Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Mbunge wa Mtwara Vijijini Hawa Ghasia pamoja na Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mtwara wakivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi la mradi wa Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara hafla iliyofanyika leo tarehe 2 Aprili 2019 mkoani humo. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakwanza kutoka kulia pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Ujenzi, Wabunge pamoja na viongozi wa mkoa, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mitambo itakayotumika katika ujenzi wa mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika eneo la uwanja wa ndege wa Mtwara kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa uwanja huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na wananchi waliofika katika uwanja wa ndege wa Mtwara mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la mradi wa Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara hafla iliyofanyika leo tarehe 2 Aprili 2019 mkoani humo. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa kushoto pamoja na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isaack Kamwelwe kulia wakati Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Mtwara na Dar es Salaam ilipoku wa ikitumbuiza uwanjani hapo. PICHA NA IKULU.

Na. Paschal Dotto-MAELEZO.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege Mtwara na kuagizi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.Philipo Mpango, wakutane ndani ya siku tano ili kutoa pesa ya mradi wa ujenzi huo kwa Mkandarasi.

Rais Magufuli alisema kuwa aslimia 15 ya pesa za mradi huo ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 7.5, zinatakiwa kutolewa ndani ya siku tano ili kumwezesha mkandarasi kuendelea na kazi na kumaliza kazi kwa muda uliopangwa kwenye mkataba wa mradi huo.

“Mimi leo naagiza, wewe Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Waziri wa Fedha na Mipango, asilimia 15 ya pesa za mradi huu ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 7.5,ziwe zimefika hapa ndani ya siku tano, kwa sababu najua fedha hizo zipo sasa kwa nini mkandarasi hajaletewa pesa hizo”, Rais Magufuli alisema.

Rais Magufuli amlitaka Mkandarasi huyo kufanya kazi yake kwa umakini mkubwa mara atakapopata pesa hizo za mradi asilimia 15, huku ikielezwa kuwa mradi mzima utagharimu Shilingi bilioni 50.4 mpaka kukamilika kwa mradi mwaka 2020, pia imeelezwa mradi uko nyuma ya muda.

“Nataka akishapata pesa hizo afanye kazi usiku na mchana na siyo kubabaisha kama alivyofanya katika Uwanja wa Ndege Mwanza, ingawa sasa yuko asilimia 98 kumalizia mradi ule, ila mwanzoni alisuasua, sasa nakueleza Waziri wa Ujenzi, Mkurungezi Mtendaji, Tanroad na Mkandarasi wa mradi huu, mfanye kazi usiku na mchana, najua mpaka sasa hivi mmeishachelewa siku kadhaa, lakini wananchi wa Mtwara wanataka kuona uwanja umekamilika”, Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alieleza utekelezaji wa miradi mingine ya Serikali kwa wananchi wa Mtwara, ikijumuisha ujenzi wa mradi wa barabara ya Mikindani, kilometa 3, stendi, kadhalika maeneo ya kupumzikia, soko, pamoja na mfereji wa maji, itagharimu Tsh.bilioni 23.843.

Miradi mingine ni ukarabati ama ujenzi wa vituo vya afya, utakaogharimu Tsh.bilioni 10.3, lakini pia utekelezaji wa mradi wa maji wa Makonde ambao utakarabatiwa na kuwa nguzo ya upatikanaji wa maji katika miji ya Newala, Nanyumbu, Tandahimba, Mtwara na vijiji 309.

“Nafahamu kuwa moja ya changmoto katika mkoa huu ni upatikanaji wa maji kwani kwa sasa ni asilimia 4, ingawa kwa mjini ni asilimia 80, lakini tatizo hili linasababishwa na uchakavu wa miundombinu katika mradi wa maji wa makonde, kwani mahitaji ya maji katika meneo haya ni lita za ujazo milioni 18.3 wakati mradi una uwezo wa kuzalisha lita milioni 24.3, lakini kutokana na uchakavu, mradi huu hutoa lita milioni 6.7, kwa hiyo asilimia 60 ya maji inapotea”, Rais Magufuli alisema.

Katika utekelezaji wa miradi ya maji kwa miji 28 nchini, ambapo Serikali inapata mkopo wa kugharamia miradi hiyo kutoka Serikali ya India, zikiwa zaidi ya Trioni 1.2, mradi wa maji makonde umetengewa dola za Kimarekani milioni 70, sawa na Tsh.bilioni 160.

Rais Magufuli pia alisema kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa kuwalipa wakulima wa korosha katika mikoa ya kusini wanakozalisha korosho, huku wakulima 39,765 waliokuwa na korosho chini ya kilo 1500 ambazo zilikuwa ni tani 16,669.3, walitengewa Tsh.Bilioni 521.8 na baada ya uhakiki walilipwa pesa zao.

“Watanzania sisi ni wataalam kwenye hewa, kwa hiyo ilibidi tukae macho tusije tukawa na korosho hewa tukalipa malipo hewa, ndiyo maana tulihakikisha kila mkulima anafanyiwa uhakiki ili kupata haki yake”, Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliongeza kuwa wakulima 373,149 wamelipwa, kwa hiyo asilimia 99 ya wakulima wenye korosho chini ya kilo 1500 wamelipwa, huku uhakiki wa wakulima wenye kilo zaidi ya 1500 ambao walikuwa 18,103, waliobainiwa kwenye uchambuzi wa pili umekamilika na wataanza kulipwa, lakini katika hao, majina 780 walikuwa hawana mashamba wala mikorosho.

“Najua kuna watu wamenunua korosho tangu zikiwa mashambani, ninafahamu imekuwa ni biashara ambayo inaendelea huko japo siyo biashara nzuri kwa sababu imekuwa ikiwadhulumu wananchi, kwa wale watakaokiri kwamba wao ni makagomba Serikali itawasamehe na kuwalipa pesa zao”, alisema Rais Magufuli.

Akihimiza malipo kwa wakulima, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Waziri wa Kilimo kupeleka bilioni 50 kuanzia kesho ili wakulima wenye korosho zaidi ya kilo 1500 waanze kulipwa mara moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: