Na Rubaba Protas.

Mwaka 2008 nilifanya safari ya kwanza kwenda kwenye mji ambao nilitamani kufika toka nikiwa na umri mdogo kabisa kutokana na historia yake niliyokuwa nikiisikia hasa wakati wa harakati za ukombozi. Mungu ni mwema sana kwakuwa nilifanikiwa kufanya safari ya kwenda CAPE TOWN nikitokea mji mwingine nchini Afrika ya Kusini wa PORT ELIZABETH.

Majira ya saa kumi jioni niliwasili kwenye kituo cha mabasi maarufu sana ya GREYHOUND, mabasi yenye ubora wa hali ya juu kabisa na yenye huduma bora. Kwa hapa nchini kwetu tungeweza kuyafananisha na kampuni iliyowahi kushinda tuzo nyingi duniani, hasa kutoka kwenye nchi za scandnavia, kampuni ambayo ilijulikana kwa jina la SCANDNAVIAN EXPRESS.

Majira ya saa kumi na mbili na nusu tulianza safari kuelekea Cape Town. Nilikaa pamoja na kijana ambaye sikumfahamu kwakuwa hatukufanya utambulisho kabla zaidi ya salamu. Kwa muda wa saa mbili hakuna aliyemsemesha mwingine lakini kwakuwa mimi nilikuwa mgeni nikahisi nitakuwa najikosesha ufahamu wa mambo mengi kama sitofanya mazungumzo na aliyekaa pembeni yangu. Nilimuuliza jina lake na kama ni raia wa Afrika ya kusini au mgeni.

Kijana yule alikuwa ni raia wa Afrika ya kusini hata kwa rafudhi. Kingereza chake kilisikika sawa na kile cha waKhosa. Swali la mwisho kumuuliza katika orodha ya maswali yangu lilikuwa ni kutaka kujua ni sehemu gani tupo kwa muda ule na tutatumia muda gani kufika Cape Town. Tayari kwa mimi kumuuliza maswali mengi tulijenga uhusiano na wote tukawa na uhuru wa kuulizana swali lolote.

Msingi wa pongezi zangu kwa Rais pamoja na kampuni ya ATCL ni kutokana na maswali aliyoanza kuniuliza yule kijana tuliyesafiri nae. Alianza kwa kuniuliza jina na nikamwambia naitwa RUBABA. 
Nilipasika kurudia jina langu kama mara tatu hivi kwasababu kila nikimtajia alikuwa hawezi kulishika. Baada ya swali lililotaka kujua jina, aliniuliza ni sehemu gani ya dunia ninatoka. Hapa ndio nilipata hasira na kuumia sana.

Nilimwambia yule kijana ya kwamba mimi ni raia wa Tanzania. Kijana yule aliyekuwa anasoma master degree alikuwa akinikodolea macho tu kila nilipomtajia Tanzania. Mara moja nikagudua nimeingiza msamiati mgeni kwenye kichwa chake na anaona aibu kusema hajui Tanzania ni kitu gani. Niliamua kumuuliza kama anafahamu Tanzania inapopatikana kwenye ramani ya Afrika. Alikiri kwamba hafahamu. Niliamua kumuuliza kama anafahamu nchi nyingine tofauti iliyopo afrika mashariki, akajibu hana uhakika kama anafahamu na kuniuliza kama iko karibu na Kenya?

Nafsi yangu ilinizuia kabisa kujibu swali aliloniuliza na badala yake mimi nikamuuliza swali lingine. Unaufahamu mlima KILIMANJARO? Alijibu ndio anaufahamu jambo ambalo mimi binafsi halikunishangaza kwasababu taarifa za mlima Kilimanjaro nimewahi kuziona mara nyingi kwenye vyombo vya habari vya Afrika ya Kusini. 

Nikamuuliza unafahamu mlima huo uko kwenye nchi gani? Bila hata kusita aliniambia mlima huo unapatikana nchini Kenya. Mshangao nilioupata ulimfanya kijana yule kuhisi kuna jambo amekosea. Nilidhani taarifa ya kwamba jirani zetu waKenya hutoa matangaza huko duniani wakiwaalika watalii kwenda Kenya kuuona mlima Kilimanjaro ni za uongo. Katika safari yangu ya Cape Town nilipata Ushuhuda.

Kwa muda nilijigeuza mfanyakazi wa Wizara ya Maliasili na Utalii au pengine mmoja wa watumishi wa bodi ya utalii. Nilianza kumueleza yule kijana Sehemu ambapo Tanzania inapatikana nikihusianisha na Mlima Kilimanjaro na kwanini waKenya wanasema mlima upo nchini mwao. Nilijaribu pia kuongelea nafasi ya Tanzania katika ukombozi wa nchi yao, maelezo ambayo kwa hakika yalikuwa magumu na hayakueleweka kirahisi. Mwisho kabisa nilimwambia mlima Kilimanjaro uko Tanzania na kama atakuwa na nafasi aje Tanzania ili nimpeleke akauone.

HONGERA SANA RAIS MAGUFULI KWA KUFUFUA SHIRIKA LA NDEGE LA TANZANIA (ATCL) NA KULIPATIA NDEGE ZENYE UWEZO WA KWENDA NCHI MBALIMBALI DUNIANI KOTE. HONGERA ATCL KWA KUANZISHA SAFARI KWENDA ZAMBIA NA ZIMBABWE.

Nembo ya shirika la ndege la Tanzania husomeka namna hii; AIR TANZANIA, The wings of Kilimanjaro. Na nembo hii, bila kumsahau twiga wetu ziko kwenye ndege zetu zote na huonekana mahala popote ambapo ndege hizi zinaruka. Na kila mtu atakaemuona twinga ataona pia neno Tanzania na Kilimanjaro. Kwa waliosoma advertising watakubaliana nami kabisa ya kuwa kila ambako ndege hizi zitakwenda, jina la Tanzania na mlima Kilimanjaro vitakuwa vikipata matangazo ya bure kabisa.

Ninatamani sana Dkt. Magufuli angekuwa Rais na kununua ndege zote hizi kabla sijafanya safari yangu ya kutoka Port Elizabeth kwenda Cape Town na kukutana na huyu kijana. 

Natamani sana pia kwamba huyu kijana angekutana na ndege za ATCL na kumuona Twiga na nembo yetu inayoihusianisha Tanzania na Mlima Kilimanjaro – Air Tanzania, The wings of Kilimanjaro. Hakika mtu niliyekutana nae kwenye safari yangu asingekuwa na maswali yenye utata. 

Ingenirahisishia sana utambulisho wa nchi yangu Tanzania kwa huyu kijana nje ya nchi

Ni Dhahiri kabisa ya kuwa ndege za ATCL sio tu zitasaidia kukuza uchumi wa Tanzania na kuleta watalii wengi lakini pia zitakuwa na msaada mkubwa sana wa kuitambulisha nchi sehemu zote itakazoruka. Natamani sana ATCL mngerusha lile dege la ajabu lenye uwezo wa kugusa ardhi na kupaa wakati huo hu kwenda Lusaka na Harare badala ya Aibus. Natamani sana mngerusha dreanliner, ndege ya kisasa kabisa naya pekee kwa ukanda huu ili hata raia wa nchi hiyo washangae zaidi na kutambua mapinduzi yaliyofanywa na RAIS MAGUFULI nchini TANZANIA.

Hongereni sana watanzania kwa kununua ndege kutokana na kodi mnazolipa, hongera sana Dkt. Magufuli kwa kuleta mageuzi ya shirika la ndege nchini, na hongereni sana viongozi wa shirika la ndege la Tanzania kwa kuanzisha safari za Zambia na Zimbabwe.

Mungu Ibariki Tanzania.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: