Kiasili na kitamaduni, mwanaume hupenda kutawala ama kuhisi anatawala.

Mwanaume akiona ama akihisi anatawaliwa na mwanamke, hata akiacha kusema hujikuta akianza kujihisi vibaya kuhusu nafsi yake na hatimaye kuhusu huyu mwanamke anayehisi anamtawala.

Katika uhusiano wanawake wengi hukosea kwa kuamini, ukali ama kuwa na maneno mengi ya kuudhi ni njia nzuri ya kupambana na wanaume zao katika yale mambo wanayowahisi.

Kitu wanachosahau kukiwaza ni kwamba wanaume huchukia kufokewa, kufanywa wajinga na kuhisi wanatawaliwa na wanawake.

Na mwanamke mwenye tabia hizo za kufoka kwa mume ama mpenzi wake, tabia ya kujihisi anamtawala mume wake sio tu anamtesa mume wake kifikra ila pia anatengeneza mazingira ama ya huyu mwanaume kuachana naye, kuwa na mwanamke wa pembeni ama kupenda kukaa mbali na mwanamke huyu.

Wanaume wengi wakiwa kazini wanajikuta wako huru na amani zaidi kuliko wakiwa na wake zao. Pia wako wanaume wengi msisimko wa kihisia na wapenzi wao umeisha ama umepungua kwa asilimia kubwa kwa sababu ya kauli na tabia za ubabe walizonazo wanawake wao.

Nimewahi kuandika mada hapa kuhusiana na namna mwanamke anavyotakiwa kuwa. Nilisema silaha ya mwanamke si kauli kali wala ubabe.

Mwanamke kajaliwa ngozi laini, sauti nzuri na uwezo mkubwa wa kucheza na hisia za mwanaume.

Vitu hivi mwanamke anapaswa kuvitumia vema ili kumfanya mume wake abadilike na si kujifanya mjuaji karibu kwa kila kitu.

Hakuna mwanamke aliyeshinda katika vita ya kutunishiana misuli na mume wake. Mwanamke hajaumbwa hivyo.

Sifa ya mwanamke ni kudeka, kumfanya mwanaume ajihisi mwenye hatia kwa sauti ama matendo yake.

Ukileta ujuaji kwa mwanaume si tu unashindwa kufanikiwa katika lengo lako pia unamfanya naye awe juu zaidi na kusababisha mahusiano mengi katika gharika.

Wanawake ni vema wakafahamu kwamba wanaweza kubadili tabia na misimamo ya wanaume kwa matendo yao ya kike sio kuiga tabia za kiume.

Mwanaume anapofokewa na mwanamke mambo mawili huja akilini kwake haraka. Kwanza atafikiri mwanamke husika anamfanya mjinga. Pili atafikiri kutafuta sehemu nyingine apate utulivu na amani.

Ijulikane pia kwamba mwanamke anapokuwa na tabia zinazomkwaza sana mwenzake, ni sababu pia hata kiwango cha muhusika kujali na kuheshimu kupungua kama si kuisha kabisa.

Mwanaume anapokuwa na mwanamke, hutegemea mwanamke huyo kuonesha uanamke wake katika tabia kauli na maamuzi yake.

Sio anakuwa mwanamke kwa jinsia huku matendo na tabia zinakuwa za kiume hapana. Sifa ya mwanamke ni kubembeleza na kunyenyekea.

Mwanamke anapokosewa harushi ngumi kwa mumewe ila hutenda ama husema mambo ambayo yatamfanya mwanaume husika ajihisi mkosaji ama mjinga.

Ukileta ubabe kwa mwanaume, mwanaume husika atataka kukuonesha wewe na yeye nani mbabe zaidi. Sasa hayo mahusiano gani?

Kauli na maneno ya kuudhi sio sifa ya mwanamke. Tathmini zinaonesha wanawake wengi wakorofi huwa hawadumu katika mahusiano na wachache wenye kudumu huwa hawako katika mahusianio yenye kuleta raha na furaha.

Matarajio ya mwanaume kwa mwanamke ni kusikia sauti ya kubembelezwa, kuona akiulizwa kwa upole na kwa heshima, ni kuona akipapaswa huku wakicheka kwa pamoja.

Sasa mwanaume anapokutana na ubabe kama anauona mtaani ama kazini kwake, hujiona kakosea sana kuwa na mwanamke husika ama anakosewa mno na mwanamke husika.

Wanaume wengi hukutana na mazingira ya kibabe na kifedhuli katika harakati zao za kimaisha. Hufokeana na mabosi ama wafanyakazi wenzao, hukutana na utata karibu kila eneo la maisha yao.

Mwanaume huyu anataka akifika nyumbani akutane na hali tofauti. Zile kero, maneno makali ya kazini ama katika biashara zake anataka yaje kumalizwa kwa kusikia sauti ya upole na iliyojaa utani kutoka kwa mwanamke anayempenda na kumuheshimu.

Sasa akifika nyumbani na kukutana na balaa kama lile alilokutana nalo katika harakati zake za maisha unafikiri atawaza nini?

Kila binadamu anahitaji faraja. Na kwa zaidi ya asilimia 70 tunategemea faraja hizo kutoka kwa watu tunaowapenda na kuwajali.

Sasa tunapokutana na kinyume cha faraja kwa watu hao, tunajikuta hata ule msisimko tuliokuwa nao juu yao huisha na kujiona tuna bahati mbaya sana.

Hiyo ndio njia pekee ya kuijenga nyumba yako
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: