Na Agness Francis, Globu ya jamii.

ZIKIWA zimesalia Siku nne kuelekea mpambano wa watani wa jadi Simba na Yanga kufanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar as Salaam, Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) limemtangaza mwamuzi wa kati atakayecheza mechi hiyo.

Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es salaam, Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema kuwa mchezo huo utakaoanza saa 11 jioni utachezeshwa na mwamuzi kutoka Mkoani Kagera Jonesia Rukyaa (pichani) mwenye beji ya FIFA, akisaidiwa na waamuzi wa pembeni Ferdinand Chacha wa Mwanza na Mohamed Mkono kutoka Tanga, huku msaidizi wa mezani akiwa Heri Sasii.

Mwamuzi Jonesia ndiye aliwachezesha Simba na Yanga katika msimu wa 2016/17 ambapo Yanga waliibuka kidedea kwa kuondoka na ushindi wa goli 2-0.

Ikumbukwe Jonesia aliteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kuchezesha fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa wanawake (Algarve Cup) zitakazofanyika nchini Ureno, mwezi Februari hadi Machi Mwaka huu. Kwa hiyo siyo mtu wa mchezo mchezo.

Mchezo huo wa Ligi kuu wa Tanzania Bara (TPL) utachezwa Septemba 30 siku ukiwakutanisha miamba ya soka Nchini Simba na Yanga kuanzia majira ya saa 11 jioni. Mbali na michezo huo kutakuwa na mechi zingine za ligi kuu zitakazoendelea kwenye viwanja tofauti kuanzia kesho Alhamisi mpaka Jumamosi kukamilisha mzunguko wa nane na wa tisa.

Katika kuelekea mchezo huo wa vuta nikuvute kikosi cha Simba kilichoweka kambi yake jijini Dar es Salaam kitamkosa mshambuliaji wake mahiri John Boko aliyepewa kadi nyekundu katika mchezo uliopita na mwadui fc. Yanga wako mji kasoro bahari Morogoro kwa matayarisho ya mtanange huo.

Michezo iliyopita simba walitoka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wachimba Madini Mwadui ya Shinyanga, Yanga wakiibuka kidedea kwa kuwafunga walima alizeti Singida United mabao 2-0.

Kurwa na Doto hao wametofautiana pointi mbili ambapo Yanga ana alama 12 wakiwa wamecheza michezo 4, huku wekundu wa msimbazi Simba wana pointi 10 michezo 5 ligi kuu Tanzania bara TPL. Timu hizo zimekutana kwa mara ya mwisho ligi kuu ya msimu wa 2017/18 Simba wakitoka na ushindi wa goli 1-0 goli likifungwa na Erasto Nyoni.

Mashabiki wa pande zote mbili wakiwa na shauku kubwa ya siku hiyo kushuhudia mchezo huo utakopigwa jumapili hii Septemba 30, 2018 majira ya saa 11 jioni kujua nani mbabe kati ya majirani hao wa Kariakoo kwa kiingilio cha VIP A 30,000,VIP B na C 20,000,kwa viti vya bluu, kijani na rangi ya chungwa ni 7,000.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: