Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dk. Angelina Lutambi, akizungumza na wakuu wa shule za sekondari na maafisa elimu kata katika kikao kazi kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Mwenge mkoani hapa.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Nelasi Mulungu, akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.

Na Mwandishi Wetu, Singida

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida Dk. Angelina Lutambi amewataka wakuu wa shule na maafisa elimu kata mkoani hapa kufanya kazi kwa bidii ili kubadilisha mitazamo ya jamii zinazozunguka shule zao.

Lutambi aliyasema hayo jana katika kikao kazi cha wakuu wa shule zote za Sekondari na maafisa elimu kata kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Mwenge ambacho kililenga kufanya tathimini ya matokeo ya kidato cha nne na kidato cha pili Mwaka 2020.

Katibu Tawala huyo alisema wakuu wa shule ni chachu ya mabadiliko kwenye jamii inayowazunguka ,wanafunzi wanapomaliza shule na kurudi kwa jamiii hivyo kama jamii haijabadilika ni ishara kwamba walimu na wakuu wa shule hawakutimiza wajibu wao.

Akifafanua zaidi umuhimu wa wakuu hao katika kuibadilisha jamii katibu tawala huyo alieleza kuwa jamii ikibadilika ulinzi na usalama wa jamii na taifa unaimarika kutokana na wengi kusoma na kupata shughuli ya kufanya na kusababisha tatizo la vitendo vya uvunjaji wa amani kuisha.

Hata hivyo aliwataka wakuu hao na maafisa elimu kata kubadilika katika utendaji wao wa kazi kwani Serikali ya awamu ya tano inawapatia posho kila mwezi na maafisa elimu kata wamepata pikipiki kwa ajili ya kurahisisha ufanyaji kazi hivyo kila kiongozi ajitathmini kwa kina kama anatosha katika nafasi yake aliyonayo.

"Mtambue kuwa wapo walimu wengi mtaani wenye sifa kama za kwenu na pengine zaidi yenu. Hivyo nikibaini Kiongozi hawajibiki nitamuondoa katika nafasi ya uongozi ili kupisha walimu wengine watakao fanya vizuri." alisema Dk. Lutambi.

Kwa upande wa miradi alisema Serikali ya Rais Dk. John Magufuli imetoa fedha bilioni 5.4 katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu mkoani hapa na fedha hizi zinaenda moja kwa moja shuleni ili kuondoa urasimu katika matumizi ya fedha hizo huku akiwataka wakuu wa shule na maafisa elimu kata kusimamia fedha hizo kwa uadilifu na kumaliza miradi hiyo kwa wakati.

Aidha Dk. Lutambi aliwakumbusha viongozi wote kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Rehema Nchimbi alilolitoa Januari 26 mwaka huu alipozunguza na wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya na Wakurugenzi juu ya kampeni yenye lengo la kuondoa changamoto ya upungufu wa madawati na madarasa ifikapo Februari 26 mwaka huu.

Awali akimkaribisha katibu tawala mkoa, Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Nelasi Mulungu aliagiza kila shule ni lazima iwe na miradi ya Elimu ya Kujitegemea (EK) kwani Rais amekuwa akitafuta fedha kwa ajili ya miradi lakini walimu wakuu na wakuu shule licha ya kuwa na maeneo makubwa wamekuwa hawayafanyii miradi yoyote.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: