*Bangi yamponza, aahidi kuwa balozi kwa wenzake.

Kamati ya kuzuia na kupambana na dawa zisizoruhusiwa michezoni ya Kanda ya Tano Afrika (RADO) imetoa hukumu ya kumfungia mchezaji Mohamed Issa kutokana na matumizi ya dawa zisizoruhusiwa michezoni aina ya Bangi.

Kwa mujibu wa Ibara ya 7.2 ADR inaelezea Mohamed Issa alivyokiuka ibara ya 2.1 ya RADO ADR ambayo inazungumzia kukataza matumizi ya dawa zisizoruhusiwa michezoni.

Kutokana na hilo Banka alitakiwa kutoa maelezo ikiwemo kukataa au kukubali kosa ambapo alikubali mashtaka hayo kwa kukiri kosa akichagua kujitetea kwa njia ya maandishi, utetezi aliouwasilisha Agosti mosi mwaka huu.

Baada ya uchunguzi wa maabara na utetezi toka kwa mchezaji huyo, Kamati imemkuta na hatia na imemfungua kwa kipindi cha miezi 14 kuanzia Disemba 9, na adhabu inatarajiwa kumalizika Februari 8, 2019.

Msemaji wa TFF Clifford Ndimbp ameeleza kuwa wakati wote Banka akitumikia adhabu hiyo hataruhusiwa kufanya chochote kinachohusiana na mpira wa Miguu, ikiwemo kufanya mazoezi hadharani au kuonekana akishiriki shughuli za mpira wa miguu.

TFF imesema kuwa mchezaji huyo alitakiwa kukutana na adhabu kubwa zaidi ikiwemo kufungiwa maisha lakini kamati kwa mamlaka iliyonayo imepunguza adhabu hiyo kufikia miezi 14 baada ya kumuona Mohamed Issa ni kijana mdogo.

Hata hivyo Kamati imesema kuwa ikijiridhisha kuwa Banka anatumikia adhabu ipasavyo itamruhusu kuanza mazoezi na klabu yake (Yanga SC) katika miezi miwili ya mwisho katika adhabu yake.

Kwa upande wake Mohamed Issa amekiri na kujutia kitendo alichokifanya cha kutumia Bangi na ameahidi kuwa balozi mzuri kwa wengine wanaotumia dawa hizo zisizoruhusiwa michezoni.

Mnamo Disemba 9, 2017 Mchezaji huyo akiwa Machakos nchini Kenya alichukuliwa vipimo vya mkojo ambavyo vilisafirishwa kwenda kwenye Maabara ya WADA iliyopo Doha,Qatar kwa uchunguzi zaidi na majibu kurudi yakiwa na tuhuma hizo zinazomkabili.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: