Articles by "KILIMO"
Showing posts with label KILIMO. Show all posts
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, ameshangazwa na kiwango cha ubunifu wa teknolojia zinazobuniwa na kuzalishwa na kampuni ya Mati Technologies baada ya kutembelea banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Kilimo (Nane Nane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Mhe. Pinda alitembelea banda hilo leo na kupokea maelezo kutoka kwa viongozi na wataalamu wa Mati Technologies kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo katika kubuni na kutengeneza teknolojia zinazolenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo na maeneo mengine ya maendeleo.

Katika ziara hiyo, alikagua teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa na kampuni hiyo, ikiwemo ndege nyuki zinazotumika kunyunyiza viuatilifu na mbolea mashambani kwa usahihi, haraka na ufanisi mkubwa, pamoja na mifumo mingine ya kisasa ya kiteknolojia inayolenga kuboresha uzalishaji wa kilimo.

Baada ya kushuhudia namna teknolojia hizo zinavyofanya kazi, Mhe. Pinda alisema ameridhishwa na hatua kubwa ya ubunifu iliyofikiwa na wataalamu wa Kitanzania.
“Ni jambo la kujivunia kuona Watanzania wakibuni na kuzalisha teknolojia za kisasa zinazotoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali za maendeleo, hususan katika sekta ya kilimo,” alisema.

Alisema maendeleo hayo yanaonesha uwezo mkubwa wa wataalamu wa ndani katika kubuni teknolojia zinazokidhi mahitaji ya nchi na kuchangia kukuza uchumi kupitia sekta ya kilimo na viwanda.
Aidha, aliipongeza Mati Technologies kwa kuwekeza katika utafiti, ubunifu na uzalishaji wa teknolojia za ndani, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono ili kuharakisha maendeleo ya taifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Kitanzania katika soko la ndani na kimataifa.

Kwa upande wake, uongozi wa Mati Technologies ulisema kampuni itaendelea kubuni na kuzalisha teknolojia zenye ubora wa hali ya juu zitakazorahisisha shughuli za uzalishaji, kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za uchumi.
Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na teknolojia, huku yakivutia maelfu ya wananchi, wakulima, wawekezaji, wanafunzi na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia ubunifu wa teknolojia zinazozalishwa hapa nchini, Mati Technologies inaendelea kujijengea sifa kama moja ya kampuni zinazochochea matumizi ya sayansi, teknolojia na utafiti katika kuongeza tija ya uzalishaji na kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania.


Na Mwandishi Wetu, Kibaha

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameitaka Tanzania Biotech Production Ltd (TBPL) kuhakikisha inazingatia ubora katika uzalishaji wa mbolea hai ili kukidhi mahitaji ya soko na kulinda afya za watumiaji.

Kapinga alitoa kauli hiyo mjini Kibaha wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya TBPL, kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), na taasisi mbalimbali ikiwemo TFC, TARI, TFRA na TPHPA.

Alisema mbolea hai ina fursa kubwa sokoni kutokana na kutokuwa na kemikali hatarishi na uwezo wake wa kuhifadhi mazingira, jambo linaloifanya kuwa salama kwa afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.

“Mbolea hii ina soko kubwa na mchango wake katika kulinda mazingira ni muhimu. Hivyo, ni lazima ubora wake uzingatiwe wakati wote ili kuendelea kujenga imani kwa watumiaji,” alisema Kapinga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mwendeshaji wa NDC, Nicolaus Shombe, alisema uzalishaji wa mbolea hai unaotarajiwa kufanywa na kiwanda hicho utachochea mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kuongeza tija na kuhamasisha matumizi ya pembejeo rafiki kwa mazingira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBPL, Mhandisi Rafael Moya, alisema mbolea hiyo itasaidia kupunguza matumizi ya kemikali katika shughuli za kilimo, huku ikichangia kulinda afya za wananchi na mazingira.

Alisema kipaumbele cha taifa kwa sasa ni kuhakikisha uzalishaji wa chakula unafanyika kwa njia salama na endelevu, huku wakulima wakinufaika na teknolojia na pembejeo zinazolinda afya na mazingira.
Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Kilimo Hai Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo (TOAM) linaratarajia kufanya Mkutano MKuu wa Nne Machi 3 hadi Machi 5 ,2026 jijini Dodoma kwa ajili ya kujadili na wadau kuhusiana na kilmo hai nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bakari Mongo amesema mkutano huo ulitakiwa kufanyika Januari mwaka huu lakini waliahirisha kutokana sababu mbalimbali na kuahidi malengo waliotaka yatafikiwa katika mkutano huo wa mwezi machi.

Amesema wadau wajitokeze katika kufanikisha mkutano huo kwa kutoa udhamini katika kukidhi matarajio ya kilamo hai nchini.

Mongo amesema Mkutano Mkuu huo unatarajia kuwa wadau 400 wakiwemo wakulima, Watunga Sera, Watafiti, Wasomi, Sekta Binafsi, Vyama vya Kiraia pamoja na Wabia wa Maendeleo.

Mongo amesema kuwa mkutano huo ni fursa ya kubadilisha maarifa na uzoefu ili kuboresha mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula cha kutosha ,kulinda mazingira na kuongeza mazao kwa wakulima nchini.

Aidha amesema katika mkutano huo wataangalia maudhui ya Usalama wa Chakula na Lishe Mbinu na Teknolojia za Kilimo Ikolojia Hai na Ustamilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ,Manufaa ya Kiuchumi ya Kilimo Ikolojia Hai kwa Wakulima ,Maendeleo ya Kiteknolojia na Mfumo ya Uzalishaji wa Chakula pamoja na Mazingiea ya Kisera na Mifumo katika kuendeleza Kilimo Ikolojia Hai.
Na Mwandishi Wetu.

KAMPUNI ya Mati Super Brands Ltd kupitia tawi lake la Mati Technology imezindua teknolojia mpya ya ndege nyuki (drone) zinazotengenezwa nchini, zenye uwezo wa kuboresha sekta ya kilimo na huduma nyingine za kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mati Group of Companies, David Mulokozi, amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika uzalishaji wa drone zinazotumika kunyunyizia dawa mashambani, kupima maeneo, kupanda mbegu, kusafirisha mizigo na kusaidia kaguzi mbalimbali.

Mulokozi ameeleza kuwa drone hizo zitauzwa kuanzia Shilingi milioni 17, bei ambayo ni nafuu ukilinganisha na gharama kubwa za kuagiza kutoka nje ya nchi. Pia, kampuni ipo katika mazungumzo na benki ili kuwezesha wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kumudu teknolojia hiyo.


“Tumeona changamoto kubwa inayowakabili wakulima hasa kwenye upuliziaji wa dawa. Kwa kutumia drone hizi, hekari moja inaweza kunyunyiziwa dawa ndani ya dakika saba pekee, jambo linaloongeza ufanisi na kulinda afya za wakulima,” alisema Mulokozi.

Aidha, amebainisha kuwa uzalishaji wa drone hizo utatoa ajira kwa wahandisi wa Kitanzania na kufanikisha uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa wataalamu wa kigeni
Kwa upande wake, Afisa Ushirika kutoka ofisi ya Msajili mkoa wa Manyara, Godamen Merinyo, amesema teknolojia hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa mazao kama mbaazi ambayo hukua kwa urefu na kufanya unyunyiziaji wa dawa kuwa mgumu na wa gharama kubwa.

“Hii itasaidia kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kuimarisha vyama vya ushirika. Tutaanza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya teknolojia hii,” alisema Merinyo.
Naye Afisa Kilimo wa mkoa wa Manyara, Paulo Eugine, amesema drone hizo zitasaidia kuwalinda wakulima dhidi ya madhara ya kiafya yaliyokuwa yanawapata kutokana na kutumia pampu za mgongoni.

“Sasa mkulima ataweza kutumia remote control bila kuingiliwa na sumu, jambo linaloimarisha usalama na afya zao,” alisisitiza Eugine.

Hatua hii ya Mati Technology inatarajiwa kuchochea mapinduzi ya kilimo nchini na kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza tija kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Na Ferdinand Shayo, Arusha.

Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC) kimetoa mafunzo ya utengenezaji wa majiko ya nishati safi pamoja na miundombinu yake kwa Maafisa wa Jeshi la Magereza kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania ili kuwawezesha kutumia nishati hiyo na kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni ambayo yanasababisha uharibifu wa mazingira .

Akizungumza katika hafla ya kufunga Mafunzo hayo ,Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania ambaye ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Manyara Felichisim Masawe amempongeza Mkuu wa Jeshi hilo kwa kutoa Maafisa waliopatiwa mafunzo na CAMARTEC ili waweze kutengeneza majiko yanayotumia gesi ya bayogesi pamoja na sufuria.

Masawe amesema kuwa Jeshi hilo limekua mstari wa mbele kutekeleza agenda ya nishati safi kwa kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka taasisi zenye watu Zaidi ya 100 kuanza kutumia nishati safi ambapo magereza wameanza tangu mwaka 2024.

Kaimu Mkurugenzi wa CARMATEC Boniface Chatila amelitaka Jeshi la Magereza kuendelea kushirikiana na kituo hicho ili kupata mahitaji yote muhimu ya mitambo ya nishati safi pamoja na kutoa ujuzi kwa Maafisa Magereza ili kueneza Teknolojia hizo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo CAMARTEC Peter Mtoba amesema kituo hicho kimesaini makubaliano ya kutengeneza majiko Zaidi ya 300 ya nishati safi yatakayosambazwa kwenye magereza mbali mbali nchini ili kuhakikisha wanatumia nishati safi na kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Na Mwandishi Wetu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametumia ziara yake nchini Belarus kunadi fursa za uwekezaji katika maeneo manne ya kipaumbele ya Serikali ya awamu ya sita ambayo ni kilimo, afya, madini na ulinzi & usalama.

Mhe. Waziri Mkuu katika siku mbili za ziara yake, tarehe 22 na 23 Julai 2025 ametembelea kampuni kubwa nane zenye nguvu ya mitaji jijini Minsk na kuzihakikishia utayari wa Serikali ya Tanzania kushirikiana nazo kwa kuzipatia kila aina ya msaada zitakapokuja Tanzania kuwekeza.

Kwenye eneo la kilimo, Mhe. Waziri Mkuu alikutana na viongozi wa kampuni ya AFTRADE ambayo tayari ipo nchini na kuwasisitiza kuongeza kasi katika kuendeleza kilimo hususan kuwa na programu za kuwasaidia wakulima wadogo mitaji, utafiti na mafunzo ili kilimo kiweze kuwa na tija, kizalishe ajira na kuongeza usalama wa chakula nchini.

Katika eneo hilo la kilimo, Waziri mkuu pia alitembelea chuo cha kilimo cha Belarus na viwanda vya matrekta na kuvishawishi viwanda hivyo kufungua matawi nchini Tanzania.

Kuhusu chuo cha kilimo ambacho mafunzo yake huyafanya kwa vitendo zaidi, Waziri Mkuu aliomba Watanzania wapatiwe fursa za masomo katika chuo hicho ili waweze kuendeleza sekta ya kilimo nchini, watakapomaliza masomo yao.

Kuhusu Afya, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kampuni ya kuzalisha na kusambaza dawa na vifaa tiba ya Belmedepreparaty ambayo ni moja ya kampuni kubwa nchini Belarus. Kampuni hiyo inayozalisha bidhaa tofauti tofauti zaidi ya 1700 na kuuza ndani na nje ya nchi katika mataifa zaidi ya 24, iliridhia maombi ya Mhe. Waziri Mkuu na kuahidi kufanya ziara nchini Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.

Mhe. Waziri Mkuu alisema Belmedepreparaty ni kampuni sahihi kuja kuwekeza nchini kutokana na kutumia teknolojia ya kisasa ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya kimataifa.

Kwa upande wa sekta ya madini, Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza mitambo inayotumika kuchimba madini migodini na kukishawishi kiwanda hicho kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Kuhusu suala la Ulinzi na Usalama, Mhe. Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kutengeneza vifaa vya ukoaji na kuzima moto na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na kiwanda hicho ili kuondoa tatizo la uhaba wa vifaa hivyo nchini.

Waziri Mkuu amemaliza ziara yake na aliondoka Julai 24, 2025 kurejea nyumbani.
Na Mwandishi wetu- Morogoro

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepongezwa kwa kuendelea kufanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na faida kwa wakulima na wananchi kwa ujumla.

Pongezi hizo zimetolewa na, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua warsha kuhusu kuimarisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Kilimo leo tarehe 16 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Mbaraka Mshee - Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro.

Dkt. Yonazi alisema, hatua hiyo ni kutokana na Serikali kuongeza najeti ya Kilimo kwa miaka mitatu mfululizo kutoka bilioni 294 (2022/2023) hadi trilioni 1.241 (2025/2026) ambapo katika kufanikisha hilo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imezindua Programu na Mipango ya kufanikisha malengo hayo ambayo ni pamoja na Programu ya BBT, Agenda 10/30 na Agricultural Transformation Master Plan.

“Ninapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuboresha muundo wa Taasisi za Umma na kuanzisha Idara ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu na Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini katika ngazi zote nchini kwa lengo la kupima utendaji wa Serikali,” alisema Dkt. Yonazi.


Pia aliongeza kwamba, warsha hiyo itakayofanyika kwa siku tano itawezeshwa na wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa kushirikiana na Mtaalam Mbobezi kutoka Benki ya Dunia kuhusu dhana mbalimbali zikiwemo muundo wa kitaasisi wa Ufuatiliaji na Tathmini nchini, Mwongozo Elekezi wa Mwongozo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Utendaji wa Serikali (M&E Operational Manual).
“Mpango mwingine ni Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Mpango kazi wa Mwaka wa Wizara na Taasisi (M&E Plan), Mkakati wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (M&E Strategy) na Moduli ya kupima utendaji wa Wizara na Taasisi husika (M&E Performance Model). Aidha, ni muhimu kupima hali ya utayari wa kila Wizara na Taasisi zake,” alieleza .

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo alibainisha kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu imekasimiwa jukumu la kuratibu, kufuatilia, kutathmini na kupima utendaji wa serikali nchini hivyo ofisi imeendelea kuratibu shughuli hizo kwa kuandaa na kuwasilisha nyaraka muhimu zitakazowezesha ubora na ufanisi wa kazi za ufuatiliaji na tathmini.

“Ni muhimu kuvisimamia vitengo vyenu kutekeleza majukumu yao kwa kufuata miongozo ili kazi zetu ziwe na ubora unaotakiwa. Aidha, ni matarajio yangu kuwa nyaraka hizo zitawaongoza kuandaa nyaraka elekezi na tendaji kwa kuzingatia muktadha wa Wizara yenu ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yenu,” alibainisha.

Aidha, Dkt. Yonazi aliwasihi washiriki wa warsha hiyo kujadili masuala yote ikiwemo changamoto zinazoweza kusababisha kuwa na utekelezaji usioridhisha katika Wizara mbalimbali na Taasisi zake ikiwemo Wizara ya Kilimo pamoja na kupendekeza namna bora ya kuondokana na changamoto hizo.