Na Bashir Yakub.
+255 784 482 959

Nimeulizwa na watu wengi ikiwa agizo la Mhe. Waziri Mwakyembe kuhusu kumtia mbaroni mara moja DUDUBAYA kwa maneno yake dhidi ya marehemu Ruuge Mutahaba ikiwa ni sawa kisheria au si sawa.

Swali la msingi lilikuwa ni je kuna kosa la kutukana,kukashifu au kudhalilisha maiti hapa kwetu mpaka DUDUBAYA akamatwe ?. Hili ndilo swali la msingi nililoulizwa na wengi.

Jibu langu kwao lilikuwa ni NDIYO kosa hilo lipo. Kifungu cha 127 cha
Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 kimeeleza jambo hili.

Kifungu kinasema kuwa “mtu ambaye kwa makusudi atakuwa na nia ya kuumiza hisia za mtu mwingine yeyote, au kutukana dini ya mtu mwingine yeyote, akaivunjia heshima ya maiti ya binadamu(offers any indignity to human corpse) atakuwa ametenda kosa”

Swali ambalo siwezi kujibu ni ikiwa maneno ya DUDUBAYA ni ya aibu au yameivunjia heshima maiti/mwili wa RUGE.

Hilo ni suala la mahakama kupima uzito wa maeno yenyewe, kadhalika kuyatafsiri kwa tafsiri ya kawaida ya matumizi yake na kuona ikiwa yanajitosheleza kuitwa yenye kuvunja heshima ya maiti au hapana.

Hayo ni masuala ya mahakama, mimi kwangu ninaishia katika kusema kuwa kutamka maneno ya aibu,yenye kuvunja heshima dhidi ya maiti ya binadamu ni kosa hapa kwetu Tanzania.

Baada ya kuona uwepo wa kosa hilo, Swali jingine ni je kosa hilo lina adhabu?. Jibu ni NDIYO, kosa hilo lina adhabu.

Kifungu kinachoanzisha kosa hilo hakikutaja moja kwa moja adhabu ya kosa hilo. Isipokuwa sheria nyingine, Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai Sura ya 20, imetaja adhabu ya kosa hilo.

Jedwali la Kwanza, Sehemu ya 14 ya sheria hiyo inasema kuwa adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miaka 2 jela. Na inasema kuwa inaruhusiwa kumkamata mtu aliyetenda kosa hilo bila kuwa na hati ya kukamata(arrest warrant).

Na zaidi, sehemu hiyo inasema kuwa kosa hilo linapaswa kusikilizwa na mahakama za chini (subordinate courts) kwa maana ya mahakama ya hakimu mkazi, au mahakama ya wilaya, au ya mwanzo.

Hatujui mambo mengi ndiyo maana watu wameshangaa kuwa inakuwaje kuchoma moto tu unaenda jela maisha.

Apumzike kwa amani ndugu yetu Ruge Mutahaba.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: