Mwenyekiti wa mnada wa Miti ya Misaji kutoka Idara ya Misitu ya Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Cellina Mongo (katikati) akimsisitizia jambo Afisa Mhakiki Mali Tanga (aliyesimama) huku Katibu wa mnada huo Kaimu meneja shamba la miti Longuza, Elinema Mwasalanga akifuatilia kwa karibu.
wadau wakifuatilia mnada.
 Sekretarieti ya mnada ikifanya upembuzi yakinifu wa maombi ya kampuni mbalimbali yaliyowasilisha zabuni za za kununua vitalu vya misaji.
Naibu Kamishna Mhifadhi wa Misitu anayesimamia Mipango na Matumizi ya Misitu TFS, Mohamed Kilongo akiwahakikishia washiriki wa mnada huo uwepo wa malighafi za kutosha za mazao ya Misitu na kuwataka wafanye uwekezaji pasipo kuwa na shaka kwenye tekolojia ya viwanda vya misitu.

Na Tulizo Kilaga, Muheza - Tanga.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - TFS leo Julai 01, 2020 umefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi milioni 900 kupitia mauzo ya miti ya misaji (teak) iliyouzwa kwa njia ya mnada katika shamba la miti Longuza lililopo Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga. 

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mnada huo, Naibu Kamishna Mhifadhi wa Misitu anayesimamia Mipango na Matumizi ya Misitu TFS, Mohamed Kilongo amesema licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za biashara zilizosababishwa na Covid 19 TFS imefanikiwa kuuza vitalu vya miti vitano kati ya 10 vilivyokuwa vinauzwa.

“Wafanyabishara wengi wa misaji wanategemea soko la nje ya nchi ambapo nchi nyingi bado zinaendelea na lockdown hali inayosababisha soko la misaji kuyumba, tutafanya tena mnada baada ya mwezi mmoja katika shamba la miti Mtibwa na Longuza katika kuhakikisha viwanda vya ndani vya misitu vinapata malighafi yakutosha,” alisema Kilongo.

Kilongo alitoa wito kwa taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na ujenzi kushiriki katika minada inayoendelea kutokana na mbao za misaji kuwa na sifa sawa na mbao za mninga na mkongo.

“Mbao za mninga na mkongo zinatoweka na hii ina maana kuwa lazima tutafute mbadala wa miti hio ambapo miti ya misaji ndio kimbilio pekee baada ya kuthibitika kuwa na sifa zinazofanana miti ya mninga na mkongo.

“Tayari tumeanza vikao na mamlaka mbalimbali za serikali na kukutana na wadau wa sekta ya ujenzi kuangalia jinsi tunavyoweza kuwa na utaratibu mzuri wa taasisi za umma kupata malighafi hizi, lakini pia tunataka mikataba wanayopewa wakandarasi itambue mbao za misaji kama mbadala wa mbao za mkongo na mninga,” alisema Kilongo.

Amesema kwa taasisi za umma hazitalazimika kushiriki kwenye mnada na badaa yake zinaweza kuchagua njia mojawapo kati ya tatu za uuzaji miti ya misaji zinatumika ikiwemo utumaji maombi yaani mnunuzi, kushiriki katika mnada wa misaji au kutumia njia ya mazungumzo na TFS.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mnada huo wa miti ya misaji Dkt. Cellina Mongo amesema kumekuwepo na maombi ya wafanyabiashara kutaka kupunguziwa bei ya miti ya misaji ili waweze kununua kwa wingi miti ya misaji lakini sheria na kanuni haziruhusu jambo hilo.

“Mnada huu unaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya misitu sura 323, kanuni za misitu za mwaka 2004 na tangazo la serikali namba 255/2017 ambapo sharia inaelekeza namna ya uuzwaji wa miti hii ya misaji na kututaka tuzingatia hali ya bei ya soko iliyopo jambo ambalo tunalifanya,” alisema Dkt. Mongo.

Yusuff Ngage wa Kampuni ya Prime Timber iliyoshiriki mnada huo aliipongeza TFS kwa kuendelea kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda hali iliyochangia kuanzishwa na kuimarika kwa viwanda mbalimbali vya mazao ya misitu nchini. 

“Nisiwe mchoyo wa fadhila, TFS mnafanya kazi nzuri mana hivi sasa viwanda vingi vinapasua magogo na kutumia malighafi kutoka katika mashamba ya miti ya Serikali kutokana na uhakika wa ubora na uwazi wa upatikanaji wake hali inayochochea kukua kwa viwanda vya ndani na kuongeza ajira,” anasema Ngage.

Mnada huo ulihudhuriwa na kamapuni mbalimbali za usafirishaji mazao ya misitu, taasisi za serikali zilizokuja kujifunza namna ya uendeshaji wa minada ya aina hiyo, viongozi waandamizi wa Idara ya Misitu ya Wizara ya Maliasili na Utalii TFS na Mhakiki mali wa Serikali.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: