
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipunga mkono kuwaaga washiriki wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) baada ya kufungua mkutano huo kwa njia ya video kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Machi 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) kwa njia ya video kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Machi 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia washiriki wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) alioufungua kwa njia ya video kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Machi 18, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania kwa nafasi yake ya
Uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)imeendelea
kupaza sauti ya kuondoa vikwazo kandamizi vya kiuchumi vilivyowekwa
katika Jamhuri ya Zimbabwe.
Amesema ili wasiache hata mmoja wao nyuma wanapoelekea kwenye utekelezaji wa Ajenda ya SADC ya baada ya mwaka 2020 yaani SADC Post 2020 Agenda, ni vyema wakaendelea kuisemea Zimbabwe katika majukwaa mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa hadi vikwazo hivyo vitakapoondolewa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatano,
Machi 18, 2020) wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo
umefanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya kimtandao (video conference).
Amesema kama ilivyokubalika katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na
Serikali na kongamano la kihistoria lililowakutanisha wadau wa Kitaifa
na Kimataifa na nchi rafiki kwa ajili ya kupaza sauti kwa kauli moja juu
ya nchi hiyo kuondolewa vikwazo, wanapaswa kuendelea hivyo hadi vikwazo
vitakapoondolewa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kuwa SADC inaamini
katika ulinzi, usalama na misingi bora ya kidemokrasia katika kutekeleza
malengo yake, hivyo masuala hayo ni ya msingi na ndiyo yatakayowezesha
kuendeleza mikakati waliyojiwekea.
Amesema katika miaka 40 ya umoja na
ushirikiano wao, wameweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo kwa nchi
zao. “Miradi mbalimbali ya miundombinu imeendelea kutekelezwa na
tumeiwekea kipaumbele sekta ya viwanda ambayo ni nguzo ya msingi katika
kusaidia kukua kwa uchumi wa kanda na wa kila mmoja wetu.
”Vilevile,
Waziri Mkuu amesema masuala ya kijamii kama elimu, afya, jinsia na
mazingira yameendelea kutekelezwa, ambapo alimnukuu Mwenyekiti wa SADC
Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika hotuba yake aliyoitoa wakati
anakabidhiwa Uenyekiti tarehe 17 Agosti 2019.
Alisema “.....malengo ya
umoja wetu kama yalivyoasisiwa na Wazee wetu wakati SADC inaundwa, bado
hatujayafikia, na iwapo juhudi za dhati na za pamoja hazitachukuliwa,
itachukua muda mrefu malengo haya kuyafikia....”. Mwisho wa kunukuu.
Waziri Mkuu amesema ni dhahiri kuwa wameendelea kupiga hatua kubwa hadi
sasa, lakini wanapaswa kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji ili
wahakikishe kuwa malengo ya SADC yanafikiwa. “Changamoto
tunazozipitia ni nyingi ikiwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, tofauti za
kisera na kimkakati baina ya Nchi Wanachama, gharama za kufanya biashara
na ushiriki hafifu wa sekta binafsi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema
jumuiya hiyo kwa sasa iko katika maandalizi ya kuwa na mkakati mpya wa
utekelezaji wa yale yote wanayoazimia kwa miaka kumi ijayo yaani mkakati
wa mwaka 2020 hadi 2030.
Amesema mkakati huo utahakikisha wanafikia
malengo ya dira ya SADC ya miaka 30 ijayo kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka
2050. “Sote tunaamini kuwa mkakati huu mpya tunaojiwekea utazingatia
changamoto hizi na nyingine nyingi ili kuweza kufikia malengo
yaliyokusudiwa.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuziomba na kuzisisitiza nchi wanachama zishiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wanapata mikakati inayotekelezeka na inayozingatia mahitaji ya kila mmoja wao na ya Kanda kwa ujumla. “Ni matumaini yangu kwamba majadiliano na maazimio ya mkutano huu wa Baraza la Mawaziri yataisogeza mbele Jumuiya yetu. Nimeona mna ajenda muhimu mbele yenu kwa ajili ya mustakabali wa Jumuiya hii. Niwaombe mzijadili kama inavyostahili na kutoa mwelekeo wa kisera ipasavyo.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mkutano huo unafanyika kwa njia ya mtandao kufuatia ushauri na mapendekezo waliyoyapokea kutoka kwa Mawaziri wa Afya wa Nchi Wanachama wa SADC walipokutana kwa dharura Dar es Salaam tarehe 9 Machi, 2020 kwa ajili ya kujadili mlipuko wa corona.
Profesa Kabudi amsema kupitia mikutano hiyo, Jumuiya imeendelea kuimarika kwa kupitisha maazimio na mikakati mbalimbali itakayowezesha SADC kujizatiti ipasavyo na kuleta mchango na maendeleo yanayotegemewa na nchi wanachama.
“Nazishukuru nchi zote za SADC kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa Sekretareti ya SADC na kwa Tanzania wakati waMaandalizi ya Mikutano ya kisekta. Ni matumaini yangu kuwa maazimio na mikakati iliyotokana na mikutano hiyo itasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo.”
Amesema pamoja na mafanikio hayo, SADC imeendelea kukumbana na changamoto nyingi ikiwemomigogoro ya kisiasa, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili, ukuaji wa idadi ya watu, ukuaji wa miji, elimu, afya, kupungua kwa kasi ya uchumi, na masuala ya utawala. “Changamoto hizi siyo mpya na kadri tunavyosonga mbele, kila mojawapo inakuwa ndiyo chachu ya kuboresha maisha ya Wanajumuiya na hatimaye kuleta ustawi kwa wananchi wetu.”
Awali, Katibu Mkuu wa SADC, Bibi Stergomena Tax alizipongeza nchi wanachama wa jumuiya hiyo kwa hatua mbalimbali walizozichukua katika kukabiliana na mlipuko ugonjwa wa homa ya mapafu ulioikumba dunia ambao unaosababishwa na virusi vya corona.
Toa Maoni Yako:
0 comments: