Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akipokea tuzo ya Kimataifa ya kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza Duniani toka kwa Makamu Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani(WHO) Dkt.Soumya Swaminatha Mjini New York, Marekani.
---
SERIKALI ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepata Tuzo ya Kimataifa ya kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) kama vile Kisukari, Shinikizo la Damu, Magonjwa ya Moyo na Saratani.

Tuzo hiyo ya Kimataifa, imekabidhiwa leo tarehe 27 Septemba, 2018 kwa Waziri ya Afya Mhe. Ummy Mwalimu na Kikosi kazi maalumu cha Umoja wa Mataifa mahususi kwa kupambana na Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (UN Interagency Task
Force on the Prevention & Control of NCDs- UNIATF). Hii ni kutokana na juhudi za Wizara ya Afya za kupambana dhidi ya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD), hususan kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.

Tuzo hiyo ya kimataifa ya mwaka 2018, imekabidhiwa kwenye mkutano wa wa viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa (United Nations High Level Meeting on NCDs) unaofanyika Mjini New York, Marekani.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tisa Duniani ambazo zimefanikiwa kupata tuzo hiyo ambayo imetolewa kwa mara ya kwanzakatika ngazi ya Kiserikali Dunianii, na ilichaguliwa kupata tuzo hiyo baada ya mapendekezo yaliyoandikwa na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza vya Tanzania (TANCDA). Hii ni kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe Rais Dr. John Pombe Magufuli katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata habari ya namna ya kujikinga na magonjwa haya.

Timu ya UNIATF imeipongeza Tanzania kwa kuanzisha programu ya kuhamashisha jamii kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha yao ya kila siku.

“Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (NCD) ndiyo yanayoongoza duniani kwa sasa kwa kusababisha ulemavu na vifo vingi. Nchini Tanzania asilimia 34 ya Vifo vilivyorekodiwa Hospitali mwaka 2017 zimesababishwa na magonjwa haya. Isitoshe kupambana na NCD ni miongoni mwa mikakakati ya Mpango wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu (SDG) ya kupunguza kwa theluthi moja vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ifikapo mwaka 2030. Amesema Waziri Ummy.

Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza ni magonjwa sugu au ya muda mrefu, ambayo hayawezi kuambukizwa kwa maana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Magonjwa hayayapo mengi nayo ni kama vile kisukari, saratani, shinikizo la damu na mishipa ya fahamu, magonjwa sugu ya mfumo wa hewa, magonjwa sugu ya figo, macho na meno, selimundu (siko seli) na mengineyo.

Waziri Ummy amelishukuru Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza la Tanzania (TANCDA) baada ya kuandika andiko la kuitambulisha Dunia kuhusu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, na dunia kuona umuhimu wa juhudi hizo.

Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kwa kushirikiana na TANCDA na wadau wengine inaamini mikakati madhubuti, Sera mbalimbali za afya zikiwekwa, kutekelezwa na kuhakikisha Watanzania wanakuwa na elimu sahihi ya kujikinga na kuyadhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, itaboresha afya ya wananchi.

Imetolewa na;
Catherine Sungura
Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (Afya).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: