Na Janeth Raphael - MichuziTv
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wananchi wanaomiliki silaha kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote za kisheria na vibali vinavyohitajika kabla ya Agosti 30, 2026, akieleza kuwa operesheni maalum ya ukaguzi wa silaha itaanza mara baada ya muda huo.
Chalamila ametoa agizo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo , akisisitiza kuwa wamiliki ambao kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kusahau au kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu, hawajakamilisha malipo ya vibali au hatua nyingine za kisheria, wanapaswa kutumia muda uliopo kufika katika mamlaka husika na kurekebisha hali hiyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha silaha zinazomilikiwa na wananchi katika Mkoa wa Dar es Salaam zinakuwa na kumbukumbu na vibali halali vinavyotambulika kisheria, kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo.
Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka watu wanaomiliki silaha bila kufuata sheria kuzisalimisha kwa hiari katika Jeshi la Polisi au kituo cha Polisi kilicho karibu kabla ya operesheni kuanza. Amesisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia wahusika kuepuka kukumbana na hatua za kisheria zitakazochukuliwa baada ya ukaguzi kuanza.
Aidha, Chalamila ametoa mwito kwa familia ambazo ndugu zao wamefariki huku wakiacha silaha zenye vibali halali kuhakikisha hazizifichi wala kuzihamisha bila kufuata utaratibu. Badala yake, amewataka kuwasilisha taarifa pamoja na silaha hizo kwa mamlaka husika ili kupata maelekezo ya kisheria kuhusu namna ya kushughulikia umiliki huo.
Kuhusu silaha zinazoripotiwa kuibiwa, amewataka wamiliki kutoa taarifa Polisi na kufuata taratibu zote zinazohitajika. Amesisitiza kuwa silaha hizo zinapopatikana, wahusika hawapaswi kuzificha au kuendelea kuzitumia bila kufuata maelekezo ya mamlaka.
Chalamila amesisitiza kuwa Agosti 30, 2026 ndiyo mwisho wa muda uliotolewa kwa wamiliki kuhakikisha wanakamilisha taratibu zao, akieleza kuwa baada ya tarehe hiyo operesheni maalum ya ukaguzi itaanza na yeyote atakayebainika kumiliki silaha kinyume cha sheria atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Amewataka wananchi kutotumia muda uliobaki kupuuza agizo hilo, bali kuhakikisha mapema kuwa umiliki wa silaha zao uko katika hali halali na unaotambulika na mamlaka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha udhibiti na usalama wa silaha katika Mkoa wa Dar es Salaam.



Toa Maoni Yako:
0 comments: