Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Mwanza, Godwin Barongo akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye waakti wa ziara yake Wilayani humo.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Mwanza, Godwin Barongo wakati wa ziara yake wilayani Sengerema, Mwanza.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Silvanus Bulapilo akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati wa ziara yake wilayani humo mkoani Mwanza.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Sengerema kuhusu utekelezaji wa anwani za makazi na postikodi wakati wa ziara yake mkoani Mwanza

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiiano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameikataa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa Anwani za Makazi na Postikodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wakati wa ziara yake wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Nditiye ameikataa taarifa hiyo ya utekelezaji iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Godwin Barongo wakati akiwasilisha taarifa yake kwa kuwa haina utekelezaji wowote uliofanyika wa kuchagua majina ya mitaa ili Serikali iweze kuweka namba za nyumba, vibao kwa maelengo ya kukamilisha anwani za makazi na postikodi ili kila mwananchi apate anwani yake na atambulike mahali anapoishi.

Amefafanua kuwa mapema mwanzoni mwa mwaka huu aliambatana na Naibu Waziri wa ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara na kuwa na kikao cha pamoja baina ya madiwani na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Buchosa ambapo wataalamu wa Wizarani na wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) waliendesha mafunzo ya kujenga uelewa kwa madiwani na watendaji kwa malengo ya kuwawezesha kufanikisha kazi ya kuchagua majina ya mitaa ili kuweza kukamilisha anwani ya makazi kwa wananchi kwa kuwa tayari nchi nzima kila kata ina postikodi ambapo tangu wakati huo hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.

“Tunachohitaji ni majina ya mitaa, ninasikitishwa na suala la madiwani wanapopata ugumu wa kuchagua majina ya mitaa, ni lazima madiwani wakae tupate majina ya mitaa na ulikuwa na taarifa kuwa tunakuja ila hukufanya jitihada zozote kutekeleza,” amesema Nditiye.

Amesema kuwa Serikali itafikiria upya na kuamua kuchukua madaraka ya madiwani ili kuweka majina ya mitaa kwa kuwa sasa hivi simu zinatumika kufanya miamala mbali mbali na hii itasaidia huduma na bidhaa zifikishwe kwa wananchi kwa kuwa anwani za makazi na postikodi ni muhimu kwa uchumi na usalama wa nchi yetu na tunataka kila mwananchi atambulike anapoishi na tunahitaji utekelezaji kwa vitendo wa mpango huu kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Afisa Masoko wa Shirika la Posta mkoani Mwanza, Rose Kavemba amesema kuwa kinachohitajika ni kurasimisha mitaa, kupata majina kutoka kwa viongozi wa vijiji, mitaa na kwa madiwani kisha kutenga itakayowaongoza kufanya utekelezaji kwa kuwa kuna changamoto mkiwaachia madiwani wanavutana.

Naye Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Makazi na Postikodi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Jampyon Mbugi amesema kuwa ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, kila halmashauri inatakiwa iunde kamati kuendana na mwongozo wa mpango huo na kurasimisha mitaa ili kupata majina ya mitaa na barabara amabpo yanatakiwa yatoke kwa wakazi husika na kuridhiwa na mamlaka husika kisha kazi ya kuweka nguzo na namba za nyumba inaanza na taarifa zinakusanywa ili kuwekwa kwenye kanzi data na baadae anwani hizo zinaanza kutumika mathalani kwa kufanya biashara mtandao.

Barongo ameomba radhi na kuahidi kwa Nditiye kuwa watakaa kikao na kukubaliana majina ya mitaa. Vile vile, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Silvanus Bulapilo amesema kuwa majina ya mitaa yapo na mitaa ipo ila anashangaa ugumu unatokea wapi wa kutekeleza mpango huo.

“Nashangaa ugumu unatoka unatoka wapi wa kutekeleza hili, nikuahidi tutatekeleza, niombe nikuahidi kuwa tutafanya hivyo,” amesisitiza Bulapilo.

Nditiye amewataka viongozi na watendahi wote kushirikiana na madiwani wote kwenye maeneo mbali mbali nchi nzima kuhakikisha kuwa wanatekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi ili Serikali iweze kuwahudumia wananchi wake.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: