Wananchi wa Kijiji cha Somanga Simu wakiwa katika mkutano wa hadhara kusikiliza masuala yahusuyo usalama na ulinzi wa bomba la gesi yaliyokuwa yakizungumzwa na wataalamu kutoka TPDC
Wananchi wa Kijiji cha Kiwanga wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu kutoka TPDC baada ya kupata elimu kuhusu masuala ya usalama na ulinzi wa miundombinu ya gesi asilia.

Na Mwandishi Wetu.

Kutokea kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Lindi na Mtwara, limelala bomba lenye kipenyo cha inchi 36 na urefu wa kilometa 551 kuelekea jijini Dar es Salaam. Bomba hili lina uwezo wa kupitisha gesi asilia futi za ujazo milioni 784 kwa siku na lina matoleo yapatayo 16 ambayo yamewekwa kimkakati kuruhusu uunganishwaji wa gesi kwa wateja maeneo bomba linapopita.

Bomba hili linapita katika vijiji takribani 136 ambapo suala la ulinzi limefanywa kuwa ni la kushirikiana kwa kuwawezesha wananchi wa vijiji husika kutoa huduma ya ulinzi katika mkuza wa bomba. Kwa kuzingatia kwamba suala la elimu na uhamasishaji ni suala endelevu, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambalo ndio msimamizi wa miundombinu hiyo limekuwa na utaratibu wa kutembelea vijiji husika na kutoa elimu juu ya umuhimu wa miundombinu hiyo kwa Taifa na namna ya kung’amua hatari na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wanakijiji wa Somanga Simu, Afisa Uhusiano wa TPDC, Ndg. Malik Munisi alisema “TPDC inatambua mchango wa kizalendo unaotolewa na wakazi wa maeneo bomba la gesi linapopita, inatambua kwamba mlinzi wa kwanza wa miundombinu hii ni mwananchi na hivyo tutaendelea kushirikiana nanyi kila wakati kuhakikisha miundombinu hii inaendelea kuwa salama na kudumu kwa kipindi kirefu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho”. Nae Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka TPDC, Ndg. Oscar Mwakasege alieleza namna ambavyo TPDC hujihusisha na dhana ya uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility-CSR) na kusisitiza kwamba maeneo ya kipaumbele katika kuwajibika kwa jamii ni masuala yahusuyo afya, elimu, maji na michezo. Ndg. Mwakasege alitoa mfano wa maeneo ambayo tayari TPDC imewajibika kwa jamii kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Marendego, ujenzi wa matundu ya vyoo shule ya msingi Kilwa Kivinje, kisima cha maji safi kijiji cha Njia Nne na maeneo mengine lukuki ambayo miundombinu ya gesi ipo au inapita.

Nae Mwenyekiti wa Kijiji cha Somanga Simu, Ndg. Athumani Mkumbaya alionyeshwa kufurahishwa kwa namna ambavyo TPDC na Songas wanavyojitahidi kuwashirikisha wanakijiji katika ulinzi wa bomba na pia kuwasaidia katika changamoto za kijamii zinazolenga kukuza ustawi bora wa jamii. Akizungumza wakati wa kikao cha hadhara, Ndg. Mkumbaya alisema “pamoja na michango mbalimbali tunayoipata kutoka kwa watu wa gesi, ombi letu kubwa kwao kwa sasa ni ujenzi wa shule ya sekondari, watoto wetu maeneo ya Somanga wanalazimika kwenda umbali mrefu kufika shule ya sekondari ambayo iko kata ya Muhoro”.

Nae Ndg. Elias Muganda, Afisa Usalama Mwandamizi kutoka GASCO anasema “TPDC kupitia kampuni tanzu ya GASCO imeingia mikataba ya ulinzi baina yake na vijiji 136 linapopita bomba, katika mikataba hii, kijiji kina majukumu makuu matatu, kwanza kusafisha mkuza, pili kulinda mkuza dhidi ya hatari na wavamizi na tatu kutoa taarifa pale kunapokuwa na jambo linaloenda kinyume na taratibu”. Ndg. Muganda anaeleza kwamba zoezi la kupita vijijini na kuwakumbusha juu ya masuala ya usalama wa bomba na faida za miundombinu hiyo ni endelevu kwani bila kufanya hivyo binadamu husahau na yakitokea madhara hasara itakuwa ni ya Taifa zima.

TPDC kupitia kampuni tanzu ya GASCO inasimamia miundombinu ya gesi asilia ambayo inajumisha mitambo ya kuchakata gesi iliyopo Madimba (Mtwara) na Songo songo (Lindi) pamoja bomba la kusafirisha gesi hiyo kutoka inapozalishwa hadi sokoni. Kwa mujibu wa taarifa kutoka TPDC, takribani megawati 831 za umeme katika gridi ya Taifa zinazalishwa na gesi asilia, hivyo suala la ulinzi wa miundombinu ya gesi ni suala ambalo linafanywa kwa ueledi wa hali ya juu kwa kuzingatia umuhimu wa kimkakati ambao mradi huu unabeba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: