Balozi wa Tanzania, The Hague, Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju akitoa maelezo kwa mgeni aliyetembelea Banda la Tanzania wakati wa Tamasha maarufu kama Embassy Festival lililofanyika hivi karibuni. Tamasha hilo huandaliwa na Manispaa ya The Hague kwa kushirikiana na Balozi za nchi mbalimbali zenye Ofisi zake The Hague kwa lengo la kutangaza tamaduni za nchi hizo.
Balozi Irene Kasyanju (mwenye fulana kulia) pamoja na Mkuu wa Utawala katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Bibi Naomi Zegezege Mpemba (wa pili kushoto) wakitoa maelezo kuhusu Tanzania kwa wageni waliotembelea Banda la Tanzania, huku Bw. Denis Baraka (wa kwanza kushoto) ambaye ni Mtanzania na mdau wa shughuli za utalii ambaye kwa sasa anasoma nchini Ujerumani na ambaye kutokana na kupenda kutangaza utalii wa Nchi yake alisafiri kutoka Kiel, Ujerumani kuja Uholanzi kuungana na Ubalozi pamoja na Watanzania wengine kwenye Embassy Festival.
Mwonekano wa Banda la Tanzania na wageni waliotembelea.
Balozi Irene Kasyanju (wa tatu kushoto) akiwa na walishiriki wa maonesho ya mavazi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wakiwa wamevaa fulana za kuitangaza Tanzania ambao ni Bw. Issa Lupatu, Mwambata Fedha wa Ubalozi (wa pili kulia aliyevaa miwani) na Bw. John Appolo Kilasara,Katibu wa Chama cha Watanzania wanaoishi Uholanzi (Tanzanians in the Netherlands – TANE) ambaye pia ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha ISS nchini Uholanzi
Balozi Irene Kasyanju akiwa na Bi. Bahia Kihondo, Mtanzania aliyeandaa maonesho ya mavazi pamoja na watoto ambao walifungua maonyesho hayo kwa kusoma shairi fupi kwa lugha ya Kidachi na Kiswahili. 
Watazamaji wa maonesho ya mavazi yaliyotangaza utamaduni wa Mtanzania walikusanyika kwa
wingi kutazama maonesho hayo
Mwonekano wa Banda la Tanzania kwa sehemu ya ndani, likiwa limefurika Diaspora waliofika kulitembelea na kupata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Uholanzi, Bi Linda Mkony (aliyevaa koti katikati) na Bw. Denis Baraka, wakiwa pia wamevaana fulana maalum za kuitangaza Tanzania
Washiriki wakionesha vazi lenye michoro ya wanyama “animal prints” wanaopatikana kwenye mbuga za Tanzania kwa mtindo wa kisasa.
Maonesho ya mavazi yakiendelea– vazi la khanga.
Washiriki wa maonyesho ya mavazi wakiwa katika vazi la Kimasaai.

Ubalozi wa Tanzania The Hague, Uholanzi umeshiriki katika Tamasha maarufu la Embassy Festival lililofanyika mwezi Septemba, 2019. Tamasha hili huandaliwa na Manispaa ya The Hague kwa kushirikiana na Balozi za nchi mbalimbali zenye Ofisi zake nchini humo kwa lengo la kutangaza utamaduni wa nchi hizo.

Kama ilivyokuwa kwa balozi nyingine, Ubalozi wa Tanzania ulikuwa na banda lake kwa ajili ya kuonesha utamaduni wa Tanzania. Kwa kushirikiana na Watanzania wanaoishi Uholanzi (Diaspora), Ubalozi ulitumia fursa hiyo kutangaza utamaduni pamoja na vivutio vya utalii zikiwemo mbuga za wanyama.

Ubalozi uliandaa maonesho ya mavazi (fashion show) kwa kuonesha vazi la Kimasai (shuka na shanga, n.k.), pamoja na khanga. Aidha, Ubalozi uliandaa maonesho ya mavazi na vitambaa vyenye animal prints za Simba, Chui (The big five), Twiga na Pundamilia na kuvionesha kwa mtindo wa kisasa na hivyo kuvutia watu wengi.

Diaspora wajasiriamali walipata fursa ya kuuza bidhaa zao mbali mbali za asili kama vile khanga, chai, kahawa ya Tanzania, shanga, hereni, viatu na bangili. Watu wengi waliotembelea Banda la Tanzania walifurahia korosho, chai na kahawa vyote kutoka Tanzania vilivyokuwa vimeandaliwa mahsusi kwa ajili yao.

Ubalozi umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuitangazaTanzania kupitia tamasha hilo ambapo idadi kubwa ya watu walishiriki na kuchukua vipeperushi vya kutangaza utalii wa nchi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

2 comments:

  1. Safi sana.. Tunazidi kupaishwa kimataifa... #Mataga

    ReplyDelete
  2. Safi sana. Tunazidi kupaishwa kimataifa... #mataga

    ReplyDelete