WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Machi 5, 2019) amewaongoza wakazi wa jijini la Dar es Salaam katika mazishi ya Imamu wa Msikiti wa Mtoro Sheikh Zubeir Yahya Mussa yaliyofanyika katika makaburi ya Kisutu.

Sheikh Zubeir ambaye ni miongoni mwa masheikh maarufu jijini Dar es salaam alifahamika sana kutokana na kuwa Imamu wa msikiti huo, ambao ni miongoni mwa misikiti mikubwa na maarufu zaidi hapa nchini, alifariki dunia jana usiku.

Pamoja na Uimamu wake, Sheikh Zubeir aliwavutia watu wengi sana kutokana na darasa zake alizokuwa akiziendesha kwa ufundi mkubwa katika msikiti huo wa Mtoro na maeneo mengine.

Sheikh Zubeir alikuwa miongoni mwa masheikh waliojiweka karibu sana na jamii na kuwa na uhusiano mzuri na masheikh wenzake kutoka taasisi mbalimbali.

Sheikh Zubeir alipata elimu yake ya juu katika chuo kikuu cha Madina, (Ummul- Quraa) akiwa pamoja na Sheikh Juma Omar Poli, Sheikh Muharram Juma Doga, Sheikh Abdallah Ahmad Bawazir na wengineo.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Mbunge wa Kibaha Vijijini, Abuu Jumaa, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: