Articles by "HABARI NA MATUKIO"
Showing posts with label HABARI NA MATUKIO. Show all posts
Na Mwandishi Wetu, Arusha.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, ameingilia kati mgogoro wa ardhi uliodumu kwa takribani miaka 20 katika Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Monduli, kwa kupendekeza ekari 100 za eneo la mwekezaji kutengwa kwa ajili ya wananchi wa Kitongoji cha Zaburi.

Hatua hiyo inalenga kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo uliohusisha wananchi kuvamia eneo la ekari 200 linalomilikiwa na kampuni ya Rhino Equipment & Transportation na kuanzisha makazi pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Zaburi, Novemba 6, 2026, Makalla alisema kampuni hiyo ndiyo mmiliki halali wa eneo hilo, lakini Serikali imependekeza sehemu ya ardhi hiyo kutengwa kwa wananchi kutokana na uwepo wa kitongoji kilichosajiliwa na kuendelezwa kwa miundombinu ya kijamii.

Alisema kitongoji hicho tayari kina huduma muhimu zikiwemo msikiti, kanisa, shule ya awali, maji na umeme, hali inayohitaji suluhisho linalozingatia maslahi ya wananchi na haki za mwekezaji.

Aidha, Makalla aliuagiza uongozi wa kampuni hiyo kukutana na wananchi walioingia katika eneo lake jingine lenye ukubwa wa ekari 100 ili kujadiliana na kufikia makubaliano yatakayowezesha matumizi sahihi ya ardhi hiyo na kumaliza mgogoro huo.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu na kusitisha uvamizi pamoja na shughuli za kuendeleza maeneo hayo hadi mazungumzo na makubaliano yatakapokamilika.

Pia, aliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo na kuhakikisha eneo litakalotengwa kwa ajili ya wananchi linakuwa na mpango mzuri wa matumizi ya ardhi.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mzee Leng’ida alisema hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa pamoja na timu yake imerejesha matumaini kwa wakazi wa Kitongoji cha Zaburi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na sintofahamu kuhusu hatma ya makazi yao.

Alisema busara na hekima zilizotumika katika kutafuta suluhisho la mgogoro huo zitasaidia kuleta matumaini mapya na kuwarejeshea wananchi amani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makuyuni, Ngayoki, alisema atahakikisha maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa yanatekelezwa katika ngazi ya kijiji na kata kwa kushirikiana na wananchi.

Naye mkazi wa Kitongoji cha Zaburi, Naserian Saitabau, alisema mgogoro huo umewafanya wananchi kuishi kwa taharuki kwa miaka mingi kutokana na kutokuwa na uhakika wa hatma ya makazi yao.

Alisema hatua ya Mkuu wa Mkoa kuingilia kati imewapa matumaini mapya ya kupata suluhisho la kudumu litakalowawezesha kuishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Dkt. Khalid Bin Mohammed Al Attiyah, Mwenyekiti wa Kampuni ya Thirty Five Investment Holding inayoshughulika na masuala ya Kilimo, Uvuvi Bahari Kuu, Ufugaji, Madini na Miundombinu kutoka Qatar, Ikulu, Jijini Dar es Salaam, tarehe 06 Novemba, 2026.
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa kwenye picha na Dkt. Khalid Bin Mohammed Al Attiyah, Mwenyekiti wa Kampuni ya Thirty Five Investment Holding ya Qatar mara baada ya mazungumzo yao, Ikulu, Jijini Dar es Salaam, tarehe 06 Novemba, 2026.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa kampuni ya Thirty-Five Investment Holding kutoka Qatar, Dkt. Khalid bin Mohammed bin Abdullah Al Attiyah, kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 6, 2026, Dkt. Al Attiyah ameeleza nia ya kampuni yake kuwekeza katika sekta za kilimo na ufugaji, ikiwemo uzalishaji wa sukari na ufugaji wa ng'ombe katika eneo la Kongwa mkoani Dodoma.

Katika sekta ya uvuvi, mazungumzo yamejikita katika fursa za uvuvi wa bahari kuu pamoja na uwekezaji katika mitambo ya uchakataji na miundombinu ya kuhifadhi samaki katika Bandari ya Uvuvi Kilwa.

Aidha, mwekezaji huyo ameeleza kuwa kampuni yake inatathmini fursa za kuwekeza katika miundombinu ya usafiri Zanzibar, ambako majadiliano kati ya timu yake na wataalamu wa taasisi husika kuhusu miradi inayopendekezwa yameanza.

Kwa upande wake, Rais Samia amezitaka taasisi zinazohusika kuendeleza majadiliano na kampuni hiyo kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kubaini fursa za uwekezaji zinazoweza kutekelezwa kwa manufaa ya pande zote.
Mahakama Kuu ya Tanzania imemhukumu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kifungo cha miaka minne jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Novemba 6, 2026, na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru. Mahakama pia imemweleza kuwa ana haki ya kukata rufaa.

Awali, akizungumza kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Lissu alisisitiza kuwa haombi msamaha kwa sababu anaamini hana hatia. Alipinga kutiwa hatiani kwa uchochezi, akisema shtaka alilokuwa akikabiliwa nalo lilikuwa la uhaini.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Baadaye alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 10, 2025, ambako alisomewa shtaka la uhaini.

Hadi leo, amekuwa kizuizini kwa takribani mwaka mmoja na miezi saba akisubiri kukamilika kwa kesi yake. Akizungumza mahakamani kabla ya kupewa adhabu, Lissu amesema leo ni siku yake ya 577 akiwa mahabusu.

MAHAKAMA YAMTIA HATIANI LISSU KWA KOSA LA UCHOCHEZI, JAMHURI YAOMBA ADHABU KALI

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

Jaji Dustan Ndunguru, akisoma uamuzi wa Mahakama leo Novemba 6, 2026, kwa niaba ya jopo la majaji, amesema Mahakama imeridhika kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, alitenda kosa la uchochezi kwa mujibu wa Kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu, hivyo kumtia hatiani kwa kosa hilo.

Jaji Ndunguru amesema Mahakama inaamini kuwa Lissu alikuwa na taarifa ya kosa dogo la uchochezi na alikuwa na nafasi ya kujitetea, huku ushahidi wote uliotolewa ukijikita katika suala la uchochezi na kauli za kumchochea umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, upande wa mashtaka ulisimama kuwasilisha hoja kuhusu adhabu inayopaswa kutolewa dhidi ya mshtakiwa.

Akizungumza kwa niaba ya Jamhuri, Katuga amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 339 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Mahakama inaweza kupokea ushahidi hadi kufikia hatua ya kutoa adhabu inayofaa.
Amesema moja ya malengo ya adhabu ni kutoa onyo kwa mtu aliyepatikana na hatia ili asirudie kosa hilo au kutenda makosa mengine, pamoja na kuwa onyo kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.
Katuga amesema licha ya kutokuwepo kwa kumbukumbu za makosa ya awali dhidi ya mshtakiwa, taarifa zilizopo polisi zinaonyesha ongezeko kubwa la watu wanaotenda makosa ya kuchochea umma kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa au kiuchumi.
Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano ili kuwa na jamii yenye umoja, mshikamano na uzalendo sanjari na kuuimarisha Muungano.

Elimu inayotolewa inahusu hoja zilizopatiwa ufumbuzi ambapo hadi kufikia mwaka 2025/26 jumla ya hoja 24 kati ya hoja 25 zimepatiwa ufumbuzi na hoja moja iliyobaki inayohusu masuala ya fedha inaendelea kufanyiwa kazi.

Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma leo Novemba 06, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbatu Mhe. Juma Othmani Hija aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuwaelimisha Wananchi Hoja zote zilizo kwisha kupatiwa ufumbuzi ili wazielewe.

Akijibu swali hilo Mhe. Kwagilwa alisema kuwa Serikali imechukua jitihada mahususi za kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano ikiwemo kueleza wananchi hoja zilizopatiwa ufumbuzi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akifurahia jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe wakati wa kikao cha Bunge jijini Dodoma leo Novemba 06, 2026.
---
Alibainisha kuwa elimu ya Muungano imekuwa ikitolewa kupitia redio, televisheni, makala za magazeti, machapisho vikiwemo vitabu kuhusu Muungano, maonesho ya kitaifa, makongamano, vyombo vya usafiri ambavyo ni treni ya kisasa ya SGR, boti za Azam Marines na mitandao ya kijamii.

Halikadhalika, Naibu Waziri Kwagilwa alisema Ofisi ya Makamu wa Rais ina mpango wa elimu kwa umma inayotolewa katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuyafikia makundi yote ya kijamii.

“Mheshimiwa Spika hivi sasa Ofisi yetu inao mpango kabambe wa kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano mkoa kwa mkoa wilaya kwa wilaya kwa kutumia njia mbalimbali na tutahakikisha wananchi wanapata elimu hii,” alisema Mhe. Kwagilwa.

Aliongeza kuwa kutokana na uwepo wa watengeneza maudhui wenye ushawishi kwa jamii hususan makundi ya vijana, Ofisi imeandaa maudhui ambapo hivi karibuni wananchi wataanza kuyapata kupitia kwa wadau hao.

Mhe. Kwagilwa alieleza hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Hija ambaye pamoja na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mpango huo wa elimu, alitaka kujua kama kuna njia zingine za kutumia kufikisha elimu hiyo.
Na Dk Reubeni Lumbagala 

Mkoa wa Tanga ni maarufu kwa uzalishaji wa matunda nchini. Machungwa ni miongoni mwa matunda yanayozalishwa kwa wingi katika wilaya za Muheza, Korogwe na Handeni mkoani humo.

Wakulima wa zao hili hufanya jitihada kubwa za uzalishaji, lakini bado hawajafaidi vya kutosha jasho lao. Wakulima hutegemea baada ya kuvuna, wauze machungwa kwa bei nzuri ambayo itarejesha gharama za uendeshaji.

Aidha, wakulima hao hutegemea kupata faida kwani kwao kilimo hicho ni ajira kwa ajili ya kuendesha maisha yao na kufanya mambo mengine ya maendeleo kama kusomesha watoto, kujenga nyumba, kufungua biashara, kununua vyombo vya moto za usafiri, kutaja kwa uchache.

Miongoni mwa changamoto katika kilimo cha machungwa ni bei ndogo na kukosa soko la uhakika. Hili limesababisha wakulima kuuza machungwa yao mashambani kwa madalali.

Kwa kufanya hivyo, wakulima wamejikuta wakiuza machungwa yao kwa bei ndogo huku madalali wakinufaika pasi na kumwaga jasho kama walivyomwaga wakulima.

Kutokana na changamoto hizi, serikali ya mkoa wa Tanga chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa, Balozi Dk. Batilda Buriani, umejizatiti kuinua zao hili ili libadili hali za maisha ya wakulima na kuchangia katika maendeleo.

Novemba 1, 2026, katika kikao cha viongozi wa mkoa na wilaya, Dk. Buriani alisema, mkoa wa Tanga huzalisha asilimia 60 ya machungwa yote nchini, hivyo ni muhimu kuweka mazingira mazuri ya biashara hiyo ili iwanufaishe wakulima.

"Tumepiga marufuku madalali kununua machungwa mashambani, machungwa yatauzwa katika vituo maalum, hii itasaidia machungwa kuuzwa kwa bei nzuri," amesema Dk. Buriani.

Katika hatua nyingine, Dk. Buriani amesema, serikali mkoani humo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), watajenga vituo vinne ambapo wanunuzi wa machungwa watakwenda kununua moja kwa moja katika vituo hivyo kwa bei elekezi.

Kimsingi, ujenzi wa vituo hivi na kuwa na bei elekezi ya machungwa ni mkakati mzuri wa kuinua zao hili. Ni wakati muafaka sasa kwa wakulima kufaidi jasho lao na kuona fahari kulima machungwa kwani sasa kilimo hicho kitalipa na chenchi itabaki.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa maelekezo kwa wapiga kura watakaoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Chamwino na Udiwani katika kata 11 za Tanzania Bara, ikiwataka kuzingatia taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa amani na utulivu.

Miongoni mwa maelekezo yaliyotolewa ni kuruhusu baadhi ya wapiga kura kupiga kura hata kama hawana kadi zao, kadi zimeharibika au kuna tofauti ya namba ya mpiga kura, mradi taarifa zao zinathibitishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs C. M. Mwambegele, amesema mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika anaweza kutumia kitambulisho cha Taifa (NIDA), leseni ya udereva au hati ya kusafiria, iwapo majina yake yanafanana na yale yaliyopo katika daftari la wapiga kura.

Aidha, amesema mpiga kura ambaye hana picha katika daftari lakini ana kadi yenye taarifa binafsi zinazolingana na zilizopo kwenye daftari, anaruhusiwa kupiga kura. Hali kadhalika, mpiga kura ambaye namba ya kadi yake inatofautiana na ile iliyopo kwenye daftari, lakini taarifa nyingine zikiwemo picha na majina zinafanana, ataruhusiwa kushiriki uchaguzi.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa mtu ambaye ana kadi ya mpiga kura lakini taarifa zake hazipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hataruhusiwa kupiga kura.

Jaji Mwambegele ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi mdogo unaofanyika leo Novemba 4, 2026, ambapo jumla ya wapiga kura 213,024 wanatarajiwa kushiriki.

Amesema kati ya hao, wapiga kura 133,864 wameandikishwa katika Jimbo la Chamwino, huku 79,160 wakiwa katika kata 11 zinazofanya uchaguzi wa udiwani.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, uchaguzi huo utasimamiwa katika vituo 665, vikiwemo 441 vya Jimbo la Chamwino na 224 katika kata 11.

Katika uchaguzi huo, jumla ya wagombea 67 kutoka vyama 17 vya siasa wanawania nafasi za ubunge na udiwani. Jimbo la Chamwino lina wagombea 16 wa ubunge, wakiwemo wanaume wanane na wanawake wanane.

Kwa upande wa udiwani, wagombea 51 wanawania nafasi hizo katika kata 11, ambapo wanaume ni 43 sawa na asilimia 84.31, huku wanawake wakiwa wanane sawa na asilimia 15.69.

Jaji Mwambegele amevikumbusha vyama vya siasa kuhakikisha vinaweka mawakala katika vituo vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura ili kulinda maslahi ya wagombea wao na kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Amesema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Hata hivyo, wapiga kura watakaokuwa kwenye foleni wakati wa kufungwa kwa vituo wataruhusiwa kuendelea kupiga kura hadi wote watakapomaliza.

Aidha, amewataka wapiga kura kwenda katika vituo walivyojiandikisha wakiwa na kadi zao, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wazee, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wajawazito na wanawake wenye watoto wachanga.

Amesema watu wenye mahitaji maalumu wanaruhusiwa kwenda vituoni wakiwa na wasaidizi wao, huku wapiga kura wakitakiwa kuondoka katika eneo la kituo mara baada ya kukamilisha zoezi la kupiga kura.

Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi wote katika maeneo yanayofanya uchaguzi kujitokeza kwa wingi na kutumia haki yao ya kidemokrasia kuwachagua viongozi wanaowataka.

Sherehe rasmi ya uzinduzi wa Plaza Premium Lounge mpya imefanyika katika Jengo la Tatu la Abiria (Terminal 3), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, tarehe 2 Novemba 2026. Ukumbi huo unawapatia wasafiri eneo maalumu la kupumzika, kupata huduma za chakula na vinywaji pamoja na kujiandaa na safari zao kabla ya kupanda ndege.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ni Mhe. Kiema Kilonzo, Mjumbe wa Bodi ya Plaza Premium Lounge Africa (kushoto), akiwa pamoja na Anis Jmour, Makamu wa Rais wa Biashara wa Plaza Premium Group, Kanda ya Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika (EMEA) (kulia).

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, 02 November 2026: Plaza Premium Group (PPG), kampuni ya kimataifa inayotoa huduma za ukarimu viwanja vya ndege, imefungua rasmi Plaza Premium Lounge yake ya kwanza nchini Tanzania, katika Terminal 3 ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam.

Lounge hiyo, iliyopo karibu na Lango la 6 katika eneo la safari za kimataifa, ina ukubwa wa mita za mraba 336 na uwezo wa kuhudumia wageni 86 kwa wakati mmoja. Inatoa sehemu za kupumzika, kuoga, huduma za chakula na vinywaji, maeneo ya kufanyia kazi, intaneti na sehemu za kuchaji vifaa vya kielektroniki, pamoja na vyumba vya ibada.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu wa Rais wa Biashara wa Plaza Premium Group, Kanda ya EMEA, Anis Jmour, alisema kuanzishwa kwa lounge hiyo nchini Tanzania ni hatua muhimu katika upanuzi wa kampuni hiyo Afrika Mashariki, huku kukiwa na fursa ya kuleta uzoefu wake wa kimataifa wa huduma za ukarimu karibu na wasafiri wanaotumia JNIA.
“Ufunguzi wa Plaza Premium Lounge nchini Tanzania ni hatua muhimu katika upanuzi wetu barani Afrika. Tunaona umuhimu wa soko la Tanzania katika kuunganisha safari za kikazi na mapumziko, na tunalenga kuwapa wasafiri huduma zinazokidhi mahitaji yao kabla ya kuendelea na safari,” alisema Jmour.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Bertha Bankwa, alisema ujio wa Plaza Premium Lounge unazidi kuonesha ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania na umuhimu wa kuendelea kuboresha huduma zinazotolewa kwa abiria kadiri mahitaji ya usafiri yanavyoongezeka.

“Ujio wa huduma hii unaonesha jinsi sekta yetu ya usafiri wa anga unavyoendelea kukua na kuvutia wawekezaji wanaoleta huduma mpya kwa wasafiri. Kadiri idadi ya abiria inavyoongezeka, ni muhimu pia kuendelea kuboresha uzoefu wao wanapotumia uwanja wetu wa ndege, ili kuhakikisha wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao,” alisema Bankwa.
Ukuaji huo unaonekana pia katika takwimu za usafiri wa anga. Kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania in Figures 2025 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), iliyotumia takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), idadi ya abiria wa ndani na wa kimataifa katika viwanja vya ndege nchini ilifikia takribani milioni 8.11 mwaka 2025, kutoka milioni 7.38 mwaka 2024. JNIA pekee ilihudumia takribani abiria milioni 2.92 katika kipindi hicho.

Ukuaji wa usafiri wa anga nchini Tanzania unaendana na umuhimu wa nchi kama moja ya vivutio vikuu vya utalii na eneo la fursa za biashara. Kutoka Serengeti na Mlima Kilimanjaro hadi Zanzibar, Tanzania inaendelea kuvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani, jambo linaloifanya huduma inayotolewa kwa wasafiri wanapowasili au kuondoka nchini kuwa sehemu muhimu ya uzoefu wao wa safari.

Ni katika mazingira haya ambapo Plaza Premium Group inaleta uzoefu wake wa kimataifa nchini Tanzania. Kwa takribani miaka 30 katika sekta ya ukarimu viwanja vya ndege, kampuni hiyo ilianzisha dhana ya lounge huru ya uwanja wa ndege mwaka 1998. Kwa sasa, inafanya shughuli zake katika viwanja vya ndege zaidi ya 600 katika nchi zaidi ya 150, ikihudumia zaidi ya abiria milioni 30 kila mwaka.

Hata hivyo, huduma za ukarimu zinapopelekwa katika soko jipya, kuzingatia utamaduni na utambulisho wa eneo husika ni sehemu muhimu ya uzoefu unaotolewa. Kupitia mkakati wake wa Proudly Local, Plaza Premium Group inalenga kuunganisha viwango vyake vya kimataifa na ladha za Kitanzania. Katika lounge yake ya Dar es Salaam, hilo linaonekana kupitia menyu inayojumuisha vyakula na vitafunwa vya Kitanzania pamoja na baadhi ya bidhaa zinazopatikana nchini.

Kwa wasafiri wanaotaka kutumia huduma hizi, Plaza Premium Lounge Dar es Salaam inafunguliwa kila siku. Nafasi zinaweza kuwekewa mapema kupitia www.plazapremiumlounge.com au tiketi kununuliwa moja kwa moja wanapofika kwenye lounge hiyo.

Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju amewataka Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake kutumia vema maarifa waliyopata kutoka katika shule hiyo kama mwanzo wa safari na si kikomo cha ndoto.

Mhe. Masaju alieleza hayo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza alipokuwa akitoa hotuba yake akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza shule ambayo naye alisoma katika safari yake ya kitaaluma.

“Leo nimesimama kama mmoja wa watu ambao safari yao ilipita katika shule hii. Sitaki mnaponisikia mseme tu kwamba mwanafunzi wa zamani wa Lake amefika katika nafasi hii. Nataka mjifunze jambo pana zaidi: safari ya maisha hujengwa kwa hatua, kwa watu wanaotusaidia, kwa maamuzi tunayofanya na kwa juhudi tunazoweka kila siku. Msifikiri kwamba lazima muanze mkiwa na kila kitu. Anzeni kwa kutumia vizuri kile mlicho nacho, muda wenu, nafasi ya kujifunza, ushauri mnaopewa na vipaji mlivyonavyo,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao kuendelea kujifunza, kuwa waadilifu, kutobadili misingi yao kwa faida ya muda mfupi, kuheshimu watu, kutumia teknolojia kwa busara, kuipenda Tanzania kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu sheria, kulinda mali za umma na kutatua matatizo ya jamii.

“Msisubiri mazingira yawe kamili ndipo mfanye bidii. Jengeni uwezo wenu katika mazingira mliyopo, huku mkiboresha mazingira hayo kwa manufaa ya wengine,” amesisitiza Jaji Mkuu na kusema kwamba, angependa siku zijazo, asikie simulizi za wahitimu wa leo: walioboresha huduma za afya, waliobuni teknolojia, walioanzisha biashara na ajira, waliotetea haki, waliofundisha vizazi vipya na walioleta mabadiliko chanya katika jamii zao. Hizo ndizo simulizi zinazojenga heshima ya taasisi.

Ameongeza kuwa, Kidato cha Nne ni hatua muhimu, lakini si mwisho wa elimu wala mwisho wa kujijenga. Ni mlango unaofunguka kuelekea hatua nyingine. Amesema, “baadhi yenu mtaendelea na Kidato cha Tano na Sita; wengine mtachagua mafunzo ya ufundi na stadi; wengine mtajiandaa kwa njia nyingine za kujifunza na kujenga taaluma. Njia zinaweza kutofautiana, lakini wajibu ni mmoja: kuendelea kujifunza na kujitengeneza.”

Aidha, amewakumbusha wahitimu hao kutokimbilia kutafuta mafanikio yanayoonekana kabla hawajajenga msingi wa mafanikio ya kweli kwakuwa Dunia ya sasa inaweza kumfanya kijana aamini kwamba mafanikio ni kuonekana, kuwa maarufu au kupata fedha haraka. Amesema, huo si msingi salama wa maisha kwani mafanikio ya kudumu yanahitaji maarifa, ujuzi, nidhamu, uvumilivu, uaminifu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayewaangalia.

Kadhalika, Jaji Mkuu amewaasa Wahitimu hao wa Kidato cha Nne kumcha Mungu na wawe na dhamira inayowaongoza kutenda yaliyo mema huku akinukuu Biblia Takatifu, katika Mithali 4:13, inayohimiza kuishika elimu na Qur’ani Tukufu, katika Suratul Al-Alaq (96:1–5), inatukumbusha umuhimu wa kusoma na kujifunza ambapo mafundisho hayo yanatuelekeza kuona elimu kama wajibu na neema inayopaswa kutumiwa kwa busara. Vilevile, amewataka kuwaheshimu wazazi, walezi na walimu wao na kusisitiza kuwa heshima si udhaifu; ni alama ya ukomavu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewataka Wahitimu hao kutosubiri Taifa liwaite viongozi ndipo waanze kuonesha uongozi hivyo, amewasisitiza kuanza kuongoza maisha yao kwa nidhamu, kwa kuwa waaminifu, kwa kuwaheshimu wengine na kwa kutimiza wajibu wao kwakuwa Uongozi huanza kabla ya cheo.

Akiizungumzia Shule ya Sekondari Lake, Jaji Mkuu amesema anaiheshimu na kusisitiza Lake isiwe shule inayojivunia tu watu waliopita hapo bale iwe shule inayowaandaa watu ambao Taifa litajivunia kesho. “Kila mhitimu anayekuwa muadilifu, kila mtaalamu anayefanya kazi kwa ubora, kila kiongozi anayewajibika na kila kijana anayebuni suluhisho jipya, anaongeza ukurasa katika historia ya Lake,” amesisitiza.

Kadhalika, Mhe. Masaju amewakumbusha watu mbalimbali waliomaliza katika shule hiyo na katika shule nyingine nchini kuwa na utaratibu wa kuzitembelea shule walizosoma. Amesisitiza kwa kusema, “Tunaporejea mashuleni tulikosoma, tunapata fursa ya kutoa shukrani na kukutana na wale waliochangia kutujenga.”

Jaji Mkuu amesema, amerudi shuleni hapo akiwa na dhamira ya kutoa shukrani, kutambua mchango wa shule hiyo na, muhimu zaidi, kuwaambia wanafunzi wa leo kwamba ndoto zao zinaweza kuwapeleka mbali zaidi ya mipaka wanayoiona sasa.

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu ameushukuru Uongozi wa Shule hiyo kwa kumualika na kumpa nafasi ya kurejea katika Shule ya Sekondari Lake mahali pa kumbukumbu, malezi na sehemu ya safari ya maisha yake na wengine wengi waliopita katika shule hiyo. Ameomba shule hiyo iendelee kung’aa, si kwa historia yake tu, bali kwa ubora wa watu inaowaandaa kwa ajili ya Tanzania.

“Nimepokea mwaliko huu kwa heshima kubwa. Lakini niseme wazi: kwangu mimi, leo si siku ya kutembelea shule nyingine tu; ni siku ya kurejea mahali ambapo sehemu ya safari yangu ya maisha ilianzia. Kabla ya vyeo vyetu, kabla ya ofisi zetu, kabla ya majukumu yetu kitaifa na kabla ya heshima tuliyokuwa nayo, tulikuwa wanafunzi. Nasi pamoja na Madaraka yetu tulikuwa vijana wenye safari mbele yetu, wenye mambo ya kujifunza, wenye ndoto na wenye wajibu wa kufanya bidii,” amesema Mhe. Masaju.

“Ningependa niwaambie jambo moja mapema: msinitazame leo kwa kuona tu cheo nilichonacho. Nitajeni pia kama mmoja wa wanafunzi waliowahi kukaa madarasani hapa, kusoma, kufundishwa na kuandaliwa kwa maisha. Cheo ni dhamana ya leo; lakini historia ya mtu hujengwa hatua kwa hatua, na mara nyingi hatua hizo huanzia katika madarasa kama haya,” ameeleza.

Kadhalika, Jaji Mkuu amekiri kupokea kwa furaha taarifa ya wazo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Lake (Lake University) ambapo amewapongeza viongozi na wadau wa shule kwa kuwa na ndoto hiyo. Amesema, Taasisi inayothubutu kufikiria hatua inayofuata inaonesha kuwa haitaki kuishi kwa kutegemea historia pekee; inataka kushiriki katika kuandika historia mpya.

“Nimeelezwa pia kuhusu changamoto ya eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili ya mradi huo. Changamoto hiyo isitumike kuzima ndoto, bali iwe nafasi ya kutathmini upya mpango. Hata hivyo, ndoto ya chuo kikuu inahitaji maandalizi ya kitaalamu na ya muda mrefu: upembuzi yakinifu, mahitaji ya jamii na soko la ajira, maeneo ya kitaaluma yatakayopewa kipaumbele, uwezo wa kifedha, miundombinu, rasilimali watu, usimamizi na utii wa taratibu za mamlaka husika,” amesisitiza.

Ameushari uongozi wa shule hiyo uandae mpango kabambe wa hatua kwa hatua, ukiangalia mahitaji ya sasa na ukuaji wa taasisi kwa miaka mingi ijayo. Eneo la chuo lisitazamwe kwa mahitaji ya leo pekee; litazamwe kwa uwezo wa kupanuka, usafiri, huduma, mazingira na mahitaji ya wanafunzi na wafanyakazi. Ndoto kubwa inahitaji maandalizi makubwa, lakini utekelezaji wake uanze kwa hatua zinazopimika.

Kadhalika, ametoa wito kwa wadau wote kuendelea kuwekeza katika walimu, maabara, maktaba, teknolojia, michezo, ushauri nasaha na mazingira salama ya kujifunzia na si kuwekeza katika majengo pekee bali wawekeze pia kwa watu, mifumo na maadili yanayofanya majengo hayo yawe na maana.

Awali akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma amesema jumla ya Wanafunzi 76 wamehitimu kidato cha nne, 30 Wanawake na 46 Wanaume.

Mwalimu Bunuma amemshukuru Jaji Mkuu, Mhe. Masaju kwa heshima na fadhila kubwa ambayo amefanya kwa uongozi wa shule hiyo kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu.

“Tunajua una majukumu mengi na katika shughuli zako ikiwa ni pamoja na familia, bado umetupa kipaumbele siku hii ya leo, na umetupa hadhi kubwa ya kitaifa, wewe ambaye ulikuwa mwanafunzi wa shule hii, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wengine waliosoma hapa na wamehudhuria mahafali ya leo,” amesema Mkuu wa Shule huyo.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya Taaluma, Mwalimu Bunuma ameishukuru Bodi ya Wamiliki ya Shule hiyo kwa kuboresha mazingira mazuri yanayohamasisha wanafunzi kujifunza na kufundisha. “Tumepata ushindi wa daraja la kwanza, la pili, la tatu pekee kwa mwaka 2025. Kidato cha nne na cha sita ufaulu wetu ni asilimia 100. Kwa mfano mwaka 2025, kidato cha nne daraja la kwanza tulikuwa na wanafunzi 44, daraja la pili wanafunzi 33, daraja la tatu wanafunzi 4. Kidato cha sita daraja la kwanza walikuwa ni wanafunzi 20, daraja la pili walikuwa ni wanafunzi 36, na daraja la tatu walikuwa ni wanafunzi 10,” amesema.

Katika Mahafali hayo Kadhalika Jaji Mkuu alipata wasaa wa kutembezwa katika maeneo mbalimbali ya shule hiyo ikiwemo Maabara, Maktaba na sehemu nyingine kadhaa ambapo alijionea maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika shule hiyo. Kadhalika, Mhe. Masaju amekutana na Mwalimu aliyemfundisha Somo la Kemia (Chemistry), Mwalimu Kiran Mody ambapo ameonesha furaha baada ya kukutana na Mwalimu huyo.

Miongoni mwa Viongozi waliosoma katika shule hiyo ni pamoja na Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Mhe. Dkt. Stegomena Tax, aliyekuwa waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, lakini pia alikuwa katibu mtendaji wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC), Dkt. Angelina Mabula na wengine kadhaa.

Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa Wahitimu, Wanafunzi na Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora igizo la uendeshaji wa Mahakama ya Mazoezi (Moot Court).

Matukio katika picha ya Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju leo tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza. Mhe. Masaju alikuwa Mgeni Rasmi wa Mahafali hayo yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.
Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza wakiwa katika Mahafali yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akitoa hotuba yake wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026 jijini Mwanza.
Sehemu ya Wazazi, Walezi pamoja na Wageni Waalikwa wakisikiliza hotuba ya Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026.
Wahitimu wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Lake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Mwanza, Mhe. Ephery Kisanya akizungumza jambo wakati wa Mahafali hayo.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akisalimiana na aliyekuwa Mwalimu wake wa Somo la Kemia, Mwalimu Mstaafu wa Shule ya Sekondari Lake, Kiran Mody.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akipokea zawadi kama ishara ya upendo kutoka Uongozi wa Shule ya Sekondari Lake iliyopo jijini Mwanza.
Sehemu ya Viongozi wa Shule ya Sekondari Lake wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne yaliyofanyika tarehe 02 Novemba, 2026. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Lucas Bunuma.


Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stagomena Tax akizungumza jambo wakati wa Mahafali hayo.


Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake, Mwalimu Lucas Bunuma akitoa neno wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake jijini Mwanza.


Katibu wa Baraza la Uongozi wa Shule akitoa neno.


Igizo la Uendeshaji Mahakama ya Mazoezi (Moot Court) likifanywa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lake wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.


Burudani kutoka kwa Wanafunzi wakati wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Lake.



Burudani kutoka katika Kikundi cha Ngoma za Asili cha Bujora.

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiangalia moja ya vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Shule ya Sekondari Lake.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi waliosoma (Alumni) katika Shule ya Sekondari Lake ambao ni pamoja na Mhe. Dkt. Stergomena Tax (wa tatu kushoto), Mwalimu Lucas Bunuma (wa kwanza kushoto). Aliyesimama wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni.


Jaji Mkuu akipata maelezo alipotembelea Maabara ya Shule ya Sekondari Lake tarehe 02 Novemba, 2026 alipoalikwa kuwa Mgeni Rasmi wa Mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo.


Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Lake kuhudhuria Mafahali ya Kidato cha Nne ya Shule hiyo tarehe 02 Novemba, 2026.




Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. George Masaju akiwa katika picha za pamoja na Wahitimu wa Kidato cha Nne pamoja na baadhi ya Viongozi wengine walioshiriki katika Mahafali hayo.


Sehemu ya picha za Makundi wakati wa Mahafali ya Shule ya Sekondari Lake. (Picha na MARY GWERA, Mahakama)