Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi Vitambulisho Maalum kwa Ajili ya Mabalozi wa Mashina yaliyomo ndani ya Wilaya ya Kahama wakati wa Mkutano wa Ndani wa Viongozi wa Kamati za Siasa.
Baadhi ya Viongozi wa Kamati ya Siasa wa Majimbo yaliyomo ndani ya Wilaya ya Kahama wakifuatilia Hotuba ya Mlezi wao Balozi Seif Ali Iddi kwenye Mkutano wa Ndani wa Chama hicho.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alionya kwamba Chama cha Mapinduzi katu hakitamsamehe Mwanachama wake yeyote atakayekinyima Kura Chama hicho katika Chaguzi zijazo ili kulinda Heshima yake ya kuendelea kuongoza Dola ya Tanzania.

Alisema Chama hicho kikongwe Barani Afrika na Duniani kwa Ujumla kwa sasa kutokana na kukomaa kwake katika nyanja ya Kisiasa hakitastahiki kuchezewa ovyo na Wasaliti wenye sura mbili zenye muelekeo wa kukumbatia ubinafsi zaidi badala ya kuisimamia haki ya Wanachama waliowengi.

Balozi Seif Ali Iddi ambae ni Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa onyo hilo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za Siasa za Wilaya za Kahama, Shinyanga Mjini, Shinyanga Vijijini na Kishapu wakiwemo pia Wenyeviti wa Vitongoji, Kata, Makatibu Wenezi wa Matawi pamoja na Mabalozi katika Mikutano Miwili tofauti ya Ndani.

Alisema wakati umefika sasa kwa kila Mwanachama wa CCM kujizatiti kwa kujiandaa wakati utakapowadia kumchagua Mwanachama mwenzake mwenye Sifa na vigezo vinavyostahiki kupambana na upinzani wowote ule akiwa na nguvu imara ya kuwatumikia Wananchi Kizalendo wakati wote .

Balozi Seif alitanabahisha wazi kwamba hilo litapatikana na kufanikiwa vyema iwapo tabia ya kujenga tamaa ya fedha au msaada, kuzingatia urafiki au kukimbilia kuangalia Ujamaa wa karibu wakati wa zoezi la uteuzi miongoni mwa Wanachama litaepukwa kwa kuwekwa kando.

Alifahamisha kwamba Chama cha Mapinduzi kimebarikiwa kuwa na utaratibu muwafaka unaostahiki kufuatwa wakati wote. Hivyo Mwanachama asiyejiandikisha anapaswa kuelewa kwamba anainyima nguvu CCM katika harakati zake za Ushindi.

“ Inachefua kuona kwamba Wanachama tunakubaliana vyema mchana katika malengo na Mikakati yetu tunayojipangia lakini wakati wa usiku wengine hubadilika na kuwa Wapinzani wakishindwa kufahamu kuwa hiyo sio kasi ya CCM”. Alitahadharisha Balozi Seif.

Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga aliwakumbusha Wanachama na Wananchi wote Nchini kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wakati utapowadia wawe na Fursa na Haki ya kuitumia Demokrasia yao ya kuwachagua Viongozi wanaofaa kuwaongoza.

Alisema haiwezekani kabisa Mwanachama wa CCM anapita kujisifia Uanachama wake wakati hata Kadi ya kupigia Kura inayokipa Ushindi wa Chama chake hana.

“ Yule ambae anaumwa na Chama hicho cha Mapinduzi lazima aepuke fitina. Hii tabia ya kugombana kwenyewe kwa wenyewe inakuaje lakini?”. Aliuliza Balozi Seif.

Aliupongeza Uongozi, Wanachama wa CCM, Wapenzi wa Chama hicho pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa mapenzi yao ya kuiridhia CCM iendelee kushika hatamu kutokana na ushindi mkubwa uliopita wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara.

Alisema ushindi huo ulioshamiri katika pembe zote za Mitaa, Vitongoji na Vijiji ni ishara njema ya ushindi mnono wa Uchaguzi Mkuu ujao wa Mwezi Oktoba Mwaka huu na kuwataka Viongozi waliochaguliwa kufanya Kazi kwa bidii itakayokuwa kigezo na sifa ya kuelekea kwenye Ushindi huo.

Hata hivyo Balozi Seif aliwaonya Baadhi ya Wabunge wa Majimbo yaliyomo ndani ya Mkoa huo wenye tabia ya kuwachukia wenzao wa Viti Maalum waache tabia hiyo mbaya inayozusha makundi yasiyo na faida yoyote.

Alitahadharisha kwamba Uongozi wa Chama ngazi ya maamuzi hautosita kumuengua Mbunge ye yote atakayebainika kuanzisha makundi kwa tamaa na madaraka ilhali hana uwezo thabiti wa kuwatumikia wananchi.

Mapema Kamisaa wa Mkoa wa Shinyanga ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa huo Mheshimiwa Zainab Rajab Telak alisema Tamaa, urafiki au Ujamaa ni sifa zisizostahiki ndani ya CCM na zinapaswa kuondolewa kwa vile hubeba ubinafsi unaovuruga Chama na kusababisha Makundi.

Mh. Zainab alisema yapo matukio yaliyoshuhudiwa kutokea wakati wa Chaguzi za Serikali za Mitaa na yalileta doa ndani ya Chama kutokana na ba baadhi ya Wanachama wake wakiwemo baadhi ya Viongozi kung’ang’ani wateuliwe wapenzi wao wakielewa kwamba hawatakubalika katika Jamii.

Alisema vitendo hivyo viovu vinavyokwenda kinyume na Katiba, Sheria, kanuni na Taratibu za Chama cha Mapinduzi zinastahiki kuachwa mara moja vyenginevyo ni kuwaongezea kazi ya ziada Wanachama thabiti walioamua ndani ya nyoyo zao kukilinda na kukitetea Chama hicho.

Mh. Zainab Telak alisisitiza umuhimu wa kuendeleza sifa na Itikadi ya Uaminifu miongoni mwa Wanachama wenyewe ambao ndio jambo la msingi linaloweza kuleta ufanisi wakati wote na kujenga sifa ya Chama iliyokuwanayo inayosababisha Kundi kubwa la Wananchi kuendelea kukiamini kutokana na Sera zake zinazoleta Ukombozi wa Uchumi na Mabadiliko ya haraka ya Maendeleo.

Mapema wakiwasilisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika Kipindi cha Miaka Minne Wabunge wa Majimbo ya Wilaya zilizomo ndani ya Mkoa wa Shinyanga walisema zaidi ya asilimia 90% imeshafikiwa ya Utekelezaji huo kwenye Majimbo yao.

Walisema uimarikaji wa Huduma za Maji safi na salama, upatikanaji wa Huduma ya Umeme, uendelezaji wa Miundombinu katika Ujenzi wa Bara bara zilizomo kwenye Majimbo hayo ni uthibitisho wa mafanikio makubwa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 205 hadi 2019.

Hata hivyo baadhi ya Wabunge hao walibainisha kwamba bado zipo baadhi ya Bara bara zinaendelea kuwa changamoto kwa Wananchi wa baadhi ya Maeneo ya Mkoa huo wakati wa harakati zao za Kiuchumi katika Sekta ya Mawasiliano ya usafiri.

Kupitia Mkutano huo wamempongeza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Poombe Joseph Magufuli kwa usimamizi wake thabiti wa Ilani ya Uchaguzi katika sehemu mbali mbalki za Ardhi ya Tanzania.

Walisema Utumishi wa Dr. Magufuli uliotukuka umewezesha kuiletea Heshima kubwa Tanzania Kiuchumi na matokeo yake Miradi Mikubwa Nchini kwa sasa inatekelezwa kwa kutumia Fedha na Rasilmali za Taifa bila ya kutegemea sana msaada wa Mataifa na Washirika wa Maendeleo.

Akimkaribisha kuzungumza na Viongozi hao wa Mkoa, Wizaya, Majimbo, Mitaa, Vitongoji na Matawi Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Nd. Mabala Mlolwa alitoa tahadhari kutokana na mfumo wa baadhi ya Wanachama kuanza kujipanga kwa ajili ya kujiweka tayari ya kampeni za uchaguzi.

Nd. Mabala alisema Chama kimeweka Taratibu Maalum za mchakato mzima wa masuala ya Uchaguzi, lakini kwa wakati huu anayefanya hivyo aelewe kwamba anakwenda kinyume na Kanuni za Chama kitendo ambacho kinaweza kusababishia kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Alisema Shinyanga haihitaji kukipa tabu Chama cha Mapinduzi katika Ujenzi wa Chama na uimarikaji wake na ndio maana suala la kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu litazingatiwa katika nyanja zote ipatikane salama ndani ya Chama na Wanachama wenyewe.

Nd. Mabala Msolwa alibainisha kwamba Uongozi wa CCM Mkoa huo kwa sasa umejiwekea utaratibu kwa Viongozi wake kuhudhuria na Vitambulisho vya kupigia kura kwenye Mikutano yote itakayoandaliwa ya Chama hicho kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa hatua itakayothibitisha upatikanaji wa kura zake CCM .

Alisema wapo baadhi ya Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wanaokuwa mstari wa mbele kuhimiza Wanachama kujitokeza kwa wingi kupiga Kura wakati wao wenyewe hawana Vitambulisho vya kupiga kura kutokana na uzembe wao.

Katika Mikutano hiyo ya ndani ya Viongozi wa Mkoa, Wilaya, Majimbo hadi Matawi Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga alikabidhi Vitambulisho Maalum vilivyotolewa na Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya Mabalozi wa Shina vikilenga kujenga Heshima ya Chama.

Wakati huo huo Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Vitambulisho kwa Mabalozi 1,557 wa Tawi la Mgodi wa Mwadui wa Williamson Diamond Limited wakati akisalimiana na Viongozi na Wanachama wa Tawi hilo mara baada ya kuutembelea Mgodi huo.

Katika nasaha zake Balozi Seif ambae ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya CCM alisema Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo wanaojishughulisha na majukumu yako kwa kuelekeza nguvu zaidi katika kutatua kero zinazowakabili Wananchi wao inakuwa rahisi kwa CCM kujinyooshea nguvu za uwajibikaji.

Alisema majukumu hayo mbali ya kuijenga CCM kiushindi kwenye Chaguzi zozote zile lakini pia huwapunguzia maswali ya ajabu pale anaporejea tena kwa Wananchi kuomba ridhaa nyengine ya kuwatumikia katika kipindi kinachofuata cha Uongozi.

Balozi Seif alitanabahisha kwamba Mbunge au Kiongozi ye yote yule inapendeza pale anapomaliza majukumu yake ya uwajibikaji kwa Umma anaacha athari ya matendo mema yatakayomuwezesha kuendelea kukumbukwa kwa mema aliyoyaacha.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: