Napenda kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kugundua kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji Bw. Brighton Kilimba alitoa taarifa za uongo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Magufuli kuwa gari ya wagonjwa ya Kituo cha Afya Ikwiriri haiwezi kutembea kwa sababu ni mbovu na inahitaji matengenezo makubwa.

Nikiwa mtumishi wa Wilaya hii niliumia sana kwa sababu nilikuwa najua ni uongo wa mchana kweupe na niliumia zaidi kwa kuwa aliyekuwa anadanganywa ni Rais wangu ninayempenda Dk. John Pombe Magufuli.

Hata hivyo nilifurahi muda mfupi baadaye nilipomuona kwenye mitandao ya kijamii Bw. Brighton Eliud Kilimba, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji akiwa kwenye pingu na bango linaonesha anatuhumiwa kumdanganya Rais. Nikasema kweli vyombo vya ulinzi na usalama sasa hivi vipo makini na havijalala.

Ukweli ni kwamba gari ya wagonjwa ya Kituo cha Afya Ikwiriri ipo na viongozi waliamua tu kuipaki wakati wananchi wanahangaika kupeleka wagonjwa wao Jijini Dar es Salaam pale wanapohitaji matibabu ya rufaa. 

Gari hilo ni zuri, ni aina ya Toyota Landcruizer namba STL 940, ni gari imara na limekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi kabla viongozi hawajaamua kulipaki na kuwaacha Wananchi wanahangaika kukodi magari kwa gharama kubwa na wakati mwingine kupanda bodaboda, ni jambo la kusikitisha sana kwa viongozi kutotekeleza wajibu wao kiasi hiki.

Kumbe siku ile Mheshimiwa Rais alipopita Rufiji na kulalamikiwa na wananchi juu ya ukosefu wa gari la wagonjwa, gari lilikuwepo na lilikuwa limetelekezwa katika Kituo cha Afya Ikwiriri likiwa halina tatizo lolote zaidi ya kuhitaji kufanyiwa service ya kawaida ya kubadilishwa oil na pengine kubadili matairi yake.

Kaimu Mkurugenzi Bw. Kilimba alipokuwa anamdanganya Rais kuwa gari ni bovu sana na haliwezi kutembea, Rais kwa machale akaamua kuagiza gari hilo lipelekwe TEMESA mara moja, nikajua hapa siri lazima itafichuka. 

Kwa kuwa gari halikuwa gereji kama Bw. Kilimba alivyosema hadharani, alichofanya Bw. Kilimba ni kupiga simu na kuagiza gari hilo lipelekwe gereji mara moja ili maafisa watakapofuatilia wakute lipo gereji, jamaa wa gereji waliposikia hivyo machale yakawacheza wakakataa kulipokea na ndipo maafisa wakagundua kuwa gari halikuwa gereji ambako Rais aliambiwa na halikuwa bovu kama Rais alivyoambiwa. Ni michezo tu ya viongozi.

Navipongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama kwa kugundua mchezo huu, na kisha kumkamata na kumweka ndani Bw. Kilimba ambaye ni Afisa Kilimo wa Wilaya.

Aidha, nampongeza Rais Magufuli kwa hatua alizochukua siku ileile hata kabla hajafika Dar es Salaam kwa kumtumbua Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Bw. Juma Njwayo ambaye ndio alikuwa anaongoza kutoa taarifa za uongo kuhusu ubovu wa magari. Hawa wote ni tatizo kubwa sana hapa Rufiji na yapo mengi ya hovyo wanayafanya, endapo uchunguzi wa kina utafanyika yatabainika vizuri.

Naamini hili litakuwa funzo kwa viongozi wengine kuwajibika ipasavyo katika kuwatumikiwa wananchi kama ambavyo Mheshimiwa Rais Magufuli anasema kila siku, kuwatumikia wanyonge vizuri badala ya kuwaacha wanahangaika wakati Serikali inajitahidi kuhakikisha inapeleka huduma kwa wananchi.

Msimamo wa Mheshimiwa Rais wa kuagiza gari hilo litengenezwe ndani ya wiki 1 na wakati gari linatengenezwa gari la Mkurugenzi ndilo litumike kubeba wagonjwa ni ujumbe tosha kuwa sisi watumishi ni lazima tuweke maslahi ya wananchi mbele na tuwatumikie kama ambavyo tunapaswa kufanya.

Asante Mheshimiwa Rais kwa uongozi wako makini unaojali watu hasa wanyonge.

Ni mimi Mtumishi
Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
02 Agosti, 2020.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: