Mheshimiwa Rais kinabeba dhana nzima ya maslahi ya taifa.

Katika kuthibitisha hili Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilijipambanua wazi katika utangulizi, misingi ya Katiba kwamba:

KWA KUWA SISI Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na
amani:

Hivyo kitendo cha Rais kuhudhuria mashindano ya usomaji Quran ni sehemu ya kuimarisha Uhuru, haki, udugu baina ya waislamu na wakristo na kuimarisha amani inayotokana na kuimarika kwa udugu baina ya watanzania.

Kuonesha kuwa suala hili lilibeba sura ya umoja wa kitaifa wasaidizi wengi wa Mheshimiwa Rais nao waliamua kufanya matukio mbalimbali yakiwemo matukio kama hili la kuhudhuria usomaji wa Qur'an na wengine kufuturisha.

Kwa bahati mbaya moja wapo ya matukio ya kufuturisha lilileta taswira tofauti baada ya kiongozi kushika T-shirt iliyokuwa na maelezo ya imani yake huku tukio likiwa linalenga kufanya ibada kwa watu wa imani ya kiislamu.

Jambo hili lilizua mjadala kwa watu wa imani ya kiislamu kwa kuzingatia udugu baina ya watanzania.

Ni muhimu sana mambo kama haya yazingatiwe na yaepukwe ili wasaidizi wa Rais wasimuangushe Mheshimiwa Rais katika kuimarisha Uhuru, haki, udugu na amani ambayo ni maslahi msingi ya taifa kama ilivyoainishwa kwenye Katiba.

Kwa mujibu wa Hans Morgenthau (1951) katika kitabu chake "In Defense of the National Interest" alieleza kuwa, Uhuru, amani, usalama na umoja ni maslahi makuu ya taifa ambayo dola/nchi haiwezi kufanya maridhiano (compromise) ya mbadilishano na dola lingine lolote au taasisi yoyote ile ili kuviachia ama kuhatarisha.

Haya yameelezwa pia katika Sera ya Tanzania ya Mambo ya Nje kwenye msingi na malengo kuanzia ile ya mwaka 1964 iliyotolewa kwa Waraka wa Rais namba 2 na hii mpya iliyotolewa mwaka 2001 zilipoeleza:

Safeguarding the sovereignty, territorial integrity and
political independence of the United Republic of Tanzania;

Defence of freedom, justice, human rights, equality
and democracy

Nina hakika kabisa pia kuwa Rais Magufuli alimsoma Samuel Huntington katika The Clash of Civilization Remaking of World Order cha mwaka 1996 alipoeleza kuwa chanzo kikubwa cha migogoro katika kipindi hiki cha baada ya Vita Baridi (Post Cold War era) ni Utambulisho wa Tamaduni na Dini (Cultural and Religious Identity) ndiyo maana aliona umuhimu mkubwa wa kuhudhuria mashindano yale ili kuimarisha udugu, upendo baina ya waisalamu na wakristo, amani, Uhuru wetu kama watanzania na haki kama ilivyoelezwa kwenye Katiba yetu.

Je Rais Magufuli si mwalimu mzuri wa somo la maslahi ya taifa?

Raia Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametuthibitishia pia kuwa yeye ni Strategic Negotiator kwa kutazama jinsi serikali yake ilivyoukataa mradi wa ujenzi wa Bandari wa Bagamoyo, mkataba wa Ujenzi wa Reli ya SGR uliokuwa ujengwe na wachina na namna alivyoshawishi bomba la mafuta liweze kujengwa kutoka Hoima, Uganda mpaka Chongoleani, Tanga.

Huu alikuwa mkakati thabiti wa kuifanya Bandari ya Tanga iweze kuketa mapato makubwa hasa kufuatia upanuzi unaoendelea.

Je Rais si strategic negotiator?

Hii sifa ya negotiator ni sifa mojawapo ya balozi, hivyo kuwa kwake mwanadiplomasia namba moja anatudhihirishia umahiri katika hili.

Kuthibitisha haya, Feltan aliainisha sifa 9 za balozi akizigawa katika mafungu mawili ya sifa za kiutendaji (functional skills) na sifa maalumu (special skills):

Kwa muktadha wa maslahi ya taifa nitaeleza sifa moja ambayo ni "cross-cultural skills" yaani ule uweledi wa kufahamu tamaduni mbalimbali.

Mfano mzuri katika hili ni pale Rais alipohudhuria kongamano la usomaji wa Qur'an pale uwanja wa Mzee Mkapa akiwa amevalia Kanzu nzuri sana ambayo binafsi ilinivutia mno na ile baraghashia yake ilivyokaa vema kichwani.

Kwa bahati mbaya sana sina hakika kama wengi wa watendaji waliopewa jukumu la kikatiba la kumsaidia Mheshimiwa Rais (tukiacha Makamu wa Rais na Waziri Mkuu) sijui kama wanamuelewa mheshimiwa Rais, sijui kwa kweli!

Jenga picha ya wale wafanya kazi wa TRA waliozuia mzigo tangu mwaka 2015 ili wapewe rushwa, jenga picha namna wafanyabiashara wanavyolalamika kuhusu kodi na tozo mbalimbali.

Unadhani wanamuelewa Rais anachotaka?

Ukimaliza kujiuliza hilo, jenga picha kile alichokisema Mkurugenzi Mkuu wa TIC bwana Godfrey Mwambe kuhusu "kukanyagana" kwa ofisi,taasisi na watendaji wa serikali kunavyokwamisha juhudi za dhati ya Mheshimiwa Rais za kuiletea maendeleo yatokanayo na viwanda nchi ya Tanzania.

Vipi kuhusu kutotambua misingi ya Katiba ya Uhuru, haki, udugu na umoja wa kitaifa?

Je wanamuelewa kweli!?

Rais Dkt, John Pombe Joseph Magufuli ni Mwalimu mzuri sana wa somo la maslahi ya Taifa, tusimuangushe!

Wenu:

Abbas Mwalimu

+255 719 25 8484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook na WhatsApp).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: