Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza mbele ya viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) nchini. 
Mwenyekiti wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula akieleza mbele ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu namna watakavyohakikisha vifaa kinga vinavyohitajika vinasambazwa kila mkoa na wilaya nchini ili kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Corona.


Na WAMJW-DSM


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu leo amekutana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) nchini.


Katika kikao hicho, Waziri Ummy Mwalimu ameshukuru baraza hilo kwa kushirikiana na Sekta ya afya katika mapambano ya ugonjwa huo.

”Mchango wa sekta binafsi mkiwamo nyie wafanyabiashara ni muhimu kwani mtaleta manufaa makubwa katika mapambano haya,” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TPSF, Bi. Angelina Ngalula amesema watahakikisha vifaa kinga vinavyohitajika vinasambazwa kila mkoa na wilaya nchini ili kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Corona.

Katika kuhakikisha kwamba sekta hiyo inakabiliana na maambukizi ya homa ya Corona, TPSF imekubaliana na wamiliki nchini kuwapatia madereva na wasaidizi wao vifaa kinga.

“Sisi kama sekta binafsi tutahakikisha kwamba tunalinda ajira za watumishi wetu kwa gharama zote,” amesema Bi. Ngalula.

Naye Mwenyekiti Kamati ya TPSF Inayosimamia Jitihada za Kukabiliana na Maambukizi ya Homa ya Corona, Bw. Abdulsamad Abdulrahim amesema sekta binafsi imebainisha maeneo 26 katika Mkoa wa Dar es Salaam ambayo ni hatarishi kwa maambukizi ya homa ya Corona na kwamba vijana waelekea mikoani kwa ajili ya kubaini maeneo mengine.

Bw. Abdulrahim amesema katika upande wa elimu ya afya nyakati za dharura na majanga, wamewasiliana na kampuni za simu na kwamba tayari zimeanza kusambaza ujumbe kuhusu elimu ya kijikinga na maambukizi ya homa ya Corona.

“Tumewatafuta wadau wanaomiliki mabango barabarani nchi nzima na wameweka ujumbe wa kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huu. Mheshimiwa Waziri hivi tunavyozungumza, tayari jumbe mbalimbali zimeshawekwa kwenye mabango ya barabarani,” amesema Bw. Abdulrahim.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: