Na Mwandishi Wetu

Katika moja ya nukuu zake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kupata taarifa Bwana Guterres amewahi kukaririwa akisema “hakuna demokrasia iliyo kamilifu bila kupata taarifa kwa uwazi na za kuaminika.
Ni msingi wa kujenga taasisi za haki za zisizo na upendeleo, na ku wawajibisha viongozi na kila wakati kueleza mamlaka ukweli.”

Wakati dunia ikiendelea kuiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, haki ya raia kupata taarifa sahihi, zinazoelimisha na kuburudisha umekuwa ndio wajibu muhimu wa vyombo vya habari katika jamii yoyote.

Kuimarika kwa teknolojia ya mawasiliano na kuongezeka kwa matumizi yake hususani mitandao ya kijamii sio tu imepanua wigo wa utoaji na upatikanaji wa taarifa miongoni mwetu lakini pia imeleta changamoto kwa vyombo rasmi vya habari, magazeti, runinga, redio katika mchakato mzima wa kuwasilisha taarifa na habari.

Moja ya changamoto kubwa ni weledi wa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na namna bora kwa Vyombo vya Habari katika kuhabarisha hadhira kwa taarifa zilizohakikiwa kwa umakini. Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaweza kuwa na usuli na motisha tofauti na Wanahabari wa Kitaaluma. Ingawa mbinu za kuwasilisha taarifa za mitandaoni zinaweza kufanana na zile za kitaaluma bado kuna changamoto kubwa ya uzingatiaji wa maadili ya utoaji wa taarifa kwa walengwa pasipo upotoshaji.

Hata hivyo, uharaka na wepesi wa kuenea kwa taarifa kutoka kwenye chanzo rasmi na kisicho rasmi na kuifikia hadhira papo kwa papo imeongeza shinikizo kwa watumiaji wa mitandao na kupelekea kusambaa kwa taarifa za uongo, zilizokuzwa zenye lengo la kupotosha. Tabia hii inakinzana na dhana nzima ya uhuru wa kutoa na kupata taarifa.

Udhibiti wa usambazaji wa taarifa za upotoshaji katika mitandao ya kijamii umesababisha madhara tofauti kwa watumiaji wake ikiwemo kifungo gerezani, unyanyapaa, ugomvi baina ya wahusika. Katika kuonesha ukubwa wa tatizo hili kampuni kubwa za mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na Google mara kadhaa zimelaumiwa kwa kushindwa kuweka mifumo kamili ya usalama ikiwa ni pamoja na kudhibiti vyanzo bandia vya taarifa zinazoendesha shughuli za kusambaza taarifa potofu.

Katika ngazi ya nchi changamoto kubwa ipo katika kuweka mfumo madhubuti utakaohakikisha matumizi sahihi ya mitandao hii itakayodhibiti upashanaji wa taarifa zisizofaa bila kuathiri haki za raia kutoa na kupata taarifa. Mfano, utungwaji na utekelezaji wa sheria mbalimbali za matumizi ya mitandao kama Sheria ya Uhalifu wa Mtandao ya mwaka 2015 mbali ya kuwalinda raia dhidi ya uhalifu, matusi na unyanyasaji bado unaathiri haki na uhuru wa raia katika kupata taarifa.

Mbali na changamoto tajwa hapo juu bado kuna tatizo la wananchi walio wengi wakiwemo wanahabari wa vyombo vya Habari kutokuwa na Elimu ya kutosha ya namna ya kutumia mitandao ya kijamii kupata na kusambaza taarifa za kimaendeleo. Pamoja na ukweli kwamba mitandao hii imewawezesha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kujieleza bado wanahitaji kufahamu kwamba hawapaswi kuingilia haki ya watu wengine. Hivyo, ipo haja ya kuimarisha yafuatayo:-

·Kufanya mapitio na kuboresha sheria na kanuni zinazosimamia utoaji na upatikanaji wa taarifa kwa njia ya mitandao kwa ushirikishaji wa wadau wote ili zifanye kazi kwa matakwa ya walio wengi.

·Umakini na uhakika wa vyanzo vya taarifa au habari zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii. Vyombo vya Habari na wananchi wajiridhishe pasipo shaka kuhusu ukweli wa taarifa (ikiwemo kupitia vyanzo mbalimbali) kabla ya kuisambaza mtandaoni.

Mwisho, rai yangu kwa waandishi wa habari na wote wenye jukumu la kuandaa maudhui mtandaoni kuzingatia ulinganifu wa pande zote za taarifa husika, kuacha kushabikia jambo katika taarifa, kujikita katika uhalisia wa tukio linalotolewa taarifa na kupunguza maumivu ya kisaikolojia au ya aina yoyote kwa wanaohusika au kuitumia taarifa husika. Ni vyema na wajibu wa kila mtumiaji wa mitandao kujielimisha  kila wakati ili kuitekeleza haki ya kutoa maoni na kupata taarifa kwa kuzingatia wajibu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: