Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy akiwa na Kamishna Mhifadhi wa Misitu Profesa Dos Santos Silayo katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira asili ya Kalambo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea maeneo ya hifadhi za misitu na mashamba ya miti ya serikali. 
Maporomoko yaliyo katikaMsitu wa Hifadhi ya Mazingira asili ya Kalambo.


Na Mwandishi Wetu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy amesema taasisi hiyo inafanya kazi kubwa kuhakikisha inasimamia rasilimali za misitu zilizopo ili ziwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho. 


Brigedia Jenerali Mkeremy ameyasema hayo akiwa kwenye Msitu wa Hifadhi ya Mazingira asili ya Kalambo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea maeneo ya hifadhi za misitu na mashamba ya miti ya serikali.

Amesema uamuzi wa serikali kuupandisha hadhi msitu wa Kalambo kuwa msitu wa hifadhi ya mazingira asili ni jitihada za kuhakikisha maporomoko ya mto huo yanahifadhiwa na kusimamiwa ipasavyo.

Brigedia Jenerali Mkeremy amesema ni wakati sasa kwa watanzania kuanza kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi hiyo ili kujionea maajabu ya maporomoko hayo.

Amesema , “Eneo hili linavutia na zuri kwa utalii, nitowe wito kwa Watanzania wakiwa katika siku za mapumziko na sikukuu kutembelea na kushuhudia maajabu ya maporomoko haya ambayo yameshatangazwa na Shirika la Umoja wa Matifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (Unesco) kuwa ni urithi wa dunia.” 

“Niwapongeze TFS kwa ujenzi wa ngazi zenye urefu wa mita 1,277 zinazoshuka hadi kwenye maporomoko haya yanayomwaga maji ziwa Tanganyika. Nimeambiwa kuwa katika ngazi za kushuka chini kwenye maji kuna “view point” tatu, ya kwanza unapotoka kwenye maji imepewa jina la Mheshimiwa waziri wa Maliasili na Utalii “Kigwangala view point” napendekeza katika “view point” ya pili ambayo ni ya kwanza unapoteremka ngazi iitwe Dos Santos View point na ya tatu inayofuatia iitwe, “Mkeremy view point,” amesema 

Kwa upande wake Kamishna Mhifadhi wa Misitu Profesa Dos Santos Silayo amesema TFS imeweka mikakati kadhaa katika kuhakikisha misitu yake inaingiza mapato ya kutosha kupitia huduma za utalii sambamba na kuuza mazao ya misitu.

Profesa Silayo amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuvitangaza vivutio vya utalii ekolojia vilivyopo kwenye misitu ya mazingira asilia iliyo chini ya taasisi hiyo.

“Utalii ekolojia na biashara ya mazao ya misitu na nyuki ni nguzo ya utendaji kazi wa taasisi yetu, tunafanya kila liwezekanalo kuimarisha maeneo ya Maporomoko ya Kalambo ili yaweze kutusaidia kuongeza tija katika jukumu letu la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuongeza mauzo ya nje na fedha za kigeni kupitia huduma za utalii na uuzaji wa mazao ya nyuki,” amesema Profesa Silayo

Aidha, Profesa Silayo amewashukuru wananchi wa kata ya Mpimbwe kwa kukubali kutoa sehemu ya ardhi yao kwa ajili ya mlima ya Mpimbe ili iwe kiunganishi (corridor) kati ya msitu wa Maporomoko ya Mto Kalambo na Msitu wa Hifadhi wa Kalambo, ambayo sasa umeunganishwa na kuwa Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asili.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: