Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imewataka wanafunzi waliopata nafasi ya kurudi kusoma kupitia mfumo usio rasmi pamoja fani mbalimbali kutumia nafasi hizo kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu ili waweze kufikia malengo yao waliyojiwekea.
Hayo yamesemwa wakati wa maadhimisho ya Kisomo ya Juma la Elimu ya watu wazima ngazi ya Halmashauri yaliyofanyika tarehe 01/09/2026 katika Viwanja vya Stendi ya zamani vilivyopo Kata ya Mailimoja, Manispaa ya Kibaha.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Elimu Bi Theresia Charles amesema wanafunzi wanatakiwa kuwa na nidhamu , kwa sababu nidhamu katika maisha itakusaidia kukufikisha mbali kwenye malengo yao.
Bi Theresia amewapongeza na kuwataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao waliopo majumbani , waliokatisha shule kwa sababu mbalimbali kurudi shule na kupata elimu hiyo ambapo inatolewa katika shule na vituo ambavyo vipo chini ya serikali.
"Vijana tusitegemee kuajiriwa pekee, bali tutumie mafunzo na ujuzi tunaoupata kujiajiri na kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi,”amesema Bi Theresia
Aidha, amewahimiza vijana waliopata mafunzo mbalimbali kuwahamasisha vijana wenzao kujiunga na mafunzo hayo ili nao waweze kupata ujuzi utakaowasaidia kujitegemea na kuboresha maisha yao
Ameongeza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu wanafunzi kurudi kusoma kwa mfumo usio rasmi na umeleta mwanga kwa vijana ambapo kwa sasa wanapata elimu na ujuzi bila malipo.

Naye, Afisa Elimu Watu Wazima Msingi Manispaa ya Kibaha, Bi. Juliana Francis Mwakatenya amesema MUKEJA ni ambao ni mpango wa Uwiano kati ya Elimu na Jamii na unahusisha watu wazima kuanzia mikaa 19 na kuendelea ambapo wanapata mafunzo ya Kisomo chenye manufaa (KCM) ambapo watu wazima wasiojua kusoma kusoma, kuandika na kuhesabu hufundishwa na wakati huo hujifunza ujasiriamali na kuendesha miradi mbalimbali ya kisomo cha kujiendeleza (KCK) ili kujikwamua kiuchumi.

Bi. Juliana amesema , kwa mwaka 2026, kuna wanafunzi 57 wa KCM kutoka kwenye madarasa 5 ikiwemo darasa la Gereza la Mkuza na KCK 145 kutoka kwenye vikundi 20 vya MUKEJA.
Hata hivyo ameongeza kuwa, wana wanafunzi 94, wanaofanga mtihani wa kidato cha pili (Qualifying test) na wanafunzi 283 wanaofanya mtihani wa kidato cha nne ( Private candidate) pamoja na wanafunzi 66 wanaopata ujuzi kutoka mradi wa IPOSA ulipo Shule ya Mamlaka.
Maadhimisho hayo yameshirikisha vikundi mbalimbali vilivyoonesha bidhaa na kazi zao za ubunifu. Kila kikundi kilipata fursa ya kuelezea bidhaa na kazi wanazofanya, pamoja na kutoa ushuhuda kuhusu namna elimu, mafunzo na ujuzi walioupata ulivyowasaidia katika shughuli zao za kila siku na kujikwamua kiuchumi.







Toa Maoni Yako:
0 comments: