Kilimanjaro-Tanzania: Kampuni ya Bia Serengeti (SBL) imeeleza mchango wa uwekezaji wa sekta binafsi katika mageuzi ya kiuchumi ya Tanzania wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Kudumi ya Bunge ya Bajeti katika kiwanda chake Kilimanjaro-Moshi.
Ziara hiyo ilitoa fursa kwa kamati kujionea moja kwa moja uwekezaji wa SBL nchini Tanzania, mchango wake katika sekta ya viwanda na uchumi kwa ujumla, pamoja na hatua zinazounga mkono kilimo cha ndani, ajira, maendeleo ya ujuzi, jamii na uendelevu wa mazingira.
Mkutano huo umefanyika wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza Dira 2050, ambayo inatambua sekta binafsi imara na yenye nguvu kama kichocheo muhimu cha mageuzi ya kiuchumi, tija, ubunifu, uwekezaji na uundwaji wa ajira.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti, Dkt. Obinna Anyalebechi, alisema SBL inaona uwekezaji wake nchini Tanzania ukienda mbali zaidi ya shughuli zake za uzalishaji hadi kufikia mnyororo mzima wa thamani na jamii inazofanya nazo kazi.
"Tanzania inapoelekea 2050, sekta binafsi ina jukumu muhimu la kuhakikisha matarajio ya Dira 2050 ya nchi yetu yanageuka kuwa matokeo halisi. Kwa hiyo tumefurahi kuwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti katika Kiwanda chetu cha Moshi na kuonyesha moja kwa moja uwekezaji tunaoufanya katika uzalishaji wa ndani, watu wetu, na mnyororo mpana wa thamani. Katika SBL, tunaendelea kujitolea kufanya kazi kwa ushirikiano na Serikali kuunga mkono ajenda ya viwanda ya Tanzania, kujenga na kuongeza ajira, kuimarisha minyororo ya thamani ya ndani, na kuchangia ukuaji endelevu wa kiuchumi," alisema Dkt. Anyalebechi.
Kwa miaka mingi, SBL imeendelea kuwekeza katika mnyororo wake wa thamani na katika mipango inayounga mkono vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania. Kupitia mpango wake wa Shamba ni Mali, kampuni inasaidia wakulima wadogo wanaolima mazao muhimu ikiwemo mtama, shayiri na mahindi, ikiwa na lengo la kufikia wakulima 10,000 ifikapo mwaka 2030. Mpango huu unalenga kuimarisha tija ya kilimo huku ukijenga uhusiano thabiti zaidi kati ya kilimo cha ndani na uzalishaji viwandani.
Katika ziara hiyo SBL pia ilieleza kuwa imewekeza katika jamii kupitia mpango wake wa ‘Water for Life’. Tangu mwaka 2010, kampuni imetekeleza miradi 32 ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 2, nakunufaisha zaidi ya Watanzania milioni mbili wanaoishi vijijini kwa kuwapatia maji safi na salama. Uwekezaji huu unaonyesha dhamira ya kampuni katika kushughulikia mahitaji ya jamii huku ikisaidia ustawi wa jamii na uchumi wa muda mrefu.
Aidha, kupitia mpango wake wa ‘Learning for Life’, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), SBL imewasaidia vijana wa Kitanzania kupata ujuzi katika sekta ya hoteli na utalii unaolenga kuboresha nafasi zao za ajira na kuimarisha mnyororo wa thamani wa utalii na ukarimu nchini.Uendelevu unaendelea kuwa kiini cha mkakati wa uwekezaji wa muda mrefu wa SBL, huku kampuni ikiendelea kuzingatia matumizi bora ya maji, kilimo endelevu, nishati jadidifu, ufungashaji wa bidhaa na hatua nyingine zinazolenga kupunguza athari zake za kimazingira huku ikijenga biashara imara.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe. Mashimba Ndaki, alisema mkutano huo ulikuwa muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na sekta binafsi na kutambua mchango wa biashara katika kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Tanzania.

"Ziara hii imetoa fursa ya kuelewa moja kwa moja mchango wa uwekezaji wa sekta binafsi katika uzalishaji viwandani, ajira, minyororo ya thamani ya ndani na jamii. Tunapoelekea kutimiza matarajio ya Dira 2050, ushirikiano endelevu kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kujenga mazingira yanayowezesha uwekezaji, tija na ukuaji endelevu wa uchumi," Mhe. Ndaki.
Ziara hiyo imethibitisha tena umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kusukuma mbele matarajio ya maendeleo ya muda mrefu ya Tanzania. Kwa SBL, ziara hii pia imesisitiza dhamira yake endelevu ya kuwekeza nchini Tanzania na kujenga thamani ya pamoja kupitia watu wake, minyororo ya thamani ya ndani pamoja na jamii kwa ujumla.





Toa Maoni Yako:
0 comments: