Na Andrew Chimesela - Morogoro 

Mkuu wa Mkoa wa morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewazuia Wajumbe wa Bodi ya Hifadhi ya Jumuiya ya Kuhifadhi na matumizi Bora ya Maliasili Ukutu (JUKUMU) wanaomaliza muda wao kutoshiriki nafasi zozote kwenye uchaguzi ujao kwa madai kuwa wameshindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yao kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Dkt. Kebwe ametoa kauli hiyo jana Februari mosi, wakati akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Mbwade Wilaya ya Morogoro Mkoani humu akiwa katika ziara ya kawaida ya kutembelea miradi ya maendeleo na nkusikiliza kero za wananchi.

Dkt. Kebwe amesema Viongozi hao kwa kiasi kikubwa ndio walioifikisha JUKUMU mahali ilipo kuwa na migogoro mingi isiyoisha na kwamba ili kuijenga upya jumuiya hiyo ya JUKUMU ni lazima kupata viongozi wengine wapya na waadilifu wa kuiendesha na kuisimamia.

“Viongozi wote waliokuwepo na nimepiga marufuku kama amefanya miaka kumi Katiba imekwisamuondoa, kwa hiyo hata mwenyekiti wa JUKUMU amekwishatoka kwa mujibu wa Katiba” amesema Dkt. Kebwe. “ lakini hata wale walikwisha tumikia miaka mitano…wasiombe na na wakiomba wasikubaliwe” alisisitiza.

Aidha, Dkt. Kebwe hakuridhika na taarifa ya fedha ya mapato na matumizi ya Jumuiya hiyo ya zaidi ya Shilingi 388 Mil. iliyosomwa kwake kwani alisema kuna harufu ya ubadhirifu wa fedha, kwa sababu hiyo ameagiza ufanyike ukaguzi wa ndani wa mapato na matumizi ya fedha hizo watakaobainika kutumia vibaya fedha hizo watachukuliwa hatua za kisheria.

Mwisho, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Kayombe Masoud Lyoba kutuma wataalamu wake kuweka mipaka ya eneo lote la Jukumu ili iwe rahisi kwa wananchi kutambua mipaka yake na kutoingia katika hifadhi hiyo kufanya shughuli za kibinadamu. 

Sambamba na suala la JUKUMU Mkuu wa Mkoa pia alitembelea ujenzi wa vituo vya Afya vya Duthumi na Mkuyuni Wilayani humo na kurudia kauli yake ambayo amewahi kutoa akiwa Wilayani Kilosa na Gairo ya kuendelea na kazi za ujezi wa vituo vya Afya kwa kasi na kujenga usiku na mchana kwani haoni sababu ya kuchelewesha ujenzi huo wakati fedha zipo.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo pamoja na kupokea maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na kuahidi kuyatekeleza ikiwa ni pamoja na kusimamia uchaguzi wa Wajumbe wa Bodi ya JUKUMU lakini pia alitumia fursa hiyo kuhamasisha ugawaji wa Vitambulisho kwa wajasiliamali wadogo ili wafanye shughuli zao bila kusumbuliwa.

Naye Afisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro Bw. Joseph Chuwa amesema Hifadhi ya Jamii ya Jukumu yenye ukubwa wa karibu Km 640 na kuzungukwa na vijiji 11 ni kati ya Hifadhi za Jamii 38 nchini ambayo iliazishwa mwaka 1996 ikiwa na malengo ya kuwashirikisha wananchi wa vijiji husika kuhifadhi wanyamapori na kuleta faida kwa vijiji hivyo kwa njia za Utalii na matumizi mengine ya rasilimali za wanyamapori.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: