Na Mwandishi Wetu

JANA Saa 9 na dakika 37 mwili wa aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na baadaye Meneja Mkuu wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF), Rehani Athumani ulizikwa katika eneo la nyumba yake Kivule maarufu kwa John Feza (Halahala) wilayani Ilala nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.

Rehani (54) ambaye hadi kufikia mwaka jana, alikuwa Meneja Mkuu wa CHF, alifariki dunia ghafla Jumanne kwenye Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.

Alizikwa katika maziko yaliyohudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki na watendaji na watumishi wa NHIF.

Awali kabla ya maziko hayo, mwili wake ulitolewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kufikishwa nyumbani kwa dada yake, eneo la Karakata, karibu na Msikiti wa Biesta kwa Mama Mihambo. Aliswaliwa hapo kabla ya maziko.

Miongoni mwa walioshiriki msibani hapo na baadaye mazikoni ni aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba, watendaji wa zamani wa NHIF, Michael Mhando, Eugen Mikongoti, pamoja na watendaji na watumishi wengine wa sasa wa mfuko huo. 

Mwanataaluma huyu wa Habari na Mawasiliano, baada ya kutoka NHIF alikuwa Mwanzilishi Mwenza wa Taasisi ya Community Health Development Initiative (CHDI) inayohusisha ushauri katika sekta ya afya.

Kwa mujibu Mwanzilishi Mwenza mwingine wa CHDI, Eugen Mikongoti, Rehani alifariki wakati akipatiwa huduma katika Hospitali ya Regency Dar es Salaam. Alikuwa Mkuu wa Miradi na Ushauri katika CHDI. 

Akiwa maarufu miongoni mwa wadau wa sekta ya afya na waandishi wa habari, Rehani anatambulika kwa sura yake ya bashasha na kasi ya kufanya kazi, sifa aliyejizolea miongoni mwa waandishi wa habari. 

Alikuwa mmoja wa viongozi waliosimama kidete katika kuhakikisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unapata ustawi, unafahamika kwa wananchi na unatekeleza lengo lililokusudiwa la kuwapatia Watanzania tiba bora.

Pamoja na kufanya kazi za utawala akiwa lililokuwa Shirika la Akiba la Taifa (NPF) baadaye Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kisha NHIF, Rehani pia amekuwa akifanya kazi za habari kwa kulisha blogu yake ya Uyui ambayo inaelezea mambo mbalimbali yanajiri mkoani Tabora. Akitumia jina la Maganga Feruzi.

Alizaliwa Agosti 21, 1964 katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora, ya Kitete akiwa ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto sita, wa Mzee Athumani Malingo na mama Joha.

Alisoma sekondari za Chemchem iliyopo Tabora na Kidato cha Tano na Sita amesema Tosamaganga mkoani Iringa.

Alipata masomo katika vyuo mbalimbali vikiwamo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Turin nchini Italia na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) akipata Shahada ya Uzamili katika Uongozi na Maendeleo.

Akiwa amefanya kazi miaka 30 katika NPF, NSSF na NHIF, Rehani Athumani ambaye pia alishawahi kushika nafasi ya Meneja Mkuu wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF), ameacha mjane na mtoto mmoja wa kike, Khadija (9).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: