Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Joelson Mpina akimwangalia farasi anayetumika kwenye doria katika ranchi ya Kalambo Mkoani Rukwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh Luhaga Joelson Mpina akiangalia nyama inayochakatwa katika kiwanda cha SAAFI mkoani Rukwa kushoto kwake ni mmiliki wa kiwanda hichi Dkt Chrisant Mzindakaya.
Kundi la Ng'ombe bora katika ranchi ya Kalambo mkoani Rukwa.

NA JOHN MAPEPELE, RUKWA.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina ametangaza neema kwa kwa kugawa ekari 972, 500 za ardhi ajili ya wafugaji wanaotangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao ili kupata ufumbuzi wa kudumu ambao utamaliza kabisa migogoro baina ya wafugaji na wakulima iliyodumu kwa miaka mingi na kusababisha uvunjifu wa amani.

Akizindua zoezi la ugawaji wa ardhi hizo kwa wafugaji nchini katika Ranchi ya Kalambo wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Waziri Mpina amesema uamuzi huo wa Serikali umekuja kufuata wafugaji wengi nchini kuhangaika kila mahali kutafuta malisho na kusababisha migogoro mingi baina ya wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi.

“Pia wafugaji wengi walipata harasa kubwa kwa mifugo yao kutaifishwa kutozwa faini kubwa na hata mingine mingi kufa kutokana na kukamatwa kisha kushikiliwa kwa muda mrefu bila huduma muhimu ikiwemo maji, malisho na matibabu kwenye hifadhi mbalimbali za taifa nchini.” Alisisitiza Mpina.

Alisema hadi sasa ekari 25,000 zenye uwezo wa kuhifadhi mifugo 6,000 katika Ranchi ya Kalambo mkoani Rukwa wafugaji zimemegawiwa ambapo na jumla ya ng’ombe 3,000 wameshaingia kwenye ranchi hiyo wakati Serikali na wafugaji wenyewe wakiendelea kutafuta suluhisho la kudumu la kupata malisho.

Amewataka wafugaji wote wanaohangaika kutafuta malisho kutumia fursa hiyo iliyotangazwa na Serikali ya uwepo wa maeneo kwa ajili ya kulishia mifugo ili wawe karibu pia huduma za tiba na chanjo pindi mifugo yao inapopata maradhi.

Akiwa katika mkutano wa pamoja baina ya Rachi ya Kalambo na wawekezaji Waziri Mpina alipongeza Timu maalum aliyoiunda ya kutatua migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi kwa kufanikisha zoezi la upimaji na ugawaji wa ardhi hiyo kwa wafugaji pamoja na kutatua migogoro yote iliyokuwepo baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.

Aidha ailiiagiza Timu hiyo kuhakikisha kwamba inazunguka nchi nzima kwenye migogoro na kuitatua ili kuboresha mifugo iweze kuchangia katika viwanda hapa nchini.

Pia alimwagiza Katibu Mkuu Mifugo kuhakikisha ukaratabi wa kituo cha uchunguzi wa magonjwa ya wanyama cha Kanda ya Kusini Magharibi kinakamilika ifikapo Februari mwakani ili kutokana na mikoa ya Katavi, Rukwa kutokuwa na kituo hicho licha ya kuwepo mifugo mingi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Halfan Haule alisema kutokuwepo kwa maeneo ya malisho na maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo kumekuwepo na migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi na kumshukuru Waziri Mpina kwa uamuzi wa kugawa vitalu kwa wafugaji.

Alisema Mkoa wa Rukwa umekuwa ukikabiliwa na magonjwa ya mifugo ikiwemo homa ya nguruwe(ASF), Homa ya Mapafu ya Ng’ombe(CBPP), Homa ya mapafu ya mbuzi(CCPP), Ugonjwa wa miguu na midomo(FMD), Ugonjwa wa mapele ngozi (LSD), Ugonjwa wa kichaa cha mbwa na ugonjwa wa mdondo (ND).

Katibu wa Umoja wa Wafugaji Ranchi ya Kalambo, Benuel Benzeth aliishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kugawa maeneo hayo ya Serikali kwa wafugaji katika kipindi ambacho wanaendelea kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto ya malisho.

Alisema mifugo yao mingi imekufa na mingine kudhoofika kutokana na kukamatwa na kushikiliwa kwenye hifadhi bila matunzo na wakati wote Serikali haijawahi kuchukua hatua za kuwasaidia wafugaji na kumshukuru Waziri Mpina kwa uamuzi huo ambao umewezesha mifugo mingi kupona na kuendelea na uzalishaji.

Awali akizungumza mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Nyama cha SAAFI kilichopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, Waziri Mpina amesema Serikali inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza kufanya kazi haraka ili kusaidia upatikanaji wa mifugo takribani milioni 6 iliyoko katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Songwe na Mbeya.

Hivyo changamoto zote zinazokikabili kiwanda hicho zitatatuliwa haraka ikiwemo ukosefu wa mtaji pamoja na uongozi wa kuendesha kiwanda hicho jambo linalosababisha kiwanda hicho kusimama kwa muda mrefu licha ya kuwa na mitambo bora na ya kisasa ya uchinjaji na usindikaji wa nyama katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Waziri Mpina amesema ni jambo la fedheha kuona kiwanda hicho chenye miundombinu yote kuendelea kubaki katika hali hiyo huku wafugaji wakiendelea kuhaha kutafuta soko la mifugo hali inayosababisha asilimia 80 ya mifugo hiyo kutoroshwa kwenda nchi za jirani na kwenda kuyanufaisha mataifa hayo.

Hali hiyo inaifanya Tanzania kugeuzwa kuwa malisho ya mifugo hiyo huku rasilimali hizo zikishindwa kunufaisha nchi kimapato jambo ambalo Serikali ya awamu ya tano haiwezi kukubali liendelee.

Waziri Mpina pia alimpongeza Mwekezaji wa kiwanda hicho, Dk. Chrisant Mzindakaya kwa ujasiri na uamuzi mkubwa wa kubuni wazo la kuanzisha kiwanda hicho kwa gharama ya sh bilioni 9 na kuwepo na eneo la malisho zaidi ya hekta 6,000 kwani watu wengi wanaweza kukopa fedha na kisha kushindwa kutekeleza mipango yao kwa mujibu wa mpango kazi alioombea mkopo.

Hivyo aliagiza taasisi zote za Serikali kuhakikisha changamoto zote zinakwisha ili kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza kazi mara moja na kwamba kama uvunaji wa rasilimali za mifugo hauko vizuri ni kipimo cha uwajibikaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyopewa dhamana ya kusimamia ukuaji wa sekta hiyo.

Kwa upande wake Mwekezaji wa kiwanda, Dk Chrisant Mzindakaya alisema licha ya kiwanda chake kufanya kazi lakini uzalishaji wake ni mdogo kutokana na changamoto ya mtaji na uendeshaji wa kiwanda na kumshukuru Waziri Mpina kwa kutembelea kiwanda na kutangaza msimamo wa Serikali katika kukinusuru kiwanda hicho.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: