Serikali ya mpito nchini Bolivia imesitisha uchaguzi wa Urais uliokuwa ufanyike Mei 03, 2020 na kuagiza siku 14 kuanzia sasa za taifa hilo kujiweka karantini ikiwa ni njia ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya COVID19 vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa Corona.

Mamlaka ya uchaguzi nchini Bolivia imesema kuwa uchaguzi huo wa Urais umesitishwa kwa sasa ili kutoa fursa ya siku 14 kwa taifa hilo kujiweka karantini, lakini hata hivyo haijaelezwa hasa uchaguzi huo utafanyika lini tena.

Mamlaka hiyo ya uchaguzi imeeleza kuwa itajadiliana na vyama vyote vya kisiasa pamoja na makundi mbalimbali ili kupanga hasa tarehe mpya ambayo uchaguzi huo utaitishwa.

Rais wa mpito nchini Bolivia, Jeanine Anez mapema jana Machi 21, 2020 aliwaarifu waandishi wa habari kuwa taifa hilo litajiweka karantini kuanzia leo Machi 22, 2020 mpaka ifikapo Aprili 04, 2020 ikiwa ni hatua yake muhimu ya kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa wa Corona.

Bolivia tayari imeshasitisha safari zake za ndege kwenda mataifa mbalimbali yaliyoathirika na Corona. Lakini vilevile imeshafunga mipaka yake kwa wageni wanaotaka kuingia nchini humo kutoka katika nchi zenye athari ya Corona.

Pamoja na hatua hiyo, Rais Anez ameagiza maduka ya bidhaa na chakula, hospitali, mabenki na maduka ya dawa kuendelea na shughuli zake kama kawaida wakati taifa hili likiwa karantini kwa siku 14.

Anez pia ameeleza kuwa serikali yake itazilipia gharama ya huduma familia za watu wenye uhitaji nchini humo ikiwemo watoto wadogo kuanzia mwezi Aprili, 2020.

Bolivia imesharipoti visa 19 vya watu waliobainika kuwa na virusi vya COVID19 mpaka sasa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: