KICHWA kina gonga kama ngoma, unaona kizunguzungu, mwili hauna nguvu, unasikia kichefuchefu, kama unataka kutapika lakini hutapiki, kwa kifupi unajisikia hovyo kufuatia unywaji wa kupindukia ulioufanya jana! Hali hii inaitwa HANG-OVER au uchovu.

Ingawa hatupendi kuelezwa ukweli au kufikiria madhara ya pombe, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa pombe ni dawa ya kulevya. Ina dhoofisha mwili na pale mtu anapokunywa kupita kiwango, mwili hujawa na sumu.

Unapokutana na hali hiyo, mwili hujaribu kujinasua kama vile ambavyo kitu chochote kingefanya kinapovamiwa na kitu kigeni.Njia bora ya kuondokana na uchovu (hangover) ni kunywa kiasi au kuacha kabisa ulevi. Kama utashindwa kujizuia kunywa na unataka kujiepusha na uchovu asubuhi, ni vyema ukila vitu vifuatavyo ambavyo vinaweza kukusaidia:

1. NDIZI MBIVU

Unapozidiwa na kilevi, kiasi kikubwa cha madini ya potasiamu hupotea, hivyo kwa kula ndizi mbivu ambazo zinaaminika kuwa na kiwango kikubwa cha madini hayo, kutakusaidia kupunguza makali ya hang-over. Unachotakiwa kufanya ni kutafuta ndizi mbivu nzuri, menya na kula kwa wingi.
2. TANGAWIZI

Tangawizi mbichi imekuwa ikitumika kwa muda mrefu kutibu magonjwa mbalimbali, yakiwemo ya kusikia kichefuchefu na mafua. Andaa juisi ya tangawizi mbichi na kunywa kama ilivyo, au unaweza kuandaa kwa kukata vipande kati ya 10 hadi 12 na uchanganye na vikombe 4 vya maji. Chemsha kwa dakika 10, epua na chuja. Kisha changanya na juisi ya chungwa moja, kipande cha limau na nusu kikombe cha asali. Kunywa mchanganyiko huo utapata nafuu mara moja.

3. ASALI NA LIMAU

Asali na limau ni kinywaji bora kuliko vyote katika tiba hii, ni rahisi kutengeneza na kunywa. Kina rudisha haraka kiasi cha sukari na maji kilichopotea wakati wa kunywa kilevi. Chemsha maji kiasi cha kikombe kimoja, changanya limau na asali kupata ladha unayoitaka. Ni bora kutumia asali ili kupata sukari ya asili, badala ya kutumia sukari ya kawaida. Ili kupata ahueni, kunywa mchanganyiko huo mara kadhaa kwa siku.

4. SUPU,
WALI Mtu anapoanza kupata nafuu kutokana na uchovu, chakula huwa kitu cha mwisho kabisa kutamani kula, lakini pamoja na kutojisikia hamu ya kula, unahitaji kula ili mwili upate nguvu. Unashauriwa kuanza kwa kula vyakula vyepesi kama vile wali mweupe, supu, n.k

5. KINYWAJI MAALUM
Kunywa pia vinywaji maalum vinavyotumiwa na wanamichezo kwa lengo la kurejesha nguvu na madini yaliyopotea mwilini. Unaweza pia kunywa vinywaji vya kutia nguvu mwili (energy drink) kama vile, Red Bull, Shark, Malta Guiness, n.k

6. BARAFU
Ili kutuliza maumivu ya kichwa, chukua vipande vya barafu, weka kwenye mfuko wa plastiki ambao utazungurusha kwenye kitaulo na kuweka kwenye kipaji chako cha uso kinachogonga.

7. JUISI
Juisi, hasa fresh ya machungwa, husaidia kupandisha kiwango cha sukari kilichopotea na husaidia kuondoa dalili za uchovu mwilini. Hata hivyo, kama tumbo lako limechafuka sana, kunywa juisi ya epo (tufaha) badala ya machungwa ambayo ina asidi.

8. MAJI
Mbali ya muda, maji ni tiba bora ya uchovu. Upungufu wa maji unaotokana na kunywa kiasi kingi cha kilevi ndiyo unaoleta kasheshe mwilini. Kunywa maji mengi wakati wote wa mchana, siyo chini ya glasi nane kwa siku.

DONDOO MUHIMU
Ili kujiepusha na ‘hang-over’ asubuhi baada ya kunywa kupita kiasi, kunywa maji mengi sana kabla ya kupanda kitandani. Au kunywa taratibu, kinywaji kimoja kila baada ya saa moja kwani huo ndiyo muda unaotumika na kinywaji kusambaa mwilini na kutoweka.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: