Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo akizungumza na walipakodi katika Ofisi ya TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam kuhusu wito wa kujitokeza kulipa kodi za mapato, majengo na kodi za ongezeko la thamani kwa wakati ili kuepuka usumbufu, riba na faini.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Richard Kayombo akizungumza na mmoja wa walipakodi katika Ofisi ya TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea ofisini hapo kuwahimiza walipakodi kulipa kodi za mapato, majengo na ongezeko la thamani kwa wakati ili kuepuka usumbufu, riba na faini.
Mkazi wa Mwanagati, Nyamizi Mgawe akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam wakati Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Richard Kayombo alipotembelea ofisini hapo kuwahimiza walipakodi kulipa kodi za mapato, majengo na ongezeko la thamani kwa wakati ili kuepuka usumbufu, riba na faini.

Na Veronica Kazimoto,Dar es Salaam.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo kote nchini kulipa kodi kwa wakati hususani Kodi ya Mapato awamu ya kwanza, Kodi ya Majengo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambapo huu ndio muda muafaka wa kulipa kodi hizo. 

Akizungumza na walipakodi katika Ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi, Richard Kayombo amesema kodi ya ongezeko la thamani inatakiwa kulipwa ifikapo Machi 20 mwaka huu, kodi ya mapato inatakiwa kulipwa kabla ya tarehe 30 Machi, 2019 wakati mwisho wa kulipa kodi ya majengo ni mwezi Juni, 2019.

“Ninachukua fursa hii kuwahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo mliopo hapa na wale watakaosikia taarifa hii kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwahi kulipa kodi hizi kwa wakati ili kuepuka usumbufu na hatimaye kujikuta mnatozwa faini na riba," alisema Kayombo.

Amesema kuwa, viwango vya kodi ya majengo ni shilingi 10,000 kwa nyumba za kawaida, shilingi 50,000 kwa kila sakafu ya ghorofa na shilingi 20,000 kwa nyumba za ghorafa zilizoko vijijini.

"Tunaona serikali imepunguza kiwango cha kodi ya majengo, hivyo hakuna sababu ya watu kuchelewesha na kusubiri dakika za mwisho, tulifanye suala la ulipaji kodi kuwa utamaduni wetu kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza Kayombo.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Kayombo amewatahadharisha walipakodi kuhusu uwepo wa watu wanaotumia jina la mamlaka hiyo kufanya utapeli kwa kujitambulisha kuwa ni maofisa wa TRA wakidai kwenda kukagua ulipaji wao wa kodi.

“TRA ina utaratibu wake wa kuwasiliana na wafanyabiashara na kuwajulisha siku rasmi ambazo maofisa wetu watakwenda kufanya ukaguzi na unafanyika kwa uwazi bila vitisho na si kwa taratibu nyinginezo,”alisema Kayombo

Ameongeza kuwa, "kama mtu atapigiwa simu au kama una mtu una wasiwasi nae tafadhali toa taarifa kwa ofisi zetu zilizopo karibu nawe au toa taarifa Kituo cha Huduma kwa Wateja namba 0800 780 078 au 0800 750 075 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa moja usiku na utupe namba ya mhusika ili tuweze kufuatilia.

“Pia kuna namba ya Whatsapp ambayo unaweza kutoa taarifa au kuuliza chochote kupitia namba 0744 233 333 ambayo ni maalum kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi na kuwawezesha kulipa kodi kwa wakati,” alisema Kayombo.

Richard Kayombo amesema kuwa, tangu mwezi Desemba mwaka jana, TRA imekuwa ikipata malalamiko kutoka kwa watu tofauti tofauti ambao wamekuwa wakitapeliwa fedha na maofisa feki wanaodai kufanya kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: