Articles by "AFYA"
Showing posts with label AFYA. Show all posts
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiongoza Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Wadau mbalimbali za Wadau wa Mkutano kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Amir Mruma akitoa neno la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa taarifa ya utekelezaji wa mikakati kwa upande wa Mahakama ya Tanzania wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe akichangia jambo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma.

Mahakama ya Tanzania pamoja na Wadau wa Sekta ya Sheria na Uchumi wamekutana kufanya Tathmini ya Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara lengo likiwa ni kuboresha ufanisi katika mnyororo wa haki za kiuchumi sambamba na kuoanisha utendaji kazi na Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

Akifungua Mkutano wa Nne wa Wadau kuhusu Tathmini na Utekelezaji wa Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi, Uwekezaji na Ushindani wa Kibiashara tarehe 16 Septemba, 2026 kwenye ukumbi wa mikutano- Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewasisitiza wajumbe wa Mkutano huo kuwa huru kutoa maoni na changamoto zilizopo zikiwemo zinazoigusa Mahakama ili kuboresha uwazi na uwajibikaji katika utoaji haki nchini.

“Mkutano huu una mambo mazuri tu yanayotusaidia kuboresha ufanisi katika maeneo yetu ya kazi kwa jinsi yanavyohusiana na kuuwiana na mnyororo wa haki jinai, haki inaweza kuwa ni haki jinai au katika muktadha wa kikao hiki cha mashauri ya kiuchumi. Kwahiyo nawashauri kwamba muwe huru kabisa mnavyoshiriki mkutano huu. Wengi wenu nawafahamu ninyi tu si kwamba ni viongozi lakini ni wataalamu mahiri katika maeneo yenu, hivyo tunategemea kupata ushirikiano wenye tija kwa sababu ya uwepo wenu,” amesema Mhe. Masaju.

Aidha, Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, umuhimu wa kiongozi haupatikani kwa Kiongozi kuwa ofisini pekee bali umuhimu wake unapatikana kwa huduma yake anayotoa katika jamii.

Mhe. Masaju amesema, nafasi na mchango wa Mahakama na Wadau katika utekelezaji wa majukumu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni muhimu.

“Msingi Mkuu wa Dira hii ni Taifa Jumuishi lenye Ustawi, Haki na Linalojitegemea.Kwahiyo tunavyokaa hapa sasa pamoja na Mikakati hii tuliyokwishajiwekea tuweke au tupendekeze mikakati ya kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba na kisheria katika muktadha wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo inamhususu kila mmoja wetu hapa. Kwa hiyo hiki kikiwa ni kikao cha tatu tunakutana ili kutathmini utekelezaji wa mikakati ya pamoja ya kushughulikia mashauri ya kodi, biashara, ardhi, mabenki na ushindani wa kibiashara,” ameeleza Jaji Mkuu.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutathmini utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea, Mkutano huo pia ni fursa ya kujadili masuala mengine yanayoweza kujitokeza baada ya kikao kilichopita na yale yanayoweza kujitokeza siku za mbeleni ambayo yanaweza kuathiri utekelezaji wa mikakati iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu ya Mahakama na Wadau.

“Mnapokuwa mmerejea katika Ofisi zenu muende mkayatekeleze haya lakini pia muwashauri viongozi wenu umuhimu wa kuyatekeleza hayo,” amesisitiza Mhe. Masaju huku akigusia juu ya umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi akirejea Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mahakama inahimizwa kukuza usuluhishi na kuzikumbusha Taasisi nyingine kuwa, zinapaswa kwanza kutatua migogoro kabla ya kufikisha mashauri mahakamani.

“Naomba niwarejeshe katika mkakati wa sita na wa kumi katika mikakati yetu inayohusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. Lakini pia kwa njia za kiutawala katika maeneo yetu ya kazi. Na hili sharti ni sharti la kikatiba linatokana na ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo Mahakama inapotekeleza jukumu lake la kutoa maamuzi katika mashauri ya madai na jinai inatakiwa pia kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya watu wanaohusika katika migogoro,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekitaka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kupitia Mawakili wake kuwasimamia wateja wao kwa maadili na kuwashauri kutumia mifumo ya usuluhishi na mamlaka za udhibiti badala ya kukimbilia mahakamani. Hatua hiyo inalenga kuepuka gharama zisizo za lazima na mapingamizi ya kisheria (preliminary objections) lakini vilevile ni utekelezaji wa Kanuni ya 59 ya Kanuni za Maadili ya Mawakili, 2018 Tangazo la Serikali Na. 118 la 2018 inayoelekeza Mawakili kuwataarifu Wateja wao kuhusu uwezekano na faida za kumaliza mashauri kwa mfumo wa usuluhishi

Akizungumzia kuhusu Uhuru wa Mahakama na Usimamizi wa Sheria; Mhe. Masaju amesema, kwa mujibu wa Ibara ya 107B ya Katiba, Mahakama itaendelea kuwa huru na kusimamia sheria huku akibainisha kuwa, mashauri ambayo hayakufuata taratibu za awali za kupatiwa ufumbuzi kwanza katika mamlaka husika kabla ya kuzihusisha Mahakama yatarejeshwa kwenye mamlaka husika.

“Na sisi huku mahakamani tutaendelea kusimamia sheria kwa ufanisi ipasavyo. Kwa sababu hata hivyo ni sharti letu la jukumu letu la kikatiba katika ibara ya 107B kwamba katika kutekeleza majukumu yetu Mahakama itakuwa huru isipokuwa itazingatia tu masharti ya Katiba na Sheria za Nchi,” ameeleza Jaji Mkuu.

Kupitia mkutano huo, Mahakama na Wadau hao wataendelea kubainisha changamoto zilizosababisha ucheleweshaji au zinazosababisha ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri ya kiuchumi na kuendelea kutekeleza ipasavyo mikakati iliyowekwa na mingine itakayokubalika katika Mkutano huo.

Mkutano huo umehudhuriwa na Amidi wa Mahakama Kuu na Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Amir Mruma, Majaji Wafawidhi kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Joachim Tiganga, Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Dkt. John Antony Jingu, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na baadhi ya Naibu Wasajili kutoka Mahakama Kuu Masjala Kuu, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi na Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara.

Wadau wengine waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe na wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Fedha, Tume ya Taifa ya Mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA), Msajili wa Baraza la Ushindani.

Wengine ni kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Umoja wa Mabenki (TBA), Chama cha Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama, Baraza la Ushindani, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).




















Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando (kushoto) akimkabidhi zawadi ya ukumbusho Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Breweries Limited (TBL) Bi. Michelle Kilpin (kulia) mara baada ya hafla ya kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) kati ya kampuni hizo mbili, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2026. Kupitia ushirikiano huo, zaidi ya wafanyabiashara 26,000 wa TBL nchini watanufaika na mafunzo ya biashara pamoja na suluhisho za kidijitali za Vodacom kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (Retailer Development Programme).

●Ushirikiano huu wa kimkakati utawawezesha wafanyabiashara wa TBL kupata suluhisho za kidijitali za Vodacom unatarajiwa kuzinduliwa rasmi jijini Mwanza Septemba 16.

Dar es Salaam, Septemba 11, 2026: Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na Vodacom Tanzania PLC leo zimeingia makubaliano ya ushirikiano (MoU) ya muda wa miaka miwili, yenye lengo la kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara nchini kupitia Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja (Retailer Development Programme), uliobuniwa mahususi ili kuwapatia ujuzi wa vitendo katika usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya teknolojia vitakavyopelekea kukuza biashara zao.

Ukiendeshwa chini ya kaulimbiu ya ‘Growing Innovatively Together’ (GRIT), mpango huu unadhihirisha azma ya pamoja ya taasisi zote mbili za kuwasaidia wafanyabiashara wanaoshiriki kwa kiwango kikubwa katika mnyororo wa thamani wa TBL pamoja na mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria na Uhusiano wa Kampuni wa TBL Neema Temba, alisema ushirikiano huu unaonesha umuhimu wa kushirikiana katika kuimarisha uwezo wa wafanyabiashara na kuwawezesha kukua kwa muda mrefu.

"Kwa TBL, wafanyabiashara ni nguzo muhimu ya biashara na ukuaji wa uchumi. Kupitia ushirikiano na Vodacom Tanzania, tunawekeza katika ujuzi, teknolojia na uendelevu wa biashara ili kuwawezesha kukuza shughuli zao na kunufaika na fursa mpya. Hivyo tunajenga thamani inayonufaisha biashara, familia na jamii kote nchini,” alisema Bi Temba.


Ushirikiano huu utaunganisha mtandao mkubwa wa TBL wa zaidi ya wafanyabiashara 26,000 na uzoefu wa Vodacom katika mawasiliano, ubunifu wa kidijitali na huduma za kifedha kimtandao, kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara kuboresha ufanisi, uimara na uendelevu wa biashara zao.

Kupitia mpango huo, wafanyabiashara watapatiwa mafunzo katika maeneo mbalimbali muhimu ya uendeshaji wa biashara, ikiwemo usimamizi wa biashara na fedha, mtiririko wa fedha, usimamizi wa bidhaa, mauzo na masoko, huduma kwa wateja, ujasiriamali, biashara inayozingatia uwajibikaji pamoja na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Mbali na mafunzo, washiriki watawezeshwa kupata uelewa na matumizi ya suluhisho za kidijitali na kifedha zinazoweza kuwasaidia kuongeza ufanisi wa biashara, kuboresha faida na kuimarisha mahusiano na wateja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya Vodacom ya kutumia teknolojia na ubunifu kusaidia wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa biashara nchini.

"Biashara ndogo ni muhimili wa uchumi wa Tanzania. Kupitia ushirikiano wa TBL na Vodacom Tanzania, wafanyabiashara wanapatiwa zana, maarifa na teknolojia za kuboresha biashara, kuongeza tija na kufungua fursa za ukuaji endelevu. Kwa pamoja, tunachochea ujumuishaji wa kidijitali na kifedha, na kuwawezesha kustawi katika uchumi unaoongozwa na teknolojia,” alisema Bw Nguvu.

Katika utekelezaji wa mpango huo, Vodacom itawapatia wafanyabiashara fursa ya kufahamu na kutumia suluhisho mbalimbali za biashara na huduma za kidijitali, ikiwemo SME Bomba, M-Wekeza, Lipa kwa M-Pesa na M-Koba, zinazolenga kusaidia ujumuishaji wa huduma za kifedha, ufanisi wa biashara na matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku.

Kadhalika, ushirikiano huu utakuza ubunifu, ujasiriamali na uwajibikaji katika biashara kupitia mafunzo ya ana kwa ana na majukwaa ya kidijitali. TBL na Vodacom Tanzania pia zitashirikiana katika mawasiliano, ushirikishwaji wa wadau, ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha matokeo yanayopimika na yenye manufaa ya muda mrefu. Mafunzo ya kwanza chini ya Mpango wa Maendeleo ya Wafanyabiashara wa Rejareja yatafanyika Mwanza Septemba 16, yakiwapa wafanyabiashara ujuzi wa usimamizi wa biashara, fedha na matumizi ya teknolojia kwa ajili ya kuboresha utendaji na ukuaji endelevu. 

Kupitia ushirikiano huu, TBL na Vodacom zinaendelea kuimarisha ujasiriamali, matumizi ya huduma za kidijitali na kuwawezesha wafanyabiashara kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Na Mwandishi wetu- Kibaha, Pwani.

Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kupitia idara ya afya imetoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kufanya tathmini ya magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kukabiliana nao.

Mafunzo hayo yametolewa na Wizara ya Afya kupitia taasisi ya TANCDA inayojihusisha na utoaji wa elimu kwa umma juu ya magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kupambana nayo ikiwemo kubadilisha mtindo wa maisha.

Mratibu kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Dkt Grace Gembe amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa kwa kasi sana ni muhimu sana wananchi waweze kupata uelewa na elimu ili kujilinda.
Gembe amesema, anaamini mafunzo haya yatakuwa na tija kwa wahudumu hawa wa ngazi ya jamii ambapo watakaporudi kwenye mitaa yao watakuwa walimu wazuri kwenye kuelemisha jamii.

Kwa upande wa Mganga Mkuu Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt Catherine Saguti amesema kwa siku ya leo wametoa mafunzo kwa vijana 40 ila wanajumla ya vijana 135 katika mitaa yote 73 ya Manispaa ya Kibaha.
Amesema, vijana hao wote watapata mafunzo ya namna ya kutoa elimu kwa jamii juu ya magonjwa yasiyo yakuambukiza katoka ngazi ya jamii na namna ya kukabiliana nayo.

Baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, vijana hao wamepatiwa kitabu kinachoelezea magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza na namna ya kujitambua pindi unapokuwa na dalili zilizoanishwa humo.


Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Kauthar D’souza akizungumza wakati wa zoezi la uchangiaji wa Damu kitaifa linaloratibiwa na Benki ya Exim Tanzania kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Damu Salama. Zoezi hilo linalofanyika katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya, Tabora na Mtwara ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 11 ya ushirikiano wao unaolenga kuhamasisha na kusaidia juhudi za ukusanyaji wa damu nchini ili kupunguza au kuondoa kabisa changamoto ya upungufu wa damu katika hospitali na vituo vya afya nchini.  Uzinduzi wa zoezi hilo umefanyika tarehe 10 Juni 2026 katika Makao Makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam, ambapo wananchi wanahimizwa kujitokeza katika vituo vilivyo katika mikoa hiyo ili waweze kuchangia damu na kuokoa maisha ya wagonjwa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Benki ya Exim Tanzania imeendesha zoezi la kitaifa la uchangiaji damu wa hiari kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Mpango wa Damu Salama (NBTS), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 11 ya ushirikiano wao unaolenga kuimarisha upatikanaji wa damu salama nchini.

Zoezi hilo lililofanyika Juni 10, 2026, limefanyika katika mikoa sita ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya, Tabora na Mtwara. Lengo lake ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kuchangia damu ili kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa damu katika hospitali na vituo vya afya nchini.

Kwa zaidi ya miaka kumi, Benki ya Exim Tanzania na NBTS wamekuwa wakishirikiana kuhamasisha utamaduni wa uchangiaji damu wa hiari. Kupitia kampeni hizo, zaidi ya chupa 800 za damu hukusanywa kila mwaka, hatua inayosaidia kuokoa maisha ya kina mama wanaopata changamoto wakati wa kujifungua, waathirika wa ajali, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, watoto na wengine wanaohitaji kuongezewa damu kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika makao makuu ya Benki ya Exim jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Kauthar D'souza, alisema mpango huo unaonesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuunga mkono vipaumbele vya afya vya taifa.

"Benki ya Exim tunaamini jukumu letu haliishii katika utoaji wa huduma za kifedha pekee, bali pia kuwa mshirika wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Kupitia programu yetu ya Exim Cares, tunaendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, ubunifu, uhifadhi wa mazingira na uwezeshaji wa jamii ili kuleta mabadiliko chanya na endelevu," alisema Kauthar.

Aliwahimiza Watanzania wenye sifa za kuchangia damu kujitokeza kushiriki katika kampeni hiyo, akieleza kuwa dakika chache za mtu kutoa damu zinaweza kuokoa maisha ya wengine. "Mchango wako unaweza kuwa sababu ya mama kurudi salama kwa familia yake, mtoto kupata matibabu anayohitaji au mgonjwa kupewa nafasi nyingine ya kuendelea kuishi," aliongeza.

Kwa upande wake, Afisa Uhamasishaji wa Damu Salama Kanda ya Mashariki kutoka NBTS, Evelyn Dielly, aliipongeza Benki ya Exim kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kuimarisha juhudi za ukusanyaji damu nchini.

"Tunathamini mchango wa Exim Bank katika kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa uchangiaji damu wa hiari na kuboresha upatikanaji wa damu kwa wagonjwa kote nchini. Kila chupa ya damu inayokusanywa husaidia kuokoa maisha na kusaidia vituo vya afya kukabiliana na mahitaji ya dharura ya kitabibu," alisema Evelyn.

Kampeni hiyo ya kila mwaka, ambayo sasa imefikisha miaka 11, inaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wenye tija kati ya sekta binafsi na taasisi za umma katika kuimarisha huduma za afya na kukuza utamaduni wa uchangiaji damu wa hiari nchini Tanzania.

Na Mwandishi Wetu.

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inahitaji kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya ubingwa bobezi ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu pamoja na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji mkubwa wa huduma hizo.

Mahitaji haya yametangazwa leo tarehe 21 Mei 2026 katika Ukumbi wa NIMR Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi katika mkutano wake na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri, Tanzania Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Miitandao Tanzania (JUMIKITA).

Alisema kwa sasa kuna watoto 50 wanaohitaji upondikizaji wa uloto na wengine 50 kwa ajili ya upandfikizaji wa figo.

Mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, hapo Julai 15 ,2026 ambapo safari ya maadhimisho haya ilizinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2025.
Tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo Oktoba 13,2015, Hospitali ya Benjamin Mkapa imekuwa na dhamira ya kutoa huduma za kibingwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa katika kuzuia, kuchunguza, na kutibu magonjwa mbalimbali, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya tafiti.

Kwa sasa, BMH inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya Tanzania, ikiwa na vitanda 400 na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 100.

Kwa mujibu wa Profesa Makubi Hospitali hiyo inatoa huduma 20 za kibingwa na huduma 18 za ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji wa viungo, upasuaji wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, huduma za radiolojia ya kisasa, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji wa nyonga na magoti, upasuaji wa njia ya matundu madogo, pamoja na uchujaji wa damu.

Profesa Makubdi amesema ndani ya miaka 10 ya utendaji, hospitali imepata mafanikio makubwa yaliyochangiwa na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na vifaa vya kiasi cha shilingi bilioni 283, huku idadi ya watumishi ikiongezeka kutoka 20 tu mwaka 2015 hadi kufikia 1,076 mwaka 2026.

Hospitali imefanikiwa kupanua na kuboresha huduma za matibabu ya kibobezi, ikiwemo uanzishwaji wa huduma muhimu za upandikizaji figo na uloto kwa watoto wenye selimundu, pamoja na kukuza tiba utalii kwa kuhudumia wagonjwa wa kigeni na viongozi mashuhuri, wakiwemo wagonjwa 2,897 kutoka Burundi, 526 kutoka Comoro, na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ubora wa huduma umeongezeka kupitia upasuaji wa matundu na uanzishwaji wa Kliniki ya Kifalme (Royal Clinic) mnamo tarehe 10 Julai 2025, ambayo imeshalaza na kuhudumia wagonjwa 18,607, wakiwemo wagonjwa wa kimataifa 390 waliofanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya (Master Health Check-up).

BMH pia imepata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO 15189:2022, imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, imeweka mfumo wa kisasa wa kuelekeza wagonjwa (queuing system) na kutoa maoni, na imefanikiwa kupunguza muda wa mgonjwa kusubiri huduma kutoka wastani wa saa 8 hadi saa 3 tu.

"Tunatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na hasa ndani ya BMH, na ninatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa huku sisi tukiahidi kuendelea kuishi kwa kauli mbiu yetu ya kuvaa viatu vya mgonjwa, uwajibikaji, na kujituma, " alisema Profesa Makubi.
Katika kuimarisha miradi ya kimkakati, hospitali inaendelea na ujenzi wa jengo la matibabu ya saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32, jengo la matibabu ya figo la shilingi bilioni 44.9 linalojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Japani iliyochangia bilioni 28 na Serikali ya Tanzania iliyochangia bilioni 16.9, uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha upandikizaji uloto, pamoja na chuo kinachotoa elimu ya ngazi ya Stashahada.

Akizungumzia mwelekeo Preofesa Makubdi alisema taasisi hiyo kwa miaka 10 ijayo inajipanga kubobea zaidi na kuwa kijiji cha utalii wa matibabu katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.

Kuelekea kilele cha tarehe 15 Julai 2026, matukio mbalimbali yamepangwa na mengine tayari yamefanyika ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau, ikiwemo mikutano iliyofanyika mwezi Aprili 2026 jijini Dar es Salaam na Arusha na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote za Umma, ambapo takriban shilingi bilioni 4 zimeshapatikana kutoka kwa wadau wa sekta ya umma na kampuni zenye ubia na serikali.
Aidha, Kongamano la Kisayansi lililoangazia hali ya huduma za upandikizaji viungo nchini lilifanyika tarehe 6 Mei 2026 katika Ukumbi wa Domiya Estate likishirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi, na hivi sasa maandalizi ya dhifa za chakula cha jioni (Gala dinners) pamoja na mbio maalumu za Marathon yanaendelea ili kuchangisha fedha hizo.

Zoezi hili la harambee la kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo linafanyika kwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo ambao idadi yao inaongezeka kila siku.

Harambee hiyo kubwa itakayofanyika tarehe 15 Julai 2026 jijini Dodoma, inatarajiwa kuongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Profesa makubdi ameyaomba Mashirika, taasisi, makampuni, wadau, na wananchi wote kuchangia kupitia njia rasmi zilizowekwa ambazo ni namba ya malipo (Control Number) 986930000001 au kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa akaunti namba 102501000407 zote zikiwa kwa jina la BMH Organ Transplant.





Ujumbe wa Tanzania

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassanakiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya pamoja na Ujumbe wake, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2026. 



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya pamoja na Ujumbe wake Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Mei, 2026.

Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC pamoja na ujumbe wake, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadili masuala mbalimbali kuhusu afya ya uzazi, mama na mtoto barani Afrika.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kaseya alisema Africa CDC ina dhamira ya kushirikiana na Rais Samia ambaye ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, pamoja na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, kwa lengo la kuimarisha huduma za afya katika sekta hiyo muhimu.

Alisema ushirikiano huo unalenga kuongeza juhudi za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na kuboresha huduma za afya kwa mama na watoto katika nchi mbalimbali za Afrika.

Dkt. Kaseya alieleza kuwa Tanzania imeonyesha mafanikio makubwa katika sekta ya afya, hususan katika upatikanaji wa huduma kwa wananchi, jambo ambalo linaweza kuwa mfano kwa nchi nyingine barani humo.

Alibainisha kuwa asilimia 85 ya wananchi nchini Tanzania wanapata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka maeneo wanayoishi, hatua aliyosema inaimarisha ajenda ya Afrika ya usalama wa afya na kujitegemea katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Rais Samia alisema Serikali ya Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na Africa CDC katika kuendeleza ajenda ya afya ya mama na mtoto, akisisitiza kuwa utekelezaji wa malengo yaliyowekwa unahitaji mipango madhubuti na uratibu wa karibu.

Aidha, Rais Samia aliiagiza Wizara ya Afya kushirikiana kwa karibu na Africa CDC katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuimarisha afya ya uzazi, mama na mtoto nchini na barani Afrika kwa ujumla.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inatarajia kutoa vibali vya ajira mpya katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa sekta ya afya pamoja na kada nyingine, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupunguza uhaba wa madaktari na wauguzi nchini.

 Akizungumza Mei 12, 2026 katika Kongamano la Kwanza la Kisayansi la Wauguzi lililoambatana na Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika Hotel Verde Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali itaendelea kuwekeza zaidi katika kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora na ya kisasa.

 Alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya ikiwemo ujenzi wa Hospitali Mpya ya Mnazi Mmoja pamoja na Hospitali ya Saratani Binguni, sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa na kuimarisha mafunzo kwa watumishi wa sekta hiyo.

 Rais Dkt. Mwinyi pia aliwataka wauguzi nchini kuendelea kufanya kazi kwa kujituma, huruma na kuzingatia maadili ya taaluma yao, akisisitiza kuwa wauguzi wana nafasi kubwa katika kuimarisha huduma za afya na kuokoa maisha ya wananchi.

 Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo, “Kuwawezesha Wauguzi ni Kuokoa Maisha” (Empowering Nurses, Saving Lives).

Mkuu wa Wilaya ya Geita Mh. Hashim Abdallah Komba(kulia) akikabidhiwa moja ya vifaa vya hospitali vilivyotolewa na Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania Bw. Stanley Kafu (kushoto) kwa lengo la kurudisha kwa jamii. Hafla hii imefanyika kama moja ya huduma za Benki hiyo chini ya Mpango wa Exim Cares ambapo wanatoa misaada kwa sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na mazingira. Tukio hilo limefanyika tarehe 6 May 2026, Mkoani Geita.
Na Mwandishi Wetu, Geita.

Benki ya Exim Tanzania kupitia mpango wake wa uwajibikaji kwa jamii unaojulikana kama Exim Cares, imeendelea kuonyesha dhamira ya kusaidia sekta ya afya baada ya kutoa msaada wa vifaa tiba katika Hospitali ya Manispaa ya Geita, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi na dharura kwa wananchi wa mkoa huo.

Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuwekeza katika maendeleo ya jamii kupitia sekta muhimu zikiwemo afya, elimu, mazingira, ubunifu na uwezeshaji wa kiuchumi. Kupitia mpango huo, Exim Bank imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kijamii nchini yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza ustawi wa jamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Abdallah Komba, aliipongeza Benki ya Exim kwa moyo wa kujitolea kusaidia jamii, akisema mchango huo utasaidia kuboresha huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya muda pamoja na wenye changamoto mbalimbali za kiafya.

“Benki ya Exim imeonyesha mfano mzuri wa uwajibikaji kwa jamii kwa kugusa moja kwa moja sekta ya afya ambayo ni muhimu kwa maisha ya wananchi. Msaada huu utasaidia kuokoa maisha ya watoto na akina mama wengi,” alisema Komba.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Stanley Kafu, alisema msaada huo umetokana na tathmini ya mahitaji halisi ya hospitali hiyo, huku lengo kuu likiwa ni kusaidia kupunguza changamoto zinazokwamisha utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa Geita.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Manispaa ya Geita, Dkt. Thomas Mauru, alisema msaada huo utaongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma kwa wakati na kwa ufanisi, hususan kwa watoto njiti na wale wanaozaliwa na changamoto za kiafya. Alisema vifaa hivyo vitasaidia kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa na hospitali hiyo kwa jamii inayowazunguka.

Mbali na shughuli hiyo ya kijamii, Benki ya Exim inatarajia kuzindua rasmi tawi lake jipya mkoani Geita, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi na wafanyabiashara wa mkoa huo. Uzinduzi huo unatarajiwa kufanywa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
SHIRIKA la Dawa Asili na Ulinzi wa Mazingira(TRAMEPRO) limesema linatambua na kuthamini mchango wao katika kukuza na kuendeleza sekta ya tiba asilia, ambayo imeendelea kuwa tegemeo muhimu kwa wananchi wengi katika huduma za afya.
TRAMEPRO imetoa kauli hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi, 2026.

Akitoa salaam kuhusu maadhimisho hayo ya Siku ya Wafanyakazi duniani Katibu Mkuu wa TRAMEPRO Boniventura Mwalongo amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa wanaungana na jumuiya ya kimataifa kusisitiza kuwa kazi ni msingi wa utu, heshima na maendeleo ya binadamu.

Amesema Kaulimbiu ya Mei Mosi mwaka huu inasema Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050,hivyo wanasisitiza umuhimu wa kazi zenye staha.

“Mafundisho ya kijamii na kiroho, kama yanavyoakisiwa na World Health Organization, yanaeleza kuwa kazi si tu njia ya kujipatia kipato, bali pia ni wito wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa jamii yenye haki, mshikamano na ustawi wa wote.

“Sekta ya tiba asilia na mbadala inaendelea kuwa mhimili muhimu wa mfumo wa afya, ikichangia utoaji wa huduma, ajira, uhifadhi wa maarifa ya jadi na kukuza uchumi wa ndani,”amesema na kusisitiza umuhimu wa kazi katika maendeleo ya taifa.

Ameongeza Baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema:“Kazi ni kipimo cha utu na msingi wa maendeleo ya binadamu.”

Kuhusu takwimu za ajira katika sekta ya tiba asili na mbadala amesema zaidi ya asilimia 70–80 ya watu duniani hutegemea tiba asilia na mbadala kwa kiwango fulani cha huduma za afya;

Amefafanua hali hiyo imezalisha mamilioni ya ajira duniani, zikiwemo za waganga wa jadi, watafiti, wazalishaji wa dawa za asili, washauri wa afya na watoa huduma za tiba jumuishi huku akieleza Shirika la Afya Dunuani inatambua rasmi kundi la wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala kama sehemu ya nguvu kazi ya sekta ya afya duniani.

Amesema kwa Afrika na Tanzania
Barani Afrika, zaidi ya asilimia 80 ya wananchi hutegemea tiba asilia, hivyo kuifanya kuwa sekta muhimu ya ajira vijijini na mijini;

Wakati huo huo amesema TRAMEPRO inasisitiza kuwa haki, usawa na heshima kwa wafanyakazi ni nguzo kuu ya maendeleo endelevu na mwito wao kwa Serikali ni kuendelea kuimarisha sera, sheria na usimamizi wa sekta ya afya na tiba asilia.

Pia kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, utafiti na ubunifu, kukuza ajira na kulinda haki za wafanyakazi na kwa vijana kuchangamkia fursa za ajira na ubunifu katika tiba asilia na mazingira.

Mwalongo amezungumzia umuhimi wa kuzingatiwa haki, mshikamano na uwajibikaji ambapo kwa kufanya hivto litajengwa taifa lenye afya bora, uchumi imara na maendeleo endelevu yanayomgusa kila Mtanzania.

“TRAMEPRO inaendelea kusimama bega kwa bega na Serikali, wadau wa ndani na nje ya nchi, pamoja na wafanyakazi wote katika kuhakikisha sekta ya tiba asilia na mazingira inachangia kikamilifu maendeleo ya taifa.”
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesisitiza kwamba bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 inapaswa kutoa mwelekeo wa Taifa katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.

Mchengerwa amesema hayo Jumapili Mei 03, 2026 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya kilichofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.

"Lazima tujiandae kikamilifu kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Hili si suala la kadi pekee bali lazima kuwe na utayari wa miundombinu, mifumo, dawa na rasilimali watu imara" alisema Mchengerwa.

Mchengerwa alisisitiza kwamba lazima mifumo ya TEHAMA iwe imara, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba uimarishwe huku akiweka mkazo kwa buzalishaji wa ndani kupewa kipaumbele na Wizara ya Afya.

"Lazima mifumo ya manunuzi itoe kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani. Katibu Mkuu nakuagiza usimamie hilo, ununuzi kupitia MSD na mifumo yetu ya manunuzi lazima izingatie hilo lakini kwa kuzingatia ubora" ameongeza.

Mchengerwa aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kupiga hatua ikiwemo kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia wastani wa asilimia 73 kwa mwezi Februari, 2026.

"Pia tumeendelea kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kupitia uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali za wilaya, vifaa tiba na rasilimali watu. Haya ni mafanikio ya pamoja chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" alisema Mchengerwa.

Pia alitoa wito kwa kila mtumishi, kuanzia makao makuu hadi hospitali za rufaa, kutoka idara hadi kituo cha afya, kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi na huruma kwa wananchi.

"Hatutavumilia ucheleweshaji wa huduma usio na sababu. Hatutavumilia upendeleo unaodhalilisha haki za mwananchi" alisisitiza Mchengerwa huku akiagiza Katibu Mkuu kufanyia kazi malalamiko ya wagonjwa kukaa muda mrefu bila kupata huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Seif Shekalaghe alisema kikao hicho kimelenga kujadili na kupitisha mwelekeo wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 yenye lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi pamoja na ustawi wa watumishi.

Naye Katibu wa Baraza hilo, Vivian Joseph ambaye ni Afisa Tawala Mkuu Wizara ya Afya alisema kupitia kikao hicho kitasaidia upatikanaji wa bajeti ambayo ni shirikishi kutekelezwa na watumishi wa wizara hiyo baada ya kupitishwa na bunge.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilicholenga kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2026/27.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi Wizara ya Afya kilichoketi jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.